PUMZIKA KWA AMANI MUME WANGU ---- SEHEMU YA KWANZA

0

Nilianza kujisikia vibaya hata kabla ya kufunga ndoa. Nakumbuka miezi mitatu kabla wakati tukiwa katika maandalizi ya Bashiri kuja nyumbani kuleta mahari miguu ilianza kuuma kiasi cha kushindwa hata kutembea. Mama alinikanda mara kwa mara na ilikuwa ikivimba na kutoa maji kama vile jasho lakini la baridi. Nilienda hospitali zote lakini sikugundulika na kitu chochote, nilipewa dawa tu za maumivu ambazo kusema kweli hazikusaidia chochote. 


Ndiyo nilikuwa nimemaliza chuo hivyo hata mchakato wa kuzunguka  kutafuta kazi ilibidi niusimamishe, Bashiri alinipa moyo na kuniambia kuwa kazi nitapata tu nishughulikie afya yangu kwanza.


Nilifuata ushauri wake na mipango iliendelea huku nikipata nafuu na kuzidiwa, napata nafuu nazidiwa hivyo yani. Kutokana na hali yangu tuliamua kuchanganya sherehe zote kwa maana ya Send off na Reception.


Kitchen Party ilifanyika kwa watu wachache na muda wote nilikuwa nimekaa. Siku ya sherehe niliingia ukumbini vizuri, sherehe ikaanza tukakata keki, tukala chakula lakini zawadi kule kusimama kupokea zawadi nilishindwa kabisa.


Miguu ilikuwa inawaka moto huku ikitoa jasho la baridi, sijui nini kilikuwa kikiendelea huko chini kwani viatu nilivyokuwa nimevaa vilijaa maji, niliwekewa kiti na MC akasema maharusi wakae na alipoona nimezidiwa alisema watu wacheze mziki na maharusi tuachwe wakapumzike. Watu hawakuelewa chochote kwani ingawa nilishindwa hata kunyanyuka lakini MC alikuwa mjanja.


Aliongea kuwa Bwana Bashiri sasa hembu mbebe mke wako kuonesha upendo kuwa utamlinda na kubeba katika maisha yako yote. Mume wangu alininyanyua na kunibeba kunitoa nje.


Nililazimisha tabasamu mpaka nilipoingia kwenye gari ambapo moja kwa moja tulielekea Muhimbili ambapo nilikaa kwa wiki mbili bila kupata nafuu yoyote. Walishindwa kwani walikuwa hawajui ni kitu gani kilikuwa kikisababisha hali ile.


Miguu ilikuwa inauma kwenye mifupa, mwanzoni ilikuwa ni mpaka magotini lakini kadri siku zilivyokuwa zikienda maumiivu yalipanda mpaka kiunoni. Mbali na maumivu nilikuwa nikitokwa na jasho la baridi kama maji, yaani nikilalia shuka au nikivaa nguo baada ya masaa mawili nakuwa kama nimemwagiwa maji. Mwili unachemka lakini natoa jasho la baridi.


Kutokana na maumivu sikuweza kufanya chochote, hata kunyanyuka kwenda kujisaidia ilikuwa shida hivyo mume wangu alikuwa na kazi ya kunibeba kila siku mpaka chooni na kunisafisha. 


Anapokuwa kazini tulikuwa na mfanyakazi ambaye alikuwa akinisaidia kama kunikausha maji lakini alikuwa hawezi kuninyanyua hivyo kazi zote za kunibadilisha na kunisafisha ilikuwa juu ya mume wangu.


Mwaka uliisha nikiwa katika hali ile, mume wangu alijitahidi sana akauza na viwanja vyake alivyonunua kipindi cha ujana na kunipeleka mpaka India lakini haikusaidia, nilipewa dawa tu kwaajili ya kukausha jasho ambazo zilisaidia kidogo lakini maumivu yalikuwa hayakomi, sana sana mwili ulikuwa unakakamaa tu.


