NDOA YA MAUTI; SITAMANI KUFA LAKINI SITAKI KUISHI --- SEHEMU YA PILI

0

 (ILIPOISHIA; Niliingia chumbani na kukuta mwanangu amelala hapumui, nilianza kumgeuza geuza huku nikimpumulia mdomoni ili anyanyuke…ENDELEA…)


Nilimgeuza geuza na ghafla nilisikia sauti ya kilio, kilikuwa kilio kama cha mara ya kwanza mtoto anapozaliwa, mpaka sasa sijui nilifanya nini mpaka akalia lakini nahisi ilikuwa ni miujiza tu ya Mungu.

Nilihisi nishampoteza mwanangu na nilijua mume wangu ndiye alitaka kumuua. Ningeweza kuvumilia vyote lakini si kumpoteza mwanangu, nilimkagua na kukuta yuko salama, aliendelea kulia, nilimnyanyua na kumbembeleza huku nikimshukuru Mungu kwa ule muujiza.


Kelele za kilio chake zilimstua mume wangu, aliingia kama anakimbia huku akihema kwa nguvu.

“Ameamka! Ameamka! Nilijaribu kumuamsha lakini hakuamka! Ahsante Mungu! Ahsante Mungu!” Alijiongelesha huku akinisogelea, alinyoosha mikono yake kutaka kumpokea mtoto lakini sikuruhusu, makusudi nilimkwepesha ili asimguse.


“Nini? Hutaki nimguse? Au sio mwanangu… sio wa kwangu huyu mtoto, sio wa kwangu!” Aliendelea kujiongelesha lakini sikumjibu, nilimuangalia kwa jicho la kumsuta na kwa aibu alitoka bila kuaga. Kusema kweli nilikuwa nimechoka na manyanyaso ya mule ndani na ilikuwa ni lazima kumuambia mtu la sivyo ningechanganyikiwa.


Nilimpigia simu shangazi yangu na kumuuliza kama yupo nyumbani, nilimuambia nataka kuonana naye kwani kuna mambo makubwa yametokea katika ndoa yangu. Niliongea huku nikilia, shangazi alishtuka kidogo kwani ilikuwa ndiyo mara ya kwanza mimi kufunguka kuhusu ndoa yangu.


Aliniambia aje kunichukua na gari kwani alikuwa dukani lakini nilikataa, nilimuomba tukutane dukani kwake ambapo ilikuwa ni gari moja tu ili twende nyumbani kwake kuongea. Alinikubalia na harakaharaka nilimuandaa mtoto na kuondoka bila kumuaga mtu yeyote.


Nilimpita Mama mkwe, wifi zangu na mume wangu pale sabuleni bila kusema chochote, sikujali kitu na hakuna hata mmoja aliyenisemesha. Inaelekea wote walishajua alichokuwa anataka kufanya mume wangu au ilikuwa ni mipango yao kwani walikuwa wakiniangalia kwa wasiwasi tofauti kabisa na kawaida yao.


*****


“Una ushahidi wowote kama alitaka kumuua?” Shangazi aliniuliza nilipomuelezea kila kitu kuhusu ndoa yangu na kilichotokea siku ile.

“Hapana shangazi ila nahisi tu, kwanini mtoto alie na akutulia, halafu kwanini afunge mlango. Kuna mambo mengi yanaendelea shangazi na yananipa wasiwasi sana. Lazima kutakuwa na kitu kibaya alitaka kumfanyia mwanangu”


“Mwanangu ndoa ni uvumilivu, huwezi kumshutumu mume wako mambo kama hayo..!” Shangazi aliongea kwa sauti ya juu kama vile ananifokea. Nilishtuka kwani nilitegemea kwa niliyomueleza atakuwa upande wangu.


“Shangazi sio kama namshutumu. Mume wangu kanifanyia mengi mabaya navumilia. Hili siwezi kuvumilia, isitoshe anasema mtoto si wake na nahisi hiyo ndiyo sababu ya kutaka kumuua?”


“Tema mate chini mwanangu, hayo unayonena ni makubwa! Mumeo hawezi kufanya hivyo na kama anasema mtoto si wake labda kuna vitu umefanya unanificha, mtu hawezi kuibuka na kusema tu mtoto si wake… lazima kuna kitu umefanya hutaki kuniambia”


Maneno ya shangazi yalinikatisha tamaa kabisa, nilishajiandaa kuondoka na kuanza maisha yangu upya bila ndoa lakini nilihitaji sehemu ya kuanzia. Nilimuomba shangazi kukaa pale kwa muda wakati nikijipanga lakini alikata akisema. Aling’aka na kuona kama nilikuwa nataka kufanya kitu cha ajabu sana.


