NILITAMANI SANA MWANANGU AFIE TUMBONI

0


Kuna Stori uliandika jana kuhusu Mama ambaye alikua anawapiga watoto wake kwakua tu Baba alikua anachepuka (ninaiandaa). Kaka naomba uandike na ufundishe namna ya kudhibiti hasira za kuachwa maana nahisi mimi ni mhanga, nimesoma kisa cha jana nusu kuchanganyikiwa.


Mimi ni Mama wa mtoto mmoja, ana miezi sita lakini sijawhai kumnyonyesha wala kumgusa mwanangu tangu kuzaliwa kwake. Naomba nikupe kisa changu kidoto Kaka kama hutajali, mimi sikuolewa ila nilikaa na huyu Kaka kwenye mahusiano kwa miaka 7. Nilikua nampenda naye alikua ananipenda, alishanitambulisha kwa kila mtu, kwao walikua wananipenda sana.


Kila mtu alikua anajua kuwa huyu Kaka ndiyo atakuja kuwa mume wangu, mambo yalianza kubadilika mwaka jana mwanzoni alipokuja kujitambulisha nyumbani kwetu. Baada ya kutajiwa mahari na kulipa nusu niliona mwanaume anabadilika, zile simu hazikua simu tena, alikua hajibu meseji zangu na mara nyingi alikua akiniambia kuwa yuko bize.


Nilikua naumia sana, kumbuka hapo ilikua ni mwaka jana 2020 mwezi wa kwanza, mipango ilipanga kufunga ndoa mwezi wa nne lakini niliona kama anabaidlika, majibu ni ya ajabu, anatoka haniagi na nikipiga simu hapokei au akipokea basi ni matusi bila sababu. Siku moja nikapigiwa simu na mwanamke akaniambia kama kusoma hujui hata picha huoni, mwanaume huyu si wako tena ni wangu, nampenda na nina mimba yake.


Alinitumia picha nyingi sana za chumbani akiwa na huyo mwanaume na mimba yake, hapo ilikua ni pili mwanzoni, kuona hivyo nilichanganyikiwa, nilijihisi kichaa, nikampigia mwanaume akaniambia ni kweli ana mimba yake na kaamua kuzaa naye kani mimi kakaa na mimi miaka sabau hata mimba sibebi, akaniambia bila kuzunguka “Siwezi kuoa mwanamke ambaye sina uhakika kama ana kizazi, mambo ya kuchangishana kila siku halafu nije kuoa jitu halizai sitaki!”Nilijisikia uchungu sana kwani pamoja na kwamba tulikua bado hatujaingia kwenye ndoa wala alikua hajawahi kuniambia kama anataka mtoto lakini hata mimi nilishaanza kuwa na wasiwasi. Nilikaa kwenye mahusiano naye miaka saba, tulikua hatutumii kinga na mara nyingi tulikua tunafanya mapenzi siku za hatari lakini nilikua sijawahi kubeba mimba yake, hali hiyo ilikua inaniumiza sana na kuna wakati nilikua nikiamini kabisa kuwa nina matatizo.


Kibaya zaidi huyo mwanamke alikua ni rafiki yangu, tena yule shoga yangu kabisa ambaye nilikua namuambia kila kitu katika maisha yangu. hata mambo ya kuwa labda siwezi kupata mtoto nilishawahi kumuambia akawa ananipa moyo kuwa mimi bado mdogo sijaingia kwenye ndoa na nisipaniki. Kumbe kila kitu nilichokua nikimuambia alikua anamuambia mchumba wangu, niliumia sana. nilijaribu kumuomba msamaha mchumba wangu lakini hakutaka kunisikiliza, sikumoja niliomba kuonana naye.


Nilikua katika siku zangu za hataei, nikiamini kuwa kaniacha kwakua sizai hivyo nikimuambia kuwa nina mimba yake basi atabadilisha mawazo nilimtega mpaka nikaibabe mimba yake. Sikutaka kumuambia mapema mpaka ujauzito ulipofikisha miezi mitatu, hapo ndipo nilimuambia, huwezi amini nikitegemea labda atafurahi basi alikasirika, alinitukana na kunitumia pesa kuwa nitoe mimba yake.