*****


Yale hayakuwa aina ya maisha ambayo nilipanga kuishi katika ndoa, kila nilichokuwa nikikiwaza kilikuwa kinyume chake, nilimuonea sana mume wangu huruma kwani badala ya kuwa mume alibadilika na kuwa nesi. 


Muda ulikuwa unaenda na kama mtoto wa kwanza nyumbani kwao wazazi walishakata tamaa, walihitaji mjukuu na kila siku walimsumbua kutafuta mke mwingine.


Hata mimi nilitamani aoe mke mwingina au hata atafute kimada wa kumtuliza hisia zake kwani tangu kuoana tulikuwa hatujakutana kimwili, kamba mwaka uliisha bila mimi na mume wangu kufanya mapenzi. 


Siku moja uvumilivu ulinishinda na nikiwa katika maumivu makali nilimshauri kuwasikiliza ndugu zake na kutafuta hata mwanamke wa kuzaa naye tu kwani mimi sikuwa na dalili za kupona.


Aliniangalia kwa huzuni kisha akaniuliza. “Unataka kuniambia kama ni mimi ningekuwa kwenye hali hiyo na wewe ungeniacha ukatafuta mwanaume mwingine?’ Jibu lake lilikuwa rahisi “Hapana, wewe ni mume wangu nakupenda sana…” 


Niliongea kwa suti ya unyonge lakini ya kumaanisha. “Sasa kama ni hivyo mbona mimi unataka nikusaliti….” Nilitulia kidogo na kumuambia “Lakini wewe ni mwanaume, una hisia, sisi wanawake tunaweza kuvumilia, lakini wewe ni mwanaume, wazazi wako wanataka wajukuu.


Mimi siwezi kupona leo wala kesho oa mwanamke mwingine hata kama hutaniacha nitafurahi kukuona unafuraha…” Nilijitahidi kujibu kwa sauti ya kutetemeka na ya kukata tamaa. Bashiru aliniangalia machoni kwa muda mrefu kisha akaniuliza.


“Hivi kuna fomu ambazo ulijaza kufanya maombi ya huu ugonjwa kwa Mungu?” Aliniuliza swali ambalo sikupata jibu… “Mimi ndiyo napaswa kukuonea huruma kutokana na maumivu uliyonayo sio wewe kunionea huruma eti nahitaji mwanamke wakutuliza hisia zangu au mtoto ili na mimi nionekane mwanaume!


Kama siwezi kuvumilia hisia za mwili wangu kwa sababu ya ugonjwa basi sipaswi hata kuitwa mwanaume achilia mbali mume wako!” Aliongea maneno ambayo yalinipa faraja na kunifanya niandelee kupigana bila kukata tamaa.


Miaka miwili ilipita hali yangu ikiwa bado haijatengamaa, nilitamani kukata tamaa lakini kila siku mume wangu alinipa nguvu ya kuendelea kupambana. 


Tulienda kwenye maombi na kutumia dawa mbalimbali za hospitalini na za kienyeji lakini haikusaidia. Watu wengi waliamini nimelogwa lakini kutokana na imani tulimkabidhi Mungu awe muamuzi wa yote.


Siku moja mume wangu alikuja na Mzee mmoja pale nyumbani, wakati huo sikuwa najua alimpatia wapi lakini yule mzee alikaa nyumbani pale kwa miezi sita akiondoka mara moja moja na kukaa kama siku nne tano na kurejea. 


Alikuwa akija na dawa za kienyeji za kunikanda, kunichemshia na kunywa, dawa zilikuwa chungu na kusema kweli ilikuwa kama adhabu kwani ilikuwa kutwa mara tatu na kukandwa tena dawa za moto.


ITAENDELEA….. (Je unadhani atapona, kwanini ameanza na pumzika kwa amani…usikose sehemu ya pili).


NB;

(Haki miliki ya stories hii in IDD Makengo)

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top