“Wewe ni mke wa mtu, siwezi kukuruhusu kukaa kwangu tu! Unafikiri Baba yako atanielewaje akijua mimi ndiyo nimevunja ndoa yako? Tatizo kidogo unataka kuondoka, unajua sisi kuna mangapi makubwa tumepitia? Unafikiri kila mwanamke anayekorofishana na mume wake angeondoka kungekuwa na ndoa kweli?


Mume wako kama kakuchoka akurudishe kama alivyokuchukua, unafikiri ukikaa hapa wazazi wako watanielewaje? Kaka atanielewa kweli kama mimi ndiyo nakuendekeza! Hapana, rudi huko huko na kama mumeo akikuleta hapa nitakupokea lakini huwezi kuja tu mwenyewe nikakupokea bila mumeo eti ndoa imekushinda.


Tena na shutuma kama hizo! Hata wazee hawajashirikishwa! Hapana siwezi! Wewe ulikabidhiwa kwa mume hukujiondokea tu nyumbani kama kichaa! Maisha hayaendi hivyo mwanangu! Jifunze kuvumilia, ndoa zote zipo hivyo!”


Aliongea maneno mengi kiasi cha kushindwa kuendelea kumsikiliza tena, kusema kweli nilichanganyikiwa, nilibaki nimeduwaa nikiwa sina hili wala lile. Nilitamani hata kurudi kijijini lakini kila nikimuwaza Baba niliishiwa na nguvu, kama shangazi amekuwa mkali vile nilijua Baba angeniua kabisa.


Nikiwa nimenyong’onyea nilimbeba mwanangu, nikachukua na pochi langu na kuanza kurudi nyumbani kwa mume. Nilishakata tamaa na maisha na sikujua ningeenda wapi tena, shangazi alitaka kunisindikiza na gari lake lakini nilikataa, niliondoka na hasira zangu nikiwa nimechanganyikiwa.


*****


Nyumbani nilimkuta mume akiwa amefura, alionekana wazi kuwa na wasiwasi kutaka kujua nilikwenda wapi? Maswali yake yalilenga kujua nilikuwa wapi, nimeongea na nani na nimewaambia nini? Alijichanganya na kuongea mambo ambayo yalionesha wazi kweli alitaka kumdhuru mwanangu.


Pamoja na kwamba sikuwahi kuongea kama ametaka kumuua mtoto lakini alianza kusema mbona sitaki amguse mtoto, “Ina maana huniamini na huyo mtoto, unaona nitamdhuru, unafikiri naweza kumfanya nini? Unaniona kama mnyama, hivi unafikri nina roho mbaya kiasi hicho kumdhuru malaika kama huyu?


Au sio mwanangu na leo nasikia bwana yako alikuja hapa! Au ndiyo Baba wa mtoto..” Alijiongelesha lakini sikumjibu kitu ambacho kilimfanya anione kiburi. Maneno yake yalinifanya kujua hasira zake zilitoka wapi, mchana alikuja Mudi kijana ambaye alikuwa akinunua mayai kwangu kwenda kuyachemsha na kuyauza.


Ni muda tulikuwa hatujaonana hivyo tuliongea kidogo na wifi zangu walimuona nadhani hicho ndicho kilimpa hasira kwani Mudi alikuwa mweupe na nilishasikia mara kadhaa wifi zangu wakinong’ona kama ndiye alikuwa Baba wa mwanangu.


Sikuongea kitu na kule kukaa kwangu kimya kulimkera hivyo niliambulia kipigo cha kufa mtu. Pamoja na manyanyaso yote lakini ile ndiyo ilikuwa siku ya kwanza mume wangu kunipiga, nililia kwa nguvu kwani kipigo chake kilitonesha mshono, damu zilianza kutoka.


Alipoona damu aliniacha chumbani na kuondoka zake, wakati huo mwanangu alikuwa akilia kwa nguvu huku na mimi nikilia kwa maumivu. Nilijikaza na kwenda kumnyonyesha mtoto ili atulie lakini haikusaidia hakutaka kunyonya.