Mwanzo hata sikukubali, nilijua kuwa ni hasira, nikajua kuwa kama nikijitahidi na kukazana kuonyesha upendo basi atamsahau rafiki yangu, lakini haikua hivyo, mwaka jana mwezi wa sita alifunga ndoa tena ya kanisani, kubwa, yaani walimualika mpaka Mc ambaye nilikua namuwaza kila siku namuambia rafiki yangu, ukumbi uleule yaani ni kama walifanya harusi yangu ila bibi harusi sikua mimi, hata gauni la harusi walichukua lilelile ambalo mimi nilichagua nikiwa na huyo rafiki yangu.


Walipost na kuhakikisha kila mtu anajua, marafiki zangu ndiyo walikua marafiki zake, baada ya kuachwa niliona kila mtu ananikimbia, kila mtu anakua adui yangu, akili haikufanya kazi, nilihisi maisha yanaisha. Hapo ndipo nilianza kuhangaika kutoa mimba yangu, niliahangaika lakini haikutoka. Kuna wakati nilipofikisha mimba ya miezi saba nilihangaika mpaka nikapata drip ya uchungu nikatundikiwa ili tu nijifungue mtoto atoke lakini hakutoka.


Nilikua najichukia sana, sikutaka tena kuwa na mtoto, nilitaka kuitoa hiyo mimba nikiamini kuwa nitamuumiza kwani nilihisi kama anapenda sana mtoto. Nilihangaika mpaka nikajifungua, tena kwa bahati mabya zaidi nikajifungua kwa kisu, hali hiyo iliniumiza sana kwani niliona kama nimeharibu usichana wangu, nilimchukia mwanangu kiasi nilitamani hata angefia tumboni lakini aliamka tena akiwa na afya nzuri kabisa.


Hospitalini nilihudumiwa na Mama yangu, baad aya kukaa vizuri alitaka kunikabidhi mwanangu lakini niligoma, wao walidhani ni kitu cha muda lakini niligoma kumchukua, hata kumnyonyesha pamoja na kuwa maziwa yalikua yanatoka mpaka kuniloanisha ila niligoma, nilikua nikiamini kama nikimuacha akanyonya basi matiti yangu yataharibika. Tulirudi nyumbani sijui walimpa maziwa gani na sikujali, niliamini kama akibaki njaa basi atakufa lakini haikua hivyo.


Pamoja na hali yangu nilirudi nyumbani hata sikukaa, nilimuacha mtoto wangu kwa Mama na kuondoka, nikapanda gari na kurudi Dar nikiwa na mshono wangu wa siku moja. Kusema kwelis ikusikia maumivu yoyote, nilikua kama chizi, nilirudi Dar na kila rafiki yangua liyeniuliza nilimuambia kuwa mtoto alifia tumboni hivyo mimi sijawahi kuzaa na sina mtoto.


Niliamini kwamba kama nikijiaminisha kuwa mtoto wangu amekufa basi ningekua kama wale wadada ambao wanameza P2 tu. Nilijifungua mwaka jana mwezi wa 12 lakini mpaka leo sijawhai kumshika mwanangu, sijawahi kumnyonyesha na sitaki hata kumuona. Hata dada zangu wakinitumia picha zake nazifuta siangalii, naumia sana kwani pamoja na kufanya yote haya X wangu hata hajali, walsiahmuambia nimetelekeza mtoto lakini hata hakunitafuta.Kila nikiingia kwenye mitandao naona jinsi walivyo na furaha, anampost mtoto wake na huyo shoga yangu naumia. Natamani hata angempost wangu, yaani maisha yangu yamekua ni ya kuishi kwa wasiwasi tu kazini kila mtu anajua kuwa sina mtotoa lifia tumboni. Nimeanzisha mahusiano mengine ila Kaka huu mshono kuna wakati natamani hata kulikata tumbo langu, napata shida kujielezea, kile kitendo cha kuonekana kama nimeza kinaniumiza sana.


Nimesoma stori ya huyo dad anikajiona kama mimi, natamani kubadilika, kuna wakati najikuta naingia ndani nalia, natamani kwenda nyumbani kumchukua mwanaangu na kumbeba kwa mara ya kwanza lakini kila nikifikiria aliyonifanyia X wangu najikuta nazidi kumchukia mtoto kuna wakati hata natamani kupokea simu kusikia mwanangu amekufa lakini hata haiku hivyo nashindwa sijui nini cha kufanya nimekata tamaa kabisa ya maisha.

 https://twitter.com/aziranigroup 

MWISHO


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top