Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma linawashikilia Watu watatu akiwemo Baba mzazi Kulwa Juakali (40) Mkazi wa kijijicha Lufubu Wilaya ya Uvinza kwa tuhuma za kumpiga fimbo Mtoto wake Mbaru Juakali ( 17) hadi kusababisha kifo chake huku chanzo cha tukio hilo kikidaiwa kuwa ni kumlazimisha Mtoto huyo kuolewa chini ya umri kwa mahari ya ng'ombe 13 bila ridhaa yake.
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani humo ACP James Manyama amesema tukio la mauaji lilitokea tarehe 10 novemba mwaka huu majira ya Saa mbili asubuhi katika kijiji hicho ambapo amesema binti Hugo aliuawawa baada ya kujeruhiwa kwa fimbo.
"Binti alipigwa sehemu mbalimbali za mwili wake akilazimishwa kuolewa ambapo kulikua na ahadi ya kulipwa mahari ya ng'ombe 13 na waliokua wakishinikiza aolewe ni wazazi na hao ndio walikua na uroho wa kupokea mahari ya hao ng'ombe 13, taarifa zilizopo binti huyu alikua anachumbiwa na Wanaume watatu kwa hiyo yule ambae ofa yae ilikuwa kubwa kwa ng'ombe 13 huyo ndio alikua analazimishwa aolewe nae wakati binti hakuridhia na kupelekea kipigo" amesema Manyama
Polisi Mkoani Kigoma wanasema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na Watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani kwa hatua za kisheria akiwemo Baba mzazi Kulwa Juakali (40), Baba mkubwa wa marehemu Shija Juakali (44) na Baba mdogo wa marehemu aitwaye Majiba Juakali ( 29) wote wakazi wa kijiji cha Lufubu wilayani Uvinza mkoani Kigoma.