TABORA: NYOKA AMKIMBIZA MWALIMU!

0

 


MWALIMU Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dk. John Magufuli katika Kata ya Kamsekwa, wilayani Kaliua mkoani Tabora, amekimbia nyumba aliyojengewa na shule kwa hofu ya kuwapo nyoka aina ya kobogo.


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kamsekwa, Ramadhan Juma, alibainisha hayo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Aloyce Kwezi, alipokuwa katika ziara ya kukagua utekelezaji miradi ya maendeleo wilayani humo.

Mwenyekiti huyo alimweleza mbunge na Kamati ya Mfuko wa Jimbo kuwa nyumba hiyo licha ya kukamilika tangu mwaka 2015 haikaliwi na mtu kwa sababu ya nyoka huyo aliyeko ndani.

Alisema licha ya mwenyewe kutomuona, lakini waliomuona walidai ni nyoka aina ya kobogo na tangu alipoonekana katika nyumba hiyo, Mwalimu Mkuu hakuingia tena.

Alisema walileta wazee wa kimila wakafanya tambiko baadaye akaja mchungaji kuombea nyumba hiyo, lakini wanaogopa kwenda kufungua mlango kujiridhisha kama bado yupo au alishaondoka.

Mwalimu Mkuu Leonard Assenga, alisema walimu na wanafunzi wana hofu kubwa na nyoka huyo na kushindwa kufundisha.

Hata hivyo, alisema hakuna madhara yaliyosababishwa na nyoka huyo, lakini ni hofu miongoni mwa walimu na wanafunzi na kuomba juhudi zifanyike ili kumwondoa na kumwezesha kurudi katika nyumba yake.

Kaka Mkuu wa shule hiyo, Joseph Jackson, alisema hawana raha na wanashindwa kusoma kwa amani kutokana na hofu.

Nyumba ya Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Dk. John Pombe Magufuli iliyoko katika kata ya Kamsekwa inayohisiwa kuwa na nyoka aina ya kobogo


Kwa upande wake mbunge wa jimbo hilo, Aloyce Kwezi, aliwataka kutafuta mtaalamu wa kukamata nyoka ili awasaidie kumwondoa kwa kuwa uwapo wake katika eneo hilo ni hatari na unawapa hofu walimu na wanafunzi.

Aliwataka viongozi wasitegemee maombi bali wawatafute wataalamu wa kukamata nyoka waje wamwondoe ili wanafunzi wasome kwa amani na utulivu.

“Shughulikieni suala hilo haraka iwezekanavyo ili maendeleo ya shule hiyo kitaaluma na miradi inayoendelea kutekelezwa isije kuathirika kutokana na hofu iliyopo," alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top