Leo ni sehemu ya Tatu NA mwisho katika somo hili la JE! KUCHEPUKA NI ASILI AU TABIA.Baada ya somo lililopita kubeba sababu mbili hebu Leo tupitie sababu hizi pia tunaendelea karibu.
HOFU ZINAZOHUSIANA NA TENDO LA NDOA
Kati ya vitu vinavyowasumbua wanandoa wengi hususani wanaume kwenye kushindwa kushiriki tendo la ndoa au kulikinai kabisa ni suala zima la kuwa na hofu au woga wowote ule. Hofu na woga katika eneo hili huweza kuletwa na vyanzo tofauti kama vile masengenyo na kejeli pale mtu anavyojaribu kuomba kupata tendo la ndoa au hata baada ya kushiriki tendo hilo.
Mara nyingine maneno haya yanaweza kurushwa kama utani lakini yanapoingia kwenye moyo wa mwanandoa mhusika yanajenga hofu kubwa akidhani kwamba unamaanisha.
Hofu nyingine yaweza kutokea kwenye dhihaka zinazofanywa pale mmoja anapoonyesha kutokufurahishwa au kutoshelezwa na mwenzake.
Hapa kunatofauti ya kijinsia, mwanamke anahitaji busara ya hali ya juu kwenye kuongea na mume wake kumwambia kama hajaridhika, pale mwanamke anapoamua kutumia dhihaka, matusi au maneno makali, humwondoa kabisa mwanaume kwenye uwezo wake wa tendo wakati mwanaume huyuhuyu akienda kujaribu pembeni anajikuta bado yuko vizuri wakati kwa mkewe alishindwa, hilo linapotokea inakuwa ngumu sana mwanaume huyu kurudi au kupenda tena kufanya tendo la ndoa na mkewe.
Fahamu kwamba hofu ya aina yoyote ni kikwazo na sumu kubwa ya tendo la ndoa, na athari zake ni kubwa zaidi kwa mwanaume kuliko mwanamke.
PENZI KUPOA AU KUFA
Penzi linapopoa au hata linapokufa hali huwa inaonyesha wazi kabisa. Kwenye kupoa mhusika anaweza kuanza kujihisi ndani ya moyo wake kutompenda mwenzake kama alivyokuwa akimpenda awali. Inawezekana mwenzake hajagundua kuanzia mwanzoni kwamba penzi la mpenzi wake limepoa ila kama hali ya kupoa huku itaendelea lazima itagundulika.
Baadhi ya vitu dhahiri vitakavyoweza kukufanya ufahamu kwamba penzi la mwenzako limepoa au kufa nikwamba kuna mambo ambayo uliyazoea kuyaona yakifanywa kawaida hautayaona tena. Kuna vitu vilikuwa vikifanywa pasipo kukumbushana sasa utalazimika kuviomba ili ufanyiwe, utaona kila kitu kinakuwa kigumu kumhusu mwenzako na hata uongeaji au kujibu kwake kunakuwa na walakini.
Kwenye tendo la ndoa nako maranyingi ndiko kwenye kuonyesha taa nyekundu mapema, ule ushiriki, furaha na bashasha zilizokuwapo awali mkiwa kwenye tendo hauzioni tena, tendo la ndoa linafanywa kama jukumu la kawaida na maranyingine hata hamu ya kushiriki haipo.
Hapa ndipo mmoja hukinai hiyo hali ya kulazimishana tendo la ndoa, au kupeana kwa masharti au kunyimwa au hata mmoja kupoteza hamasa ya kulifanya tendo hilo na mtu asiyekuwa na hisia naye. Huo unakuwa mwanzo wa mmoja au wote kutoka nje ya mahusiano au ndoa. Penzi ni kama moto, ukiwashwa pasipo kuchochewa hupoa au hata kuzima kabisa. Wengi wanapoingia kwenye ndoa wanadhani mkishaoana basi mambo yanajiseti yenyewe tu, mapenzi yanajichanulia yenyewe tu, la hasha! Lazima kuwepo na jitihada za dhati za wanandoa kuhakikisha wanachochea penzi lao, kulilinda na kulipalilia ili liendelee kumea, kunawiri na kuzaaa matunda.
KAMA HUKUSOMA MWANZO TAFADHALI BOFYA HAPA KUSOMA "HIVI KUCHEPUKA NI TABIA AU ASILI YA MTU?"
USHAWISHI WA MARAFIKI
Wako watu wengi sana kwenye ushauri wa wanandoa na hata wale wasiowanandoa ambao wamekiri kuchepuka kwasababu ya kushawishiwa na marafiki. Ni lazima ukafahamu nguvu waliyonayo marafiki.
Usipokuwa na hekima ya juu ya kuweza kuchagua nani wa kuwanaye rafiki na nani sio basi utajikuta unapelekeshwa kila upande hata kule usipopenda utapelekwa kwasababu tu nguvu ya maamuzi haiko kwako tena bali iko kwa marafiki zako.
Yamkini unasema mimi ni rafiki tu sifanyi vile wanavyovifanya wao, mimi nasikiliza na kuchangia tu hoja zao, lakini ngoja nikwambie, taratibu utasikiliza, taratibu utaanza kuchangia na taratibu utavutika kuyafanya yale wanayoyafanya.
Yamkini wao kuchepuka ni hadithi ya kwaida na kwako sio kawaida, ukiendelea kukaa nao kidogokidogo utaanza kuona kuchepuka sio kitu cha kushangaza sana maana wengine nao wanafanya, na utaanza kidogokidogo na mwisho utakuwa mtaalamu.
Wako waliofundishwa kiutaniutani leo hii ni wataalamu kuliko walimu wao. Jifunze kuwa na msimamo. Jifunze kuchagua marafiki wanaokujenga na sio kukubomoa. Jifunze kufanya maamuzi binafsi yenye busara na yasiyokufungulia milango ya majuto. Kumbuka ukijakujuta hautokula majuto hayo na hao marafiki zako. Utayala mwenyewe na wanaokuhusu. Ni hasara na anguko kwao na familia yako na ndugu zako.
KUSOMA SEHEMU YA PILI YA SOMO HILI BOFYA HAPA "SABABU MBILI ZA KWANINI WATU HUCHEPUKA"