HABARI ABIRIA zaidi ya 40 waliokuwa wakisafiri kutoka Bukoba mkoani Kagera kuelekea Mkoa wa Mwanza wamenusurika kifo baada ya basi la Kampuni ya Salvation lenye namba za usajili T746 kupinduka na kisha kuteketea kwa moto, katika eneo la Ilemela wilayani Muleba.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amesema kuwa ajali hiyo imetokea leo Julai 30,2021 saa 5:14 asubuhi, baada ya basi hilo kujaribu kukwepa gari lililokuwa linakuja mbele yake.
"Basi lililopata ajali lilipofika eneo la Ilemela, kulikuwa na mabasi mawili yaliyokuwa yakitoka mkoa wa Dar- es-Salaam kwenda Bukoba, ghafla basi la kampuni ya Super Video lenye namba za usajili T589 AUA lilijaribu kulipita la mbele yake bila kuchukua tahadhali, ili kuepuka wasigongane uso kwa uso ilibidi dereva wa basi la Salvation alikwepe ndipo gari lake likapinduka" amesema.
![]() |
Picha kwa mujibu was Nipashe. |
Amesema baada ya kulikwepa basi la Super Video, gari hilo lilimzidi nguvu dereva likaanguka na kuungua moto, na kwamba hakuna vifo maana abiria wote waliokuwemo wameokolewa.
"Hakuna vifo lakini kuna baadhi ya abiria wamejeruhiwa, majeruhi hao 12 wamepelekwa zahanati ya Ilemela na wengine kituo cha afya cha Kaigara kilichoko Muleba mjini, tunaendelea kufuatilia afya zao tutawaeleza baadae" amesema Kamanda Malimi.
Chanzo:Nipashe