NDOA YANGU, PIGO LA MUNGU; SEHEMU YA PILI

0

(Inaendeleaa, kutoka sehemu mume wangu aliniambia tuachane kwa kuwa alishapata mtoto na mwanamke mwingine baada ya ndoa yetu ya miaka saba)

Sijui nini kilinitokea lakini nilijikuta naingia chumbani na kuanza kukusanya nguo zangu, nilikuwa kama chizi, nilikusanya nguo zangu chache nakutoka na begi na pochi yangu ndogo ambayo niliichukua tu sikujua hata ina nini ndani. 


Sikusema chochote, sikulia wala kulalamika, nilikuwa kama nimepigwa shoti ya umeme. Mume wangu alinifuata na kuniambia sikutakiwa kuondoka wakati ule ningeweza kulala pale lakini sikunyanyua hata mdomo, alijiongelesha maneno mengi lakini hata hayakuingia masikioni ni kama nilikuwa sipo pale.


Nilisukuma begi langu mpaka getini nikatoka na kuanza kutembea kusikojulikana, kwa kifupi nilikuwa sijielewi, mume wangu alinifuata nyuma akinibembeleza kurudi lakini sikumsikiliza, niliona Bajaji inakuja nikaisimamisha na kupanda.


Bado mume wangu alikuwa akinikimbilia na alisimama pembeni ya Bajaji kujaribu kunizuia akisema tuongee kiutu uzima lakini sikumsikiliza nilimuamuru Dereva wa Bajaji aondoke na yeye alinisikiliza.


“Tunaelekea wapi Dada?” Aliniuliza dereva, sikuwa na jibu nilikaa kimya kwa muda wa kama dakika kumi , aliendelea kuendesha mpaka alipofika sehemu nzuri akapaki kisha akanigeukia na kuniuliza tena. 


“Hata sijui mdogo wangu, wewe endesha tu…” Nilimjibu huku nikitoa noti tano za elfu kumi katika pochi yangu, nilimuambia akaongeze mafuta kisha tuanze kuzunguka mpaka nitakapo choka.

Kusema kweli sikuwa nikijua ni wapi pa kwenda, sikuwa na ndugu Mwanza zaidi ya marafiki tu ambao hata hawakua marafiki zangu wa karibu kihivyo. Nilitaka kutoa simu ili kumpigia Mama yangu nimuelezee kilichotokea lakini niligundua kuwa sikubeba simu, niliiacha nyumbani hivyo nilitulia tu.


Tulizunguka kwa muda wa kama masaa mawili, giza lilishaingia na Kaka wa watu alikuwa bado hajui naenda wapi? Alishajua kilichotokea kwani nikiwa ndani ya Bajaji bila kujijua nilikuwa nalia huku nikiongea mwenyewe, Kaka wa watu alinisikiliza bila kuchoka wala kusema chochote.

Baada ya kuona nimechoka nimenyamaza alisimamisha Bajaji katika nyumba ya kulala wageni, alienda kuchukua chumba na kuja kunichukua. “Dada pumzika hapa ukiwaza nini cha kufanya, ukiendelea kuzunguka hivi vijana wanaweza hata kukuibia, usiku huu…”


Aliongea kwa upole huku akinishika mkono kunitoa ndani ya Bajaji, alichukua begi langu na kulipeleka mpaka kwenye chumba alichochukua. Aliniuliza nataka kula nini nikasema nimeshiba lakini hakukubali, alitoka na kwenda kuchukua Chips Kuku na soda kisha kuniletea, alikaa pale na kunilazimisha kula mpaka nikamaliza.

Yule kijana alikuwa akiitwa Nick, kusema kweli alikuwa mchangamfu na aliongea maneno mengi sana kiasi cha kunifanya nisahau kidogo shida zangu. Nilikuwa mkubwa kidogo kwake nikimzidi kama miaka mitatu hivi. 


Baada ya mimi kumaliza kula aliniaga huku akiandika namba yake ya simu kwenye kikaratasi na kuniachia. “Dada nitapita baadaye kukuangalia, sasahivi ngoja nikakamilishe hesabu…” Aliongea huku akiweka ile elfu hamsini niliyompa pale mezani.

