MTUHUMIWA WA WIZI WA KUKU AUAWA,RPC ATOA ONYO KWA WANANCHI MAKETE

0


Mkazi wa Kijiji cha Ihanga wilayani Makete mkoani Njombe amefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kupigwa na wananchi kwa tuhuma za wizi 

Afisa Mtendaji wa kata ya Ukwama kilipo kijiji hicho Bw. Absalom Mwenga amesema kijana huyo aliyefariki anaitwa Tobadi Sanga na kwa mujibu wa wananchi wa kijiji hicho anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30



Amesema Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Julai 9, 2021 ambapo Marehemu pamoja na mtuhumiwa mwingine aliyetajwa kwa jina la Egidi Sanga walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa kuku na kupelekwa kwa mtendaji wa kijiji cha Ihanga na kuwekwa mahabusu kwa ajili ya kupelekwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi, lakini walitoroka baada ya kuvunja mahabusu hiyo ya kijiji na kutokomea kusikojulikana


Amesema baada ya kutoroka watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki tena kuiba na ndipo walipokamatwa wakiwa na kuku mmoja, ambapo inadaiwa walishushiwa kipigo na mmoja wapo kufanikiwa kukimbia lakini mwenzake alipigwa na kufikishwa tena kwa mtendaji wa kijiji lakini alifariki baadaye na chanzo kikidaiwa ni kutokana na kipigo


Amesema Mnano Julai 7, 2021 watuhumiwa hao walifikishwa kwa mtendaji wa kijiji na kuchukuliwa maelezo ambapo walikiri kuiba kuku watatu na kwa kuwa ilikuwa ni majira ya usiku wakawekwa mahabusu ya kijiji lakini wakatoroka na taarifa zikadai wametorokea Mbeya lakini wananchi walikutana nao kesho yake usiku na ndipo walipoamua kuchukua sheria mkononi kwa kuwapa kipigo

Mtendaji Mwenga amelaani kitndo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi na kupelekea kifo cha mwananchi huyo kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria ya nchi



Kamanda wa polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi zaidi kufahama ni mazingira gani yamepelekea kifo hicho ili sheria ichukue mkondo wake

Kamanda huyo amewaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi  na kuahidi kufanya ziara katika vijiji vya wilaya ya Makete na viongozi wenzake wa jeshi la polisi hasa vile wanavyoona vimekuwa na matukio ya mauaji ili kuzungumza na wananchi kwa kuwa kitendo cha kukatisha uhai wa mwananchi mwingine hakikubaliki



Mwili wa marehemu huyo tayari umezikwa leo katika kijiji hicho cha Ihanga

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top