Nipo kwenye mahusiano na huyu Dada kwa mwaka mmoja na nusu sasa. Hatuishi pamoja lakini muda mwingi nipo kwake, ananihudumia kwa kila kitu. Mimi nafanya kazi lakini kipato changu ni kidogo sana siwezi kuhudumia mwanamke nayeye anajua. Tangu kuja hapa Arusha yeye ndiyo ananihudumia, amenilipia kodi kwenye nyumba nzuri, kaninunulia Pikipiki na kila mahitaji yangu yote.
Namshukuru Mungu kwa hilo, wakati naanzisha naye mahusiano nilimuambia kuwa nina mwanamke wangu ambaye yuko mkoa mwingine na anajua tunawasiliana naye. Hakuonekana kuwa na shida na hilo lakini kadri siku zinavyoenda niliona nazidisha wivu hataki niwasiliane na huyo mwanamke, alikua ananibana sana kuna kipindi akamblock mwanamke wangu kwenye simu yangu.
Kwakua nampenda nilitafuta namba nyingine na kumuambia Mpenzi wangu kuwa ile namba yangu nilipoteza na Voda wakaigawa hivyo asiipige na kweli nikawa nawasiliana naye kimyakimya mpaka sasa. Sababu ya kuja kwako ni hivi, huyu dada alikua analazimishia sana nimbebeshe mimba akiamini kuwa akishabeba mimba ndiyo nitamuoa, mimi nilikua nakwepa sana lakini kama unavyojua haya mambo ukitengewa chakula unakula, ana mimba yangu.
Amelazimisha sana niende kujitambulisha kwao na kutoa mahari lakini nilikua nakataa kwa madai kuwa sina kipato cha kutosha, alinipa milioni mbili ili kwenda kutoa mahari kwao, nilienda hivyo hivyo nikajitambulisha kwao lakini sikutoa mahari nilimuambia bado mpaka kwetu wajipange kwani Baba alikua anaumwa.
Baada ya kuona kuwa ananisumbua nilihisi kuwa naweza kumtafuta mpenzi wangu na kuniharibia kwani yeye nishamtambulisha kwetu na kwao najulikana. Nilichukua ile milioni mbili, nikaenda kwa mpenzi wangu, nikatoa mahari nusu na kuwaambia kuwa nataka kufunga ndoa ya harakaharaka na wiki iliyopita nimefunga ndoa ya Kanisani. Sababu ya kuja kwako ni hivi, namuachaje huyu dada bila kumuumiza kwani pamoja na kwamba ana wivu sana na ni king’ang’anizi sana lakini hajawahi kunifanyia kitu kibaya.
Mke wangu anataka kuja ninapoishi lakini sina maisha ya kumhudumia. Pesa zote nilizokua nikimtumia zilitoka kwa huyu Dada, mimi naishi chumba kimoja hivyo picha nilizokua namtumia ni za kwa huyu Dada anajua nina maisha mazuri, nifanye nini maana sitaki kumuumiza yoyote. Mwanzo haya mambo yalianza kama utani ila sasa hivi naona nitaumiza watu wengi sana nisaidie?