Nilimuambia achukue ni zake kwaajili ya muda niliompotezea alinijibu kwa upole “Dada unazihitaji kuliko mimi, angekuwa ni Dada yangu kafanyiwa hivyo ningependa mtu atakayekutana naye amsaidie..” 


Aliongea na kuondoka, nilimuangalia machozi yalinitoka. Sikulia kwasababu ya mume wangu bali kwasababu ya kitu alichokuwa amenifanyia, ni muda mrefu ulikuwa umepita kufanyiwa kitu cha kiubinadamu namna ile. Wakati huo ilikuwa ni kama saa mbili usiku kwani niliwasha TV na kukutana na taarifa ya habari.


Nilikaa tu pale kitandani nikiwa sina hili wala lile, nilijikuta naanza kulia tena kama mtoto, nililia sana lakini baada ya muda niliona nitakufa kwa mawazo niliamua kutoka kwani kwenye ile nyumba ya wageni kulikuwa na baa. Niliagiza mzinga mkubwa wa Konyagi na kuanza kunywa.

Ingawa nakunywa pombe lakini si mnywaji sana mara nyingi huwa nakunywa wine lakini siku ile nilitaka kulewa haraka haraka, na kweli nililewa kwani ule mzinga nilikuwa nikiunywa kama maji. Kulikuwa na mziki unapigwa pale hivyo nilinyanyuka na kucheza mara kwa mara.


Katika meza niliyokuwa nimekaa kulikuwa na wakaka wawili waliokuja kukaa pale na baada ya muda tulizoeana na kuanza kuongea kama vile tunafahamiana, mmoja wao alianza kunitongoza na kwa namna nilivyokuwa nikinywa walijua kabisa ni malaya nimeenda kutega. 


Sijui ni pombe, maumivu ya kuachwa au kukata tamaa na maisha lakini nilijikuta namkubalia na kumuambia kuwa nimechukua chumba pale. Ndiyo katika miaka kumi nilikuwa tayari kufanya mapenzi na mwanaume tofauti na mume wangu na wala sikuhisi kitu kibaya.


Alikataa nakusema kuwa tunaondoka wote, alitaka tubadilishe kijiwe twende sehemu nyingine sikubisha nilinyanyuka huku nikiwasisitizia tuondoke, yaani mimi ndiyo nilikuwa na haraka ya kuondoka kuliko wao, bila kukumbuka kama chumba nimefunga au la nilikuwa tayari kuondoka tulinyanyuka na kuanza kuondoka.


******

Wale wakaka walilipa bili tukaanza kutoka, ilibidi wanisaidie kutembea kwani sikuweza hata kusimama vizuri. Walikuwa na gari na walinikokota mpaka karibu na gari yao, kabla ya kufungua mlango na kuingi kuna Bajaji ilipaki pembeni, alikuwa ni Nick yule dereva wa Bajaji aliyenipeleka pale.


Aliniona na kushuka haraka haraka, aliingilia kati na kuwauliza wananipeleka wapi? Wale wakaka walimkoromea kumuuliza kuwa yeye ni nani. Nick alisema mimi ni mkewe na siwezi kuondoka nao. Wale wakaka walianza kumtukana kwa dharau kuwa hawezi kuwa na mwanamke kama mimi, waliniuliza nikasema simfahamu.


Mmoja wao alimsukuma Nick ambaye alipepesuka na kuangukia kwenye jiwe lililokuwa pembeni, alinyanyuka huku akichechemea. Hakuwafuata tena alirudi kwenye Bajaji yake, wale wakaka walianza kuniingiza kwenye gari yao, Nick hakuondoka, kumbe alienda kutoa sime kubwa kwenye bajaji yake na kuwarudia.


“Broo nitawageuza mishikaki sasa hivi, muacheni huyo Dada?” Aliongea kwa kujiamini lakini wale vijana kutokana na pombe waliendelea kubisha, Nick hakuwa na utani, aliinyanyua ile sime na sijui alifanyaje lakini kaka mmoja alianza kupiga kelele za maumivu huku akishika kifua, Nick alimchana kwa sime yule Kaka kifuani. 


Yule mwingine aliyekuwa amenishikilia kuona vile alinisukuma pembeni na kutaka kwenda kumuokoa mwenzake lakini Nick alikuwa mjanja alirudi kwa nyuma na kuanza kuwatishia, sasa madereva wa Bodaboda walishajazana na kuanza kumshangilia Nick wakiwatukana wale akina kaka.