Nilichukua upande wa khanga na kuukandamizia kwenye kidonda ili kuzuia damu zisitoke. Nilijitahidi kunyanyuka na kuanza kumbembeleza mwanangu ambaye alikuwa akilia sana, nilikuwa katika maumivu makali lakini sikuwa na namna, hakukuwa na mtu wa kunisaidia.


Niliendelea kumbembeleza mpaka nikawa sijisikii maumivu tena, yaani niliyazoea, mwanangu alilala hivyo nikamlaza. Nilienda kusafisha kidonda na kukifunga vizuri na bandeji kisha kwenda kupika chakula cha usiku kwaajili ya familia, wifi zangu na Mama mkwe walikuwa sebuleni wakiangalia TV nilijua kama nisingepika mimi wasingepika na ingekuwa tabu nyingine, mume wangu hakurejea tena mpaka asubuhi.


*****


Mume wangu ni kama alionja asali na kuamua kuchonga mzinga kabisa, baada ya kunipiga mara ya kwanza ilianza kuwa kama tabia yake, kila akikasirika kidogo alikuwa akinipiga hata bila sababu na ndugu zake walikuwa wakishangilia wakiongea maneno ya mafumbo wakisema kama nimechoka si niondoke nasubiri nini pale? 


Lakini niliamua kuvumilia nikiamini ipo siku yataisha. Lakini hayakuisha yaliendelea kila siku mpaka nikaona kama kipigo ni sehemu ya maisha yangu, mwanangu alikuwa na Mungu alianza kuwaumbua. Kadri mwanangu alivyokuwa akikua ndivyo alikuwa akifanana na Baba yake.


Weupe ulikuwa ukiondoka siku hadi siku na alipofika miaka miwili alikwua anaelekea kuwa mweusi kama Baba yake, sura ya Baba yake ilichomoza usoni kwake kiasi kwamba hata mtu ambaye alikuwa hajui kuwa ni mtoto wake kwa kuona tu alisema wamefanana. Jambo hilo lilimpa aibu sana mume wangu akajirudi rudi ingawa manyanyaso hayakuisha.


Kutokana na maneno maneno ya mule ndani nilijikuta naelekeza nguvu zangu katika kufanya kazi, kutwa nzima nilikuwa kwenye kuku na biashara ilikubali. Niliacha biashara ya kufuga baada ya kupata mtaji nakufungua duka la kuuza vyakula vya kuku na vifaranga.


Hapo ndipo nilipoanza kuishika pesa ya kweli, biashara ilichanuka na ndani ya mwaka mmoja niliweza kununua gari pikapu na kiwanja nikimshauri mume wangu tuanze ujenzi ili tuondoke pale nyumbani lakini alikataa akisema tukarabati nyumba tuliyokuwa tukiishi kwanza.


Kwa kuwa yeye ndiyo alikuwa kila kitu nilimsikiliza. Lakini mafanikio yalikuja na changamoto, ndugu wa mume walianza maneno mengine wakisema mimi nawaloga ndiyo maana wao hawafanikiwi mimi nafanikiwa. Pia mume wangu ni kama alichoka kunipiga na kuninyanyasa, alirudisha upendo kidogo kitu ambacho kiliwaumiza vichwa.


Lakini waliumia zaidi pale walipogundua nina ujauzito wa miezi mitatu, ni muda sana mume wangu alitaka mtoto mwingine lakini nilijaribu bila kufanikiwa hivyo walipoona nina ujauzito walizidisha chuki kwani walijua Erick angezidisha upendo.

 

Tangu agundue ni mjamzito hakunipiga tena, hata akiwa na hasira vipi alijizuia akiishia tu kutukana huku akisema nina bahati nina mimba angenipiga mpaka kuniua. Kwao hilo waliona kama ni uchawi na kila siku waliibua kitu kipya kutaka kuonesha kama kweli mimi ni mchawi na sipaswi kuishi pale kwani nawaloga wao wasiendelee na namloga mume wangu asiwasikilize.

Walikua wakiamini kweli kama nawaloga na mara nyingi walilalamika kwa mume wangu ambaye kwa kuwa ni msomi alikuwa haamini sana hayo mambo. Hali hiyo ilizidi kuwakera na kila kitu kibaya kilipotokea walisingizia uchawi, amani iliyoanza kurejea ilianza kutoweka tena.


