Mimi ni Mama wa watoto wawili, nimeolewa na ndoa yangu ina miaka 6 sasa, mwaka jana nilikutafuta, nilikuambia kuwa nimepata kazi lakini mume wangu hataki nifanye. Baada ya kukuelezea hali ya mume wangu uliniambia niache ujinga nifanye kazi. Mume wangu yeye alikua anafanya kazi, lakini akaacha kwakua tu anasema hiyo kazi si ya hadhi yake anataka kufanya Biashara. Wakati huo Mama yangu alikua kafariki dunia hivyo kuna pesa ambazo watoto wote tulipata za mafao.
Mume wangu aliacha kazi na kuniambia nimpe hizo pesa lakini akaishia kwenda kuhonga akanidanganya kuwa katapeliwa kumbe kuna mwanamke ambaye alimnunulia gari kumbe ni mke wa mtu mume wake alikua mkoani. Alifumaniwa, akapigwa na kulazwa hospitalini miezi miwili, akiba yote niliyokua nayo ikaisha, nikapata kazi ndiyo akagoma nisifanye, uliniambia nisikubali, ni bora kumuambia aniache kuliko kuacha hiyo kazi.
Nilikusikia lakini Dada yangu aliniambia nisisikilize maneno ya watu yule ni mume wangu ni lazima kumtii. Kaka kweli niliacha ile kazi, ilikua ni kazi katika shirka moja hivi na ilikua na masalahi mazuri. Mume wangu alifurahi na kuniambia kuwa akipona atafanya Biashara na tutafanikiwa, lakini alipopona alinirudisha mimi nyumbani kwao akiniambia kwakua hana kazi basi nibaki kwao akatafute kazi kisha atakuja kunichukua.
Kaka nimekaa tangu mwaka jana nilipoongea na wewe mpaka sasa ni mwaka mzima, mume wangu hajageuka kunifuata na nikimuuliza ananiambia bado hajapata kazi. Lakini juzi nilikua instagram nikaona kuna mwanamke kampost mume wangu, nikamuuliza huyo mwanamke ni nani akasema ni rafiki yake, jana mwanamke kapost pete ya ndoa namuuliza ananiambia kuwa huyo mwanamke ni mwanamke wake lakini anamdanganya kuwa hana mke ili amsaidie kupata kazi kwani kwao huyo mwanamke wana pesa.
Ameniambia wamefunga ndoa ya kiserikali wakati sisi tuna ndoa ya Kanisani hivyo hata haitambuliki kisheria. Kaka naomba ushauri wako hapa, je mwanaume anaongea ukweli au, je ndoa ya kiserikali hatambulikiki? Ni kweli ananipenda au? Sina kazi sina hata pakwenda, nina watoto wawili nashindwa hata nikiondoka nitakua mgeni wa nani?
Nyumbani Baada ya Mama kufariki kabaki dada tu ambaye naye ana majanga yake kwenye ndoa yake, mwanaume kaniacha hapa na Mama yake, matumizi yenyewe ya shida, naomba ushauri wako Kaka kwani nimekwama kabisa.
USHAURI; Nilishakuambia tangu mwanzo, mwanaume anaogopa kama ukifanikiwa hutavumilia ujinga wake, lakini yeye ana mwanamke mwingine. Ndoa yake ya Kiserikali inaweza isiwe halali, anaweza kuwa anamdanganya huyo Dada lakini ukweli nikuwa, wanaishi pamoja na wana maisha yao. Dada unapaswa kujiangalia wewe na wanao, maisha ni mafupi ukikaa kulilia ndoa tu wakati mtu kashakuacha utachanganyikiwa, tafuta kazi mdogo wangu.
MREJESHO; Mara ya mwisho uliongea na mimi kwa uchungu kama mdogo wako, niliamua kufuata ushauri wako kutafuta kazi kimya kimya. Kaka sikumuambia mume wangu kuwa nimepoata kazi, nilimuomba kwenda nyumbani kwetu kusalimia, yaani ni kama alishangilia, nikamuambia ninaenda kwa Shangazi yangu kumsaidia Kazi za ndani akakubali.
Kaka baada ya kwenda kwetu si yeye wala ndugu zake walinitafuta, kumbe hata hakutafutiwa kazi na huyo mwanamke bali alikua kama anafugwa. Wanaishi wote na kachukua ndugu zake wamehamia huko. Nimefanya kazi na sasa hivi nina kipato changu Kaka. Nimekuja kwakua Mama mkwe kanitafuta eti anataka nirudi kwa mume wangu kwani huyo mwanamke anamharibu mtoto wao.
Nimekuja kuchunguza kumbe yule dada alimuambia kuwa hajaoa na si ndoa ya Kiserikali kumbe walifunga ndoa ya Kanisani na sababu ya Mama mkwe kunitafuta nikuwa, kumbe wamekamatwa kwa Mganga wakimloga huyo Dada, amewafukuza wote ile bado mwanaume kabaki hataki kuondoka ndiyo Mama yake eti anataka nikamtoke huko kwa mwanamke wake kwani kalogwa, nimerudi tena Kaka nifanyeje?