NDOA YANGU, PIGO LA MUNGU; SEHEMU YA KWANZA

0

Ingawa siku zote nilitamani sana mume wangu kupata mtoto lakini niliumia sana nilipozipata habari zile, namna nilivyozipata na ile hali kuwa si mimi niliweza kumpa mtoto ilinifanya kuchanganyikiwa kabisa.

Ulikuwa ni ujumbe katika simu yangu kwa njia ya Whatsapp kutoka kwa wifi yangu ambaye muda mrefu kama ndugu wengine wa mume wangu walikuwa wakinipiga vita kwa kushindwa kumpatia kaka yao mtoto.

"Sasa hivi utaondoka tu wanaingia watu na vizazi vyao..." Ulisomeka ujumbe ule ukiambatana na picha kama kumi hivi za mume wangu akiwa na mwanamke mwingine ndugu zake na mtoto mchanga.

Kusema kweli nilifurahi hasa nilipoliona tabasamu la mume wangu na namna alivyomshikilia yule mtoto, nilikuwa sijawahi kumuona mume wangu akiwa na furaha namna ile.

Katika kipindi chote cha kuishi naye, miaka mitatu kama mpenzi na miaka saba ndani ya ndoa sikuweza kumuona akiwa amefurahi namna ile. Nilifurahi kwaajili yake lakini wakati huo huo niliumia kwani nilitamani mimi ndiyo ningempa yule mtoto.

Mume wangu hakuniambia chochote kuhusu mtoto, siku na miezi ilipita bila kuniambia, nilitamani kumuuliza lakini nilijua italeta ugomvi, hivyo na mimi nilijifanya kutokujua chochote ingawa nilikuwa nikiumia sana.

Alianza tabia ya kuchelewa na nilipomuuliza alisema tu kazi nyingi, alirudi kachoka kuliko kawaida yake, sikutaka kumchokonoa sana kwani nilijua sababu na nilijua kama ningeleta kiherehere ningefukuzwa.

Siku moja alikuja Mama mkwe akiwa ameongozana na wifi yangu pamoja na yule mwanamke aliyezaa na mume wangu, hawakuwa na mtoto. Nilimtambua kutoka kwanye picha lakini nilijifanya kutokujua chochote.


Niliwakaribisha vizuri, mume wangu alikuwa bado hajarejea kutoka kazini lakini ulikuwa ndiyo muda wake. Niliwakaribisha na wakati nikiwaandalia juice kwani kulikuwa na joto sana ile narejea sebuleni sikuwakuta.

Nilijua wameondoka hivyo nilitoka nje kuwaangalia lakini sikuwaona, nilitoka mpaka nje ya geti lakini sikuwaona, nikasema potelea ya mbali nikarudi ndani, ile naingia nawakuta wanazunguka zunguka mule ndani kujaribu kufungua kila chumba.

Mama mkwe na wifi yangu walikuwa wakimuonesha nyumba yule mwanamke, wakimuambia nyumba kubwa, wakimuonesha chumba chake, ambacho ni chumba nilichokuwa nikilala mimi na mume wangu wakimuaonesha chumba ambacho anaweza kukifanya cha watoto.

Niliwaangalia kwa hasira mpaka walipomaliza na kurudi kukaa, sikusema chochote, ulitawala ukimya kidogo mpaka wifi yangu aliposema.

"Nilikuambia utatoka tu, wenye vizazi vyao wanaingia. Nyumba kama hii inahitaji watoto sio watu wa kukaa tu...!"

Nilitamani nimjibu lakini nilijizuia, nilijua ningenyanyua mdomo ningemtandika na makofi. Waliendelea kujiongelesha ili kunipandisha hasira lakini sikuwajibu chochote, niliamua kufanya hivyo wala sikuondoka, nilikuwa nimechoka na maneno yao na nilikuwa nikimsubiri mume wangu kuja pale.

Haikuchukua muda mume wangu alirejea, alishtuka sana kuwaona kwani bado alikuwa hajaniambia chochote. Aliwasalimia huku akijifanya kutokumjua yule mwanamke.


"Msalimie vizuri mzazi mwenzako..." Mama yake alimuamrisha baada ya kuona kama anazunga, mume wangu hakufurahishwa na ile hali, alimshika Mama yake mkono na kutoka naye nje. Waliongea kama dakika kumi hivi kisha wakarudi.

Mama mkwe alirudi akisema “Twendeni! Twendeni! Huyu ameshalogwa.." Aliongea kwa hasira huku akiwashika wifi na yule mwanamke na kuondoka nao. Rohoni nilitabasamu kichwani nilijua mume wangu kamuweka sehemu yake na kamkatalia.

Baada ya kuondoka nilitegemea kusikia msamaha kutoka kwa mume wangu, nilishajiandaa kumsamehe kwani nilijua siwezi pata mtoto na kama mwanaume ilikuwa ni lazima angetafuta mtoto. Mume wangu aliniambia nikae huku akionge kistaarabu alisema.

"Sikutegemea iwe hivi kwani nakupenda sana, lakini kama unavyoona hali si shwari, tumekaa kwenye ndoa miaka saba bila mtoto na mimi nilichoka kuonekana kama si mwanaume kamili..."

Alitulia kidogo kisha kuendelea. "Nilitoka nje ya ndoa na nimebahatika kupata mtoto..." Nilitamani kumuambia kuwa namuelewa na nipo tayari kumlea mtoto kama wangu lakini hakuniruhusu aliendelea.

"Yule aliyekuja na Mama ni Mama wa mtoto wangu, tuna mtoto wa miezi mitano sasa, tumekuwa tukiishi mbali lakini naona siwezi tena, mwanangu anahitaji malezi ya Baba na Mama hivyo naamini ni wakati nimchukue.

Nimepata wakati mgumu sana kujua namna ya kukuambia ila ni lazima uondoke kwani hamuwezi kuishi wote hapa na kusema kweli siwezi kuishi mbali na mwanangu. Nakupenda sana lakini ndiyo hivyo ni wakati tuachane kila mmoja aendelee na maisha yake"

Alimaliza kuongea maneno ambayo yaliniziba mdomo, ingawa nilishahisi lakini sikuamini kuwa ninaachwa, nilishindwa hata kuongea nikabaki nimeduwaa, nilitamani kulia lakini hata chozi halikutoka…. 

Unataka kujua nini kitatokea

*****ITAENDELEA

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top