Kaka naomba ushauri wako kwani nahisi kuchanganyikiwa, mimi ni mwanamke wa miaka 35, sijaolewa lakini miaka 10 iliyopita nilikua kwenye mahusiano na huyu Kaka. Tulikua tunapendana sana lakini ilipofika suala la kuona wazazi wake walinikataa kwasababu kuna mwanamke alimpa ujauzito hivyo wakamlazimisha amuoe, niliumia sana lakini alinihakikishia kuwa ananipenda na yule mwanamke kamuoa kwa kulazimishwa.
Pamoja na kuoa lakini muda mwingi alikua kwangu, alikua ananijali, ananihudumia kuliko hata mke wake, walikua wanagombana na kila nikimuambia kitu mimi ananisikiliza. Kaka nimekaa na huyu mwanaume tangu kaoa nina miaka 25 mpaka sasa hivi, yeye ana watoto watatu ambao alizaa na mke wake. Mimi kila nikibeba mimba yake alikua ananiambia nitoe kwani muda si sahihi.
Nimetoa mimba zake 9 mpaka sasa hivi nimechoka, ananiambia ananipenda lakini sijui ananifanyia nini Kaka kila nikibeba mimba atafanya juu chini mpaka naitoa. Mwaka jana mke wake alifariki dunia, Kaka nilijua kuwa labda baada ya mke wake kufariki dunia atanioa mimi eti kaenda kufunga ndoa kimya kimya na mwanamke mwingine hata mwaka mke wake hajamaliza.
Nimeumia sana nimemuambia kuwa tuachane lakini ananiambia kuwa ananipenda na hajui ni kwanini ameenda kuoa. Kaka nimechoka natamani kumuacha huyu mwanaume lakini Kaka kwa umri huu nitapata mwanaume kweli, nilikua nafanya kazi aliniachisha, yaani nahisi kuchanganyikiwa, maisha yangu ni kama yamesimama, naomba unisaidie Kaka nifanye nini?
JIBU LANGU; Najua kila mtu atakushangaa na kukuona chizi, lakini baada ya kuongea na wanawake napenda kukuambia kuwa wewe si chizi yaani naona vitu vingi wanawake hufanya kwaajili ya mapenzi mpaka shetani mwenyewe anashangaa. Dada wewe ni mhanga wa mapenzi ya huyo mtu, umekua teja wake na si rahisi kutoka kama wengi wanavyodhani ila ukiamua utatoka.
Kwanza kabisa unapaswa kujua kuwa huyo mwanaume hakupendi bali kuna kitu anakutumia, unaweza usikione lakini kuna kitu anapitia kiasi kwamba anahitaji mwanamke wa kunyanyasa, wa kumdhalilisha na kumuharibia maisha ili nayeye ajione maisha. Mwanaume anapomuacha mwanamke na kumrudia tena kuna kanguvu flani anakapata ambako kanampa kaunyama flani na kujiona kama Mungu flani.
Dada una miaka 35, hujafa bado, una nafasi ya kurekebisha. Kwa imani yako piga magoti muambie Mungu, nimekosea ninyanyue tena, kisha nyanyuka chukua simu yako mpigie huyo mwanaume muambie nimekuacha. Atajiongelesha sana lakini usimuambie kuwa kakuumiza, cha kumlalamikia kuwa amekuharibia maisha bali muambie nimekuacha kwakua nimekua mtu mpya na nimetambua thamani yangu.
Baada ya hapo nipigie simu, wenzako nikiwaambia hivi hawanipigii ila wewe nipigie, kuna kitu kitakua kimekukaba, kuna mawazo yatakujaa, utawaza hivi nitapata mwanaume mwingine kweli, nimetoa mimba tisa hivi nina kizazi, hivi Mungu atanipa mtoto tena. Hata usijali, miaka ni namba na dhambi tumeumbiwa wanadamu, tutaongea utakata simu utaingia chooni utalia kisha utatoka.
Wiki yako itakua ngumu sana, mwezi huo utakua mgumu sana, utatamani kumpigia simu mara mia, utatamani kuomba msamaha. Kwakua ni mjeuri basi hatakutafuta, atakaa wiki hakutafuti, mwezi hakutafuti, hiyo itakuuma zaidi, utachanganyikiwa kwamba inamaana amenisahau, mbona hanitafuti.
Lakini yeye atafanya hivyo akiamini kuwa wewe ni mdhaifu, kwamba huwezi kuishi bila yeye na utamtafuta ila usifanye hivyo. Tafuta kitu cha kukufanya uwe bize, inga Youtube, jifunze kupika, jifunze kushona, angalia vitu vingine, ingia angalia magonjwa ya ajabu, angalia namna watu wanavyoteseka, kwa kifupi kuwa bize na kitu flani nakuahidi utamsahau.
Credit IDD Makengo