Dunia ya sasa kila mmoja wetu ni shahidi wa hili, matapeli au walaghai wa mapenzi wamekuwa ni wengi kuliko wale wenye mapenzi ya dhati. Ni nadra sana kumpata mtu sahihi kwenye ulimwengu huu uliojaa matapeli wa kila namna. Kuna ambao ni hodari wa kuwatumia wanawake, kuna wengine pia ni hodari wa kuwatumia wanaume. Bahati mbaya sana matapeli hawa wana mbinu za hatari.
Ukihisi umempatia na kumtambua katika mbinu hii, mwenzako kumbe ana mbinu nyingine. Mtu anakuja utadhani kweli ni muoaji kumbe wapi, tapeli tu. Anakuhadaa kwa maneno matamu, anakwambia anahitaji kuwa na wewe kwa maisha yake lakini baada ya muda anakuchenga. Anageuka kama kinyonga baada tu ya kupata kile anachokitaka. Wakati mwingine anakuwa anaongozwa na tamaa tu. Akishapata anachokitaka basi hakuna tena mapenzi. Anahamia kwa mtu mwingine na kukuacha solemba.
Hivyo basi, tunapaswa kuwa makini sana katika suala zima la uhusiano. Unapaswa kuwa makini kabla ya kuanzisha uhusiano na mtu. Unapaswa kumjua kiundani mhusika kabla ya kuzama penzini.
Sio unakutana leo tu na mtu anakulaghai, unamkubalia kesho tayari ameshakuwa mpenzi wako. Hujui anatokea wapi, ndugu zake ni kina nani au ana tabia gani wewe unabeba tu. Hii ni hatari sana, uhusiano mzuri ndugu zangu ni ule wa watu wawili ambao wamesomana kwa muda kidogo kama si muda mrefu.
Unapomjua mtu kwa undani angalau inakupa picha ya kule uendako. Unaweza kumfanyia tathimini na kujua kama anafaa kuwa mwenza wako au la. Acha papara za kuwa mpweke, wakati mwingine ni bora kuishi peke yako kuliko kuishi na mtu ambaye atakuwa ni pasua kichwa.
Mimi na wewe ni mashahidi juu ya matukio mabaya ya wapendanao yanayotokea katika dunia ya sasa. Watu wanauana, ukichunguza kwa makini wanaofanya matukio haya huwa na historia ya ukorofi au hata ujambazi.
Unaolewa au kuoa jambazi unategemea nini kwenye maisha yako? Jambo dogo tu ukimkosea mtu wa aina hiyo ni rahisi kukuua kwa risasi kama si kukukata mapanga. Mtu anakuwa hana ubinadamu, kukuua ni dakika tu. Wa nini mtu wa aina hiyo? Jifunze kukaa kwenye mazingira salama ya kuwa na watu wazuri.
Mathalan waweza kuwa karibu na watu ambao wana imani na hofu katika Mungu. Watu wa namna hiyo wapo katika maeneo fulanifulani, yatafute. Nako ukiwa pia si kwa kukurupuka. Ni vizuri pia ukamsoma mtu aliye karibu nawe kabla ya kuanzisha uhusiano.
Angalau umjue kidogo tabia, historia yake na hata watu wanaomzunguka. Mfanye awe rafiki kwa muda fulani kabla ya kuwa mpenzi wako, mchumba na hata mumeo au mke wako.