Maliza na yesu watuhumiwa kuuza dawa za serikali kinyume cha sheria.

0

 


MAMLAKA ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), Kanda ya Magharibi, imemkamata mfanyabiashara Zakayo Bagomwa anayemiliki duka la dawa muhimu kwa tuhuma kutoa huduma za matibabu ndani ya duka, kuuza dawa za ugonjwa wa kifua kikuu (TB), kadi za kliniki za wajawazito na vifaa tiba mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kenya vyote vikiwa na thamani ya Sh 4,869,900.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya hiyo Kanda ya Magharibi, Christopher Migoha, alisema tukio hilo lilitokea Julai 20, mwaka huu baada ukaguzi maalumu wa duka la dawa katika Kijiji cha Kanindo, Kata ya Kanindo, Tarafa ya Ulyankulu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.

Alisema katika duka hilo liitwalo ‘Maliza na Yesu’ walikuta dawa za serikali ya Tanzania zikiwa zimetunzwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuuzwa kinyume cha Kifungu cha 312(1) cha Kanuni ya Adhabu Sura 16.

Migoha alisema walikuta vitendanishi vya kupima virusi vya ukimwipamoja na vitendanishi vya kupima malaria ambavyo ni mali ya serikali vikiwa vimehifadhiwa na kutunzwa kwa ajili ya kuuzwa kinyume cha sheria.

Kaimu Meneja huyo alisema katika duka hilo, pia kulikuwa na dawa zisizosajiliwa kutumika nchini zikiwa zimehifadhiwa na kuuzwa kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Migoha, ndani ya duka hilo walikuta dawa mali ya serikali ya Kenya zikiwa zimetunzwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuuzwa.

Aidha alibainisha kuwa, pia ndani ya duka hilo pia walikuta dawa zisizoruhusiwa kuuzwa katika maduka ya dawa muhimu zikiwa zimetunzwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuuzwa kinyume cha Kanuni ya 63 ya Makundi ya Dawa ya Mwaka 2015.

Alisema walikuta pia dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi zikiwa zimetunzwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuuzwa kinyume cha Kifungu cha 75(1) cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219.

Kaimu Meneja huyo alisema mmiliki huyo wa duka hakuweza kuwasilisha risiti za manunuzi wala mauzo ya dawa zote alizokutwa nazo na kwamba hiyo ni kinyume cha Kanuni za Uendeshaji wa Biashara ya Dawa za Binadamu.

Katika ukaguzi ndani ya duka hilo, pia walikuta vifaa tiba ambavyo ni seti ya kufanyia tohara vikiwa vimetunzwa kinyume cha sheria pamoja na dawa za wangojwa wa kifua kikuu ambazo hazikustahili kuwepo ndani ya duka hilo wala kuuzwa kwenye maduka ya dawa muhimu.

Aidha, aliwataka wadau wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) na wafanyabiashara wote wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi kufanya biashara zao kwa kuzingatia Sheria ya Dawa na Vifaa tiba Sura 219 pamoja na sheria nyingine.

Chanzo Habari leo

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top