Kuona vile wale akina Kaka waliingia kwenye gari yao na kuondoka. Nick alinichukua na kunipeleka ndani, alinilaza kitandani ambapo dakika mbili tu nililala fofofo.


*******

Nilishtuka asubuhi kichwa kinauma balaa, nilikuwa najisikia vibaya na kabla ya kufanya chochote nilielekea chooni ambapo nilianza kutapika, yaani nilitapika kwa zaidi nusu saa, kila nikirudi kulala natapika, hali ilikuwa mbaya na nilianza kujutia zile pombe.


Baada ya muda kutapika kuliisha, nilioga na kubadili nguo, niliamua kutoka ili nipate chochote na kwa kuwa kulikuwa na baa pale basi kulikuwa na supu, nilipiga bakuli la supu na malimau ya kutosha baada ya kushiba nilirudi ndani.


Nilianza kujisikia sawa na nilianza kukumbuka yaliyonitokea, sikutaka kulia tena nilianza kuwaza namna ya kuwasiliana na nyumbani kwani sikuwa na simu na nilihisi labda mume wangu kawapigia kuuliza kama nimewasiliana nao na wangekuwa na wasiwasi sana.


NIlitoka nje na kumfuata mhudumu mmoja, nilimuomba simu yake kuongea na mtu, ilikuwa haina salio hivyo nilitoa noti ya elfu kumi alinipa nikajiunga kisha nikampigia Mama. Kumbe mume wangu hata hakuwapigia kuwaambia kuwa sipo nyumbani, tuliongea mengi akanishauri nirudi Dar, nilimuambia sitaweza nataka nikaonane na mume wangu nijue nini kitaendelea, alikataa katakata na kusema atamtuma mdogo wangu wa kiume kuja kunichukua.


Basi tuliagana na wakati huo Nick alikuwa ameshafika, alinisalimia, nilimjibu kwa aibu kutokana na mambo niliyoyafanya jana yake. Alinitania tu huku akicheka na kunipigia story za kunichangamsha, aliniuliza kama nimewasiliana na ndugu zangu nikamuambia ndiyo, alitoa simu yake moja na kunipa akiniambia niitumie kwa kipindi hicho.


Aliniaga kuwa anaenda kutafuta riziki na kuniambia kama nitahitaji chochote nimpigie, nilimuambia niko sawa. Nilirudi ndani mpweke nikitamani kumpigia mume wangu lakini nilisita. Siku ile ilienda nikiwa na mawazo sana, Nick alikuja baadaye tukaongea sana, tulishaanza kuwa marafiki alikaa mpaka usiku wa manane na kuaga kuondoka.


Sijui kwanini lakini alipoondoka nilianza kujisikia vibaya, jana yake nilikuwa nimelewa sana lakini hakunigusa hata kidogo na siku ile tulikaa na kuongea wawili tu chumbani lakini hakunigusa. Sio kwamba nilitaka kufanya naye mapenzi lakini nilitaka hata anitamani.


Nilianza kujihisi kama mbaya, nilipoteza kujiamini na kila mara nilijiangalia kwenye kioo kama nina kasoro. Mara zote aliniita Dada kitu ambacho nilipokuja kufikiri baadaye kiliniumiza kwani nilijiona kama mzee sana ingawa ndiyo nilikuwa na miaka 32 na siku zote nilijihisi bado mbichi.


Nilijikuta nakata tamaa, usingizi ulipotea nikabaki na mawazo, sikuwa nikiwaza sana ndoa bali kuzeeka kwangu, wakati mwingine nilimtetea mume wangu kuwa labda ameniacha sababu ya uzee na si kutokuzaa, niliumia sana.


Niliamka na kuanza kujaribu nguo zote nilizokuwa nazo kujiangalia kama ni mzuri. Sijui kwanini lakini nilitamani Nick hata angenigusa au kuniangalia kwa kunitamani na si kuniangalia kama Dada yake, nilijikuta nalia, nalia kwa kuzeeka.


******

Siku iliyofuata Nick alikuja asubuhi, Mdogo wangu ambaye alikuwa ni umri wa Nick (hata yeye nimemzidi miaka mitatu) alikuwa ashaondoka Dar na kwa kuwa alikuwa na gari binafsi nilitegemea atawahi. 