Kusema kweli ni kitu ambacho kilinishangaza kwani sijui ni namna gani wangefanikiwa kama wote walikuwa wakikaa tu nyumbani, kila kazi waliyokuwa wakitafutiwa walikuwa wakiharibu na hata kuja tu kukaa dukani wasingeweza kukaa kutwa nzima bila kutoka hivyo kulazimika kuajiri wafanyakazi wa nje.


Lakini haikuishia hapo, walikuwa wakiingia dukani kama kwao na kuchukua pesa tu bila taarifa na pale niliposema walisema ni pesa za kaka yao na kweli mume wangu aliwatetea na kuona kama nina wanyanyasa.


Siku moja nikiwa nimetoka dukani niliwakuta wote wakiwa wamekaa sebuleni, niliwasalimia lakini hawakuniitikia, mume wangu alionekana kukasirika sana, alikuwepo yeye, Mama mkwe na wadogo zake wote. Mezani kulikuwa na vitu ambavyo viliwekwa.


Vilikuwa vimefungwa fungwa kama hirizi, ndipo bila hata salamu mume wangu alianza kunishutumu kuwa nawawekea madawa, alininyang’anya pochi niliyokuwa nimebeba na kuanza kuikagua, aliifungua na kuangalia kila mfuko ndipo alipoona vitambaa tambaa kama hirizi sawa na vile vilivyokuwa mezani.


Alianza kunipiga kuniuliza ni nini lakini mimi sikujua kwani sikuwa mimi nimeviweka, alinipiga kweli huku akisaidiwa na Mama yake na wadogo zake, walinipiga kama mbwa wakinitukana matusi ya nguo. Mwanangu ambaye wakati huo alikuwa na miaka mitano alianza kulia na kuwaambia waniache lakini hawakusikia.


Aliruka na kunidondokea hivyo tukawa chini pamoja, lakini hawakujali waliendelea kunipiga mpaka nikapoteza fahamu. Hawakutaka hata kuninyanyua waliniacha pale pale chini, nilizinduka kama masaa mawili baadaye, mwanangu kalala pembeni yangu kapitiwa na usingizi.


Nilijaribu kujinyanyua lakini nilishindwa, mwili wote ulikuwa unauma nilijikuta nalala pale pale mpaka asubuhi. Asubuhi nilijitahidi na kuamka, niliingia chumbani nikiwa nimepanga kuondoka, sikutaka kwenda nyumbani kwani nilijua wataniambia nivumilie.


Nilishachoka kuvumilia kwani nilijua siku moja watakuja kuniua, nilidhamiria kuondoka, niliingia chumbani na kuanza kukusanya nguo zangu, mume wangu bado alikuwa amelala, sikua nikiogopa, nilikuwa tayari kuacha kila kitu na kuondoka.


Wakati nakusanya vitu vyangu mume wangu aliamka, aliniangalia kana kwamba hakujatokea kitu kisha akaniuliza. “Unafanya nini?”


Nilimuangalia na bila uoga nilimuambia “Nakusanya nguo zangu, nimechoka haya mateso, hapa tulipofikia ipo siku mtakuja kuniua bure, naondoka zangu, sijui nitaenda wapi lakini bora kufa porini kuliko kufia hapa…” Nilimjibu kwa kujiamini.


“Afadhali uondoke, chukua kila takataka uliyokuja nayo, kasoro mwanangu, hukuja na mtoto utaondoka hivyo hivyo ulivyokuja! Na ukijifungua huyo mwingine nakuja kumchukua! Ulijue hilo kabisa! Ingekuwa inawezekana ningekupasua tumbo sasa hivi nimchukue! Siwezi kuishi na mchawi nyumba moja!” 


Aliongea kwa dharau na sauti ya kumaanisha, alimshika mtoto mkono aliyekuwa amekaa kitandani akilia na kuanza kumvuruta kumtoa nje.


Mwanangu alianza kulia akiita huku akipiga kelele Mamaaa! Mamaaa! alijaribu kujitoa mikononi mwa Baba yake lakini alizidiwa nguvu, alimburuza kama mnyama mpaka nje, huku akimuambia 


“Tulia! Mama yako hakujali, anaondoka wewe utabaki hapa na mimi Baba yako!” alitoka haraka haraka huku akifunga mlango kwa nguvu, nilijikuta nanyong’onyea, nguvu ziliniishia nilishindwa hata kunyanyua nguo kupanga tena nilijikuta nakaa chini…


Unadhani ataondoka na kumuacha mtoto wake? 

Credit; IDD Makengo

ITAENDELEA…..

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top