PUMZIKA KWA AMANI MUME WANGU---SEHEMU YA PILI

0

Ukichanganya na maumivu basi ilikuwa kazi sana lakini sikuwa na namna nilivumilia. Kweli miezi sita ile nilianza kupata nafuu, maumivu yaliisha kabisa ingawa bado nilikuwa siwezi kunyanyuka, miguu haikuwa ikitoa maji tena wala kukakamaa niliweza kukunja lakini sikuwa na nguvu ya kusimama. 

Baada ya kupata nafuu ile yule mzee alituambia kuwa ameshafanya yake yaliyo ndani ya uwezo wake sasa kilichobaki ni kumuachia Mungu, alinipa dawa za kunywa na kumpa mume wangu jukumu la kunifanyisha mazoezi

****

Hali yangu ilianza kutengamaa, kila siku asubuhi na jioni mume wangu alikuwa akinifanyisha mazoezi. Kwa mara ya kwanza tangu kuingia kwenye ndoa, niliweza kumuangalia mume wangu na kuanza kumuona kama alivyo bila maumivu. 

Siku moja wakati akinifanyisha mazoezi, nilimkodolea macho, alikuwa amekonda kupita kiasi, kusema kweli kila siku nilikuwa naye lakini siku ile ndiyo niliona tofauti.

Yaani alikuwa amepungua na kuwa kama mtoto, uso wake ulionekana hauna nuru ingawa kila mara alikuwa akilazimishia tabasamu lakini alionekana kweli na mawazo. 

Nilijipa moyo nikiamini labda ni sababu ya ugonjwa wangu ndiyo ulikuwa unammaliza kutokana na mawazo, siku nilimuomba kuangalia picha zetu za harusi kweli alikuwa amekonda sana kuliko hata nilivyowaza awali.

Nilishindwa kuvumilia na kumuuliza nini kilikuwa kinamsumbua tofauti na hali yangu, aliishia kutabasamu na kusema hakuna kitu ni maisha tu nikipona na yeye atakuwa sawa. Lakini ukweli mume wangu hakuja kuwa sawa tena. 

Siku moja mume wangu aliingia chumbani, nilishaanza kupata nafuu ingawa bado nilikuwa siwezi kunyanyuka wala kufanya chochote. Alionekana kuwa na huzuni kuliko kawaida yake, ingawa alijaribu kutabasamu lakini nilimuona kabisa akilengwa lengwa na machozi. 

Aliongea na kunikalisha kitandani kisha na yeye akakaa pembeni yangu na kuniambia. “Mke wangu kuna kitu naomba unisaidie, yaani uniahidi kukifanya, nakuomba sana unahidi kitu hicho na hata iweje usije kubadilisha mawazo, naomba sana…”

Aliongea huku akilengwa lengwa na machozi, nilimuambia hakuna hata haja ya kuuliza nilikuwa tayari kufanya kitu chochote. Alisisitiza niahidi kufanya na mimi niliahidi huku nikinyanyua mikono yangu kumkumbatia. 

“Mke wangu naomba nikifa uolewe tena na kama Mungu akikujalia mtoto basi kama ni wa kiume umpe jina langu na kama ni wa kike basi jina la kati liwe la kwangu…”

Aliongea machozi yakimtoka, sikutaka kumsikiliza kwanini anaongelea kufa nilijaribu kumtuliza lakini aliniomba nimuahidi hicho kitu. Alirudia zaidi ya mara kumi ndipo nilipomuahidi kuwa nitafanya hivyo. 

Baada ya kumuahidi aliniambia kuwa yeye hawezi ishi muda mrefu, aliamua kunificha lakini anajua hana muda hivyo kuamua kuniambia. Mwaka mmoja uliopita aligundulika kuwa ana kansa ya damu na ilikuwa katika hatua mbaya.

Hakutaka kuniambia kutokana na ugonjwa wangu lakini Daktari aliyekuwa anamhudumia alimuambia kuwa hana zaidi ya mwaka ila mpaka wakati ananiambia ilikuwa ni karibu miaka mwili kitu ambacho ilikuwa ni kama miujiza. 

Aliniambia hajisikii vizuri na kaamua kuniambia kwani hata nguvu ya kunihudumia hana tena. Kweli mume wangu alikuwa amechoka na hali yake ilikuwa mbaya.

Sijui nilipata wapi nguvu lakini nilijikuta nasimama, ingawa sikusimama kwa muda mrefu lakini sikutaka kulia, nilijitahidi kuzuia machozi na kumkumbatia mume wangu. 

