HII ni hali ambayo
mwanamke anakuwa na hamu ya kufanya tendo la ndoa lakini anapata ugumu kutokana
na maumivu makali anayopata. Hali hii inatokana na kubana au kukaza kwa misuli
ya uke lakini pia inaweza kusababishwa na matatizo ukeni.
Mfano endapo kuna
michubuko au vidonda au kasoro yoyote ya uke, aidha uke ni mdogo au maumbile ya
uke hayana uwiano na uume. Tatizo hili huwapata wanawake wa rika zote ilimradi
tayari yupo katika umri wa kuzaa.
: TATIZO LINAVYOGAWANYIKA
Tatizo hili la
maumivu wakati wa tendo la ndoa limegawanyika katika maeneo makuu mawili. Kwanza
ni *Primary Dyspareunia*. Hapa mwanamke anakuwa hana historia ya maumivu wala
hana historia ya kuwahi kufanya tendo hilo ndiyo, kwanza anaanza. Kitaalamu hali
hii ya maumivu huitwa Honey moon Dypareunia au maumivu ya fungate na hutokea
mara tu anapoanza kujamiiana kwa mara ya kwanza. Katika hali hii misuli ya uke
inaweza kubana kutokana na michubuko au kuchanika ubikira au hata kuchanika
upande wa chini wa uke na wakati mwingine michubuko hutokea katika tundu ya
mkojo.
Hali ya michubuko inaweza kuwa mbaya na ikajitokeza hata kwa kugusa tu
upande wa nje wa uke. Maumivu yakiendelea au yakizidi husababisha mgonjwa apate
matatizo ya kisaikolojia kiasi kwamba huanza kuogopa tendo lenyewe na kuhisi
endapo atalifanya ataumia.
Tatizo hili likileta michubuko kwenye njia ya mkojo
husababisha maambukizi sugu ya kibofu cha mkojo kutokana na michubuko ya mara
kwa mara ya tundu ya mkojo.
Michubuko ukeni au kuhisi moto ukeni wakati wa tendo
la ndoa kunaweza kusababishwa na matumizi ya vilainishi visivyofaa au kuumwa
kutokana na uwepo wa vinyweleo virefu ukeni na endapo havikupunguzwa vitaingia
ukeni wakati wa tendo na kukuchubua.
Kasoro katika ubikira pia husababisha
mwanamke ahisi maumivu wakati wa tendo. Maumivu haya huwa hayahusiani na yale ya
awali ya fungate na wakati mwingine huanza baada ya kipindi kirefu cha miaka
mingi tangu uanze tendo la ndoa na wengine huwa na tatizo hili tayari wana
watoto.
Chanzo cha tatizo hili ni ukavu ukeni, umri mkubwa wa mwanamke na
kusinyaa kwa misuli ya uke. Maumivu ukeni hutokana pia na maandalizi mabovu
kabla ya tendo ambapo uke unakuwa haujalainika kwa kutofanya romance ya
kutosha, kutofanya tendo hilo kwa ustaarabu, yaani kutumia nguvu au endapo
mwanamke atakuwa na maambukizi ukeni mfano fangasi ambayo huambatana na kutokwa
na uchafu ukeni na muwasho, magonjwa ya uke kama kuvimba kwa tezi za uke,
kuvimba kwa mashavu ya uke au hali yoyote inayomuondolea amani mwanamke pale
ukeni inaweza kumfanya kisaikolojia aathirike na kuhisi maumivu wakati wa tendo.
Matatizo haya isipokuwa la umri mkubwa hutokea katika umri wa kati na tayari
mwanamke anayo historia ya kuwa katika mahusiano na hata tayari ana watoto.
Umri mkubwa tunaouzungumzia ni zaidi ya miaka 50 Kubana misuli ya ukeni hutokana
na makovu baada ya kushonwa msamba au kuongezewa njia wakati wa kujifungua au
upasuaji wa kurekebisha fistula pia husababisha tatizo hili.
Vyanzo vingine vya
maumivu haya ya tendo la ndoa ni kushuka kwa kizazi ambapo mwanamke atahisi kitu
kama gololi ukeni wakati akijisafisha au kuhisi kizazi kinasukumwa wakati wa
tendo, kugeuka kwa kizazi, matatizo katika tabaka la ndani la kizazi, maambukizi
sugu ukeni ambapo uchafu na muwasho ukeni hujirudiarudia, matatizo katika njia
ya mkojo na maambukizi katika viungo vya uzazi ’PID’ husababisha maumivu wakati
wa tendo la ndoa.
Matitizo ya kisaikolojia husababisha maumivu wakati wa tendo
la ndoa pale ambapo misuli ya ukeni itakaza na mwanamke anapochunguzwa huwa hana
tatizo au kasoro yoyote ukeni. Matatizo katika mishipa ya fahamu ya ukeni,
kuogopa tendo lenyewe kuhisi utapata maumivu au kama kuna historia ya kuingiliwa
kwa nguvu na ukaumia, kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu tendo la kujamiiana,
yote haya na mengine mengi humharibu mwanamke kisaikolojia na kujikuta anaanza
kuhisi maumivu hata kabla ya tendo lenyewe kwa kuingiwa na hofu.
Hali nyingine
inayoweza kumfanya mwanamke aathirike kisaikolojia na asiwe tayari kwa tendo na
hata akilifanya apate maumivu ni kuogopa kupata ujauzito wakati hayupo tayari
kwa hilo, kuogopa kupata maambukizi, kulazimishwa penzi endapo haupo tayari na
mwanaume uliye naye na kuhisi kuna tofauti ya maumbile na mume uliyenaye.
Endapo
mwanaume anakukwaza kutokana na kutokwa na jasho jingi sana wakati wa tendo,
kutoa harufu mbaya ya pua, kinywani, makwapani au sehemu zake za siri, huwa na
magonjwa ya ngozi au hata mwilini mwake, matatizo haya huweza kumwathiri
mwanamke kisaikolojia na asifurahie tendo na kutotoa ushirikiano wakati wa tendo
na kupata maumivu.
UCHUNGUZI Tatizo hili ni pana sana, unaweza kuhisi una kasoro
au maambukizi kumbe tofauti. Kwa hiyo basi ni vizuri uchunguzwe kwa umakini
katika kliniki za madaktari wa akina mama katika hospitali za mikoa ili kujua
chanzo halisi cha tatizo.