Katibu Mkuu wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Laban Kihongosi amesema wanasikitishwa na matendo yanayofanywa na Mbunge Humprey Polepole kuhusu suala la chanjo, kwani Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshasema Kwamba chanjo ni hiari na maamuzi yake lazima yaheshimiwe.
“Tunapenda kumwambia Mbunge Polepole kwamba awe na nidhamu na adabu kama aliyokuwa nayo wakati wa Utawala wa Awamu ya Tano, nidhamu ileile aiendeleze pia katika Utawala huu wa Awamu ya Sita Inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mijadala yake kuhusu chanjo ni bora akakaa kimya kama haitaji kuchanja, lakini sio kujificha katika kivuli cha chanjo kuipinga Serikali”———Kihongosi
“Kamwe hatutovumilia utovu wowote wa nidhamu kwa Rais Samia na Serikali yake, sasa kuendelea kutengeneza maneno ya kejeli, dhihaka na mengine ya aina hiyo yanabeba mazingira yanayotia shaka dhamira yake aliyonayo kwa Mwenyekiti wetu na Rais wetu wa Tanzania, tunamtaka aache mara moja”———Kihongosi
“Chama cha Mapinduzi sio Chama cha harakati bali ni Chama kilichojijenga katika misingi ya kutii na kuheshimu Viongozi, hivyo jambo lolote la kupinga au kuendeleza mijadala ambayo Mwenyekiti wa CCM Taifa ameshaitolea maelekezo ni utovu wa nidhamu kwa Chama na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi”———Kihongosi
“Tunamuonya na tunamtaka aache mara moja kwani hatutakubali Kiongozi yoyote avunje heshima ya Rais Samia Suluhu Hassan au kupinga yale aliyoyaelekeza”———Kihongosi
Siku moja kabla ya kutolewa kwa kauli hiyo ya kihongosi Mh.Polepole kupitia ukurasa wake wa Intagram aliandika haya.
Katika pitapita yangu nimesoma ripoti hii ya Uwekezaji Duniani Mwaka 2021 yaani World Investment Report 2021 iliyotolewa na UNCTAD.
Ripoti inasema Mwaka jana 2020 katikati ya wimbi la korona bado Tanzania iliendelea kuaminiwa na hakukuwa na mabadiliko ya kiuwekezaji kutoka nje kitu ambacho kilikuwa tofauti kwa majirani zetu.
Nikipitapita huku mitaani bado naona kuishinda HOFU ni silaha muhimu zaidi dhidi ya korona na nyenzo muhimu ya kuimarisha Uchumi na kuleta maendeleo kwa watu wetu.
Wakati nikipongeza jitihada nzuri za Serikali ya @ccmtanzania kuweka uchumi wetu sawa katika ya linalosemwa wimbi lingine la korona Mwaka 2021 mbinu moja tusiiache, kwamba korona si kubwa kama tunavyo ambiwa.
Yako magonjwa mengi na yanayoua zaidi, tusije tukatolewa kwenye mstari na korona, nimesoma pia wengi ya wanaoshambuliwa na korona ni wale wenye mashambulizi ya magonjwa mengine yanayoteteresha Kinga ya Mwili ambayo korona inafanya magonjwa hayo yasisemwe kwa kiwango kinachostahili.
Naomba kwa unyenyekevu kutoa rai kwamba ni muhimu sana watu wetu wakumbushwe tena na tena namna ya kujenga kinga ya Mwili ikiwemo elimu ya chakula na lishe bora kama hatua ya msingi ya kukabiliana na magonjwa na maambukizi yanayoweza kuzuiwa na kinga imara ya Mwili.
Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika hili na ni Imani yangu vitatenga nafasi na kuzungumzia masuala haya kwa maslahi Mapana ya Nchi yetu, Taifa letu na Watu wetu wa Tanzania 🇹🇿
Mungu ibariki Tanzania
Ibilisi na Huu ugonjwa wake hawana nafasi Tanzania.
NB:
1. Kuchanja ni hiyari lakini sio kila kitu, mimi nitaimarisha Kinga ya Mwili na chanjo kwangu HAPANA
2. Sasa baadhi yenu msihangaike na mimi, hangaikeni na rai yangu hapo juu