Ilikuwa ni karibu miaka mitatu tangu tuoane na katika muda wote huo tulikuwa hata hatujakutana kimwili, alivumilia ugonjwa wangu tangu siku ya kwanza ya ndoa yetu na mimi nilimuomba Mungu anipe nguvu hata niwezie kumhudumia lakini haikutokea. Sikuweza kusimama tena mpaka sasa wakati naandika hapa.

Ingawa nimeweza kupona lakini magoti yangu hayana nguvu kuubeba mwili wangu hivyo nalazimika kutumia kiti cha magurudumu. Mume wangu alifariki mwezi mmoja baada tu ya kunipa zile taarifa na kila siku katika mwezi huo alisisitiza niolewe ili niwe na furaha. 

Ni mwaka wa pili sasa, sijaolewa na sidhani kama nitakuja kuwa na furaha, naweza kufanya kazi zangu lakini sijui kama nitaweza kuufungua moyo wangu tena.

******

Kila siku maneno ya mume wangu hunijia, najua alitaka niwe na furaha na kila siku na muomba anipe mwanaume wa kunipa furaha. Natamani sana nimzalie mtoto ili tu abebe jina lake, nadhani hicho ndiyo kitu ambacho kinanipa nguvu mpaka sasa. 

Mungu alinipa Mume akanipa na Nesi. Alijitoa kwaajili yangu akiwa mzima na hata baada ya kugundua kuwa ni mgonjwa aliweka ugonjwa wangu mbele na kunihudumia mimi kwanza.

Natamani kuandika mengi ila leo niishie hapa. Lengo la kuandika kisa changu hiki ni kuwaasa tu nyie mlioko katika ndoa kuwa msipoteze muda wenu katika kunyanyasana na kuudhiana, katika kugombana, kuna muda mchache sana wa kupendana na kila siku utakuwa ukijuta kama hukumpenda mwenza wako ipasavyo. 

Mapenzi ni furaha, ingawa ndoa yangu yote ilikuwa ya mateso lakini yalikuwa ni mateso ya ugonjwa, ilikuwa ni ndoa ya amani na mume wangu kila siku alihakikisha natabasamu.

Alifanya kila kitu ili kuhakikisha kuwa nina furaha hakuchoka kunifanya nitabasamu hata nikiwa katikati ya maumivu makali. Nakumbuka alijua napenda sana kuvaa viatu virefu hivyo karibu kila mwezi aliniletea zawadi ya viatu na kila viatu vipya vilipotoka alikuwa akiniletea. 

Alivipanga ndani na kuniambia hakutaka fasheni inipite hivyo nikipona nitavaa vyote. Mpaka sasa sijaweza kuvivaa kwani bado sijaweza kutembea ila naamini ipo siku Mungu atanisimamisha na nitaweza kutembea na nitavivaa vyote kwaajili yake.


Naomba nimalizie hapa, samahanini kwa stori ndefu nitafurahi sana kama utatumia sekunde chache kushea  stori yangu. Lengo langu ni kwa yule anayesoma awe mwanamke au mwanaume kumpenda sana mtu aliyenaye na kumuonyesha mapenzi ya kweli kwani siku akiondoka utatafuta mtu wa kumuonesha mapenzi itashindikana. 

Mimi nina mambo mengi ya kumkumbuka Mume wangu, hembu jiulize wewe ukiondoka leo mume au mke wako atakukumbuka kwanini? Atakukumbuka kwa mazuri au mateso uliyompa?

Ahsante sana kaka, huwa natumia muda wangu mwingi kwenye ukurasa wako nikisoma unachoandika kuhusu mapenzi. Watu wengi wanachezea upendo wanaooneshwa leo kwa kuwa wanadhani labda hautakoma, siku ukikoma ndipo watajuta. 

Mungu awabariki wote na awasaidie msije kujuta kwa mnayowafanyia wapenzi wenu bali muwatengenezee kumbukumbu nzuri na kuwapa faraja kila siku.

Kumbuka kuna siku utatamani kumuambia mkeo au mumeo unampenda lakini hatakuwepo kukusikia, kuna siku utatamani kumnunulia zawadi na kumpa tabasamu, kuna siku utatamani kutoka na familia nzima kufurahia maisha lakini mwenza wako hatakuwepo. 

Kwanini unatumia muda wako mwingi kutengeneza ugomvi, chuki na manyanyaso kwa mwenza wako. Ahsante sana kaka Iddi kwa kukubali kukiandika kisa changu na kunisikiliza, Mungu awabariki wote mliosoma kisa hiki na kitumieni kusambaza upendo.


***MWISHO***

Na Iddy Makengo

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top