Akiwa pale nilijaribu kumtega, kujiliza nikimuegemea kuona kama nitamshawishi anitamani lakini wapi. Kusema kweli sikuwa nikimtaka kimapenzi nilitaka tu anitamani nijisikie vizuri lakini hakufanya vile, Nick alikuwa akiongea kwa heshima mpaka ilikuwa inaboa, niliumia sana.


Aliniambia anataka kunitoa nikapunge upepo lakini nilikataa, nilijifanya sitaki kuiona Mwanza, napata uchungu, ingawa haikuwa kweli, nilitaka aendelee kukaa pale labda nikiendelea kumtega atanitamani lakini wapi, tulikaa mpaka jioni mdogo wangu alipofika nilimtambulisha Nick kama rafiki yangu mtu aliyenisaidia.


Mdogo wangu ni mtu wa kuongea na mchangamfu walisalimiana na alilazimisha tutoke tukale burudani ili nichangamke, tulitoka ingawa sikunywa wao walikunywa na kweli nilifurahi. Siku iliyofuata nilikuwa naondoka, Baba alimuambia nisirudi kwa mume wangu na wala nisiwasiliane naye tena.


Tulimuaga Nick, nilichukuwa mawasiliano naye na kumuahidi kumtafuta, nilijikuta natokwa machozi kwa wema wake ambao haukuhitaji chochote, nilitaka kumpa pesa lakini alikataa na kuniambia “Wewe ni Dada yangu na haya ni maisha nafurahi uko salama hilo kwangu ni malipo tosha..” Nilijikuta natokwa na machozi tuliagana na Nick tukaanza safari ya Dar.


*****

Maisha yaliendelea, nilirudi nyumbani na kupokelewa vizuri, wiki za kwanza zilikuwa ngumu lakini nilianza kuzoea, mpaka wakati huo mume wangu alikuwa bado hajampigia ndugu yangu yeyote simu zaidi ya marafiki zangu kuwauliza kuhusu mimi. Baba aliniambia nisihangaike naye kwani kama angekuwa mwanaume kweli basi angenirudisha nyumbani mwenyewe kwa heshima kama alivyonichukua.


Nilianza kuwa na furaha ambayo ilitokana na kuongea na Nick kila siku, tulikuwa tukiongea kirafiki karibu kila kitu tukitaniana lakini bado alikuwa hajanitongoza au kuonesha dalili za kunitaka. Mwanzoni nilihisi labda ana mke lakini wapi aliniambia hana.

Nikaanza kuhisi kwamba labda ana matatizo sio riziki lakini stori zake kuhusu wanawake zilizidi kunivuta kwake, kwani kusema kweli alikuwa mtu wa majanga na kwa kuwa muda mwingi tulikuwa tukizungumza kama marafiki basi alinisimulia kila kitu, namna anavyofumaniwa, aliniambia sababu ya kutokuoa ni kushindwa kutulia na mwanamke mmoja.


Kusema kweli nilishangaa kutokana na ustaraabu aliokuwa nao lakini kwa upande wa wanawake alikuwa kicheche sana tena sio wa wanawake wa kutongoza bali wale wa siku moja kalale mbele. Nilijipa moyo labda ndiyo sababu ya yeye kukataa kunitongoza mimi kuwa ni mstaarabu sana,  ingawa bado suala la uzee lilinisumbua.


Rafiki za mdogo wangu nao walikuwa wakija kunisalimia Dada mpaka nikajikuta nakasirika kabisa. Kusema kweli ile hali ilinisumbua na kwakuwa sikuwa mtokaji, miezi mitatu baada ya kuachika sikuwahi hata kutongozwa na mtu.


******

Nilishachoka kukaa nyumbani, nilipata taarifa kuwa mume wangu kashamchukua mama wa mtoto wake na wanaishi pamoja nilizidi kupata hasira kwani nilijua kuwa mimi ndiyo basi tena. Nilitaka kutafuta kazi, miaka saba baada ya kumaliza chuo na kuamua kuwa Mama wa nyumbni nilitaka kufanya kazi.


Suala la ajira kwangu kwa Dar halikuwa shida sana kwani Baba yangu alikuwa akifahamiana na watu wengi, tatizo lilikuwa ni vyeti, kila kitu changu niliacha kwa mume wangu. Ingawa tulijenga pamoja na kununua viwanja na mali nyingi lakini Baba aliniambia nisichukue hata kijiko kwani sicho kilichokuwa kimenipeleka.


Kweli hata mimi sikutaka mali zake, sikutaka kuonana naye tena na mchakato wa talaka najua ungeniumiza kama ningetaka mali, lakini vyeti ilikwua ni lazima nikachukue kwani nisingeweza kuajiriwa bila vyeti.


Baba alitaka mdogo wangu kwenda kuchukua lakini nilikataa nilitaka kwenda mwenyewe, alitaka tuongozane naye nilikataa nikamuambia sitaki anione mdhaifu nataka aone simhitaji. Walitaka kunilazimisha lakini nilikataa na kuamua kwenda Mwanza mwenyewe.


Lakini hiyo haikuwa sababu, sikuwa nikimuwaza tena mume wangu bali Nick, bado nilikuwa naumiza kichwa kwanini hanitongozi na nilitaka kumuona, mume wangu ni kama nilishamsahau. Nilienda Mwanza na mtu wa kwanza kumtafuta alikuwa ni Nick alifurahi kuniona kwani tulishakuwa marafiki.


Alikuja kwenye Gest niliyoshukia usiku na tukaongea sana, alitaka tutoke kupunga upepo nikamuambia nataka kupafahamu kwake. Aliniambia nitafahamu tu nisubiri kesho yake, sikukubali, nilimsisitizia na kumtania kama ana mke aseme nisiende alicheka akisema yeye si muoaji.


Nilimtania tena kuwa kama hajafanya usafi asijali mimi ni mshikaji tu, alicheka zaidi na kuniambia twende. Niliingia kwenye Bajaji yake na kuanza safari ya kwenda alikokuwa akiishi. Kwanza nilipofika nje nilishangaa nyumba yenyewe, kiuhalisia kwa kazi yake nilijua anaishi uswahilini lakini haikuwa hivyo.


Alikuwa akiishi nyumba nzuri yenye geti zuri na wapangaji watatu kila mmoja akiwa na ki appatment chake chenye vyumba viwili, sebule, kajiko na choo cha ndani. Huko ndani ndiyo usiseme, TV kubwa, sofa nzuri kila kitu kilikuwa kizuri yaani sikutegemea kukuta anaishi vile.


Mpaka niliogpopa labda kulikuwa na mwanamke anaishi pale au si kwake, chumba kilikuwa kisafi balaa, aliuona mshangao wangu na kucheka huku akitania “Ulijua naishi getto?” Nilibaki nimeduwaa tu na nilishindwa na kumuambia kuwa kweli ndiyo niliwaza hivyo anaonekana msela sana kuishi vile.


“Maisha mafupi Dada yangu, tunaishi mara moja..” Nilitingisha kichwa na kusema kweli, huku nikijiambia kuwa humu sitoki. Aliniambia nakunywa kinywaji gani, bila kujijua nilijiachia kama Mama mwenye nyumba, nikaenda kwenye friji nikaangalia kulikuwa na wine na bia za kutosha tu, nlitoa chupa mbili za Castle Light na na kuziweka mezani.


Aliniangalia na kucheka, aliingia ndani kujimwagia maji akiniacha na mawazo kibao. Nilitamani hata kumvamia kule bafuni lakini nilijizuia, nilikunywa zile bia harakaharaka nikaona silewi nikaongeza nyingine mbili, baada ya kama dakika kumi na tano hivi alitoka, alishaoga na kung’aa, alivaa singlend na pens kitu kilichofanya niuone mwili wake uliojengeka kimazoezi na utanashati wake. Yaani ule udereva Bajaji wote ulimtoka, sikuvumilia nilimvamia na kumkumbatia nikimbusu mwili mzima, alijaribu kunizuia lakini nilishachanganyikiwa.


Kwanza nilikuwa na muda mrefu sijafanya mapenzi, pili nilikuwa namtamani alivyo wakati ule na tatu nilishachoka kuonekana bibi na kama unavyojua wanaume wakiguswa hawalazi damu alishindwa kuvumilia alinipa shughuli pevu. Nililala pale na kesho yake nilienda tu gest kuchukua mizigo, sikujