MAKETE,Na Fadhili Lunath-Greenfm.
Mwili wa kijana Enock Mbilinyi (20) mkazi wa kijiji cha Ikonda kata ya Tandala wilayani Makete mkoani Njombe umepatikana kwenye mtaro akiwa amefariki dunia Julai 18, 2021 karibu na daraja la Ikonda.
Hata hivyo kumekuwa na utata juu ya mazingira ya kifo hicho huku baadhi ya watu waliokuwa eneo la tukio wakidai kuwa huenda alibebwa na dereva bodaboda na wengine wakidai kuwa huenda alikuwa anaendesha yeye mwenyewe.
Utata wa kifo hicho unatokana na baadhi ya mabaki ya vifaa vya pikipiki kukutwa karibu na mwili wa marehemu huku pikipiki hiyo ikiwa imeondolewa eneo la tukio na mtu asiyejulikana.
Pia bado haijajulikana tukio hilo limetokea muda gani kwani wengi wa walioshuhudia tukio hilo wanadai kuwa wamepata taarifa majira ya asubuhi.
Baadhi ya mashuhuda waliofika eneo la tukio wameelezea kusikitishwa na mazingira ya kifo hicho,ambacho wanadai kimewaacha njia panda kujua sababu za kifo cha kijana huyo.
Wamewashauri madereva bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani wanapokuwa wanatumia vyombo vya moto ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Tazama pia hii ya mauaji makete ya wizi
Nao baadhi ya ndugu wa marehemu waliofika katika eneo la tukio wamedai kuwa kijana huyo hakuwa Akifanya kazi ya bodaboda bali alikuwa anaazima kwa watu wengine na kuendesha huku wakiliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tukio hilo.
Wametoa wito kwa watumiaji wa vyombo wa moto kuacha mazoea ya kuendesha vyombo vya moto huku wakiwa wamelewa pamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani wanapotumia vyombo hivyo.
Kwa upande wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe kupitia kwa kamanda wa polisi Hamis Issah limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwa sasa linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho huku pia akitoa wito kwa madereva bodaboda kuheshimu sheria za usalama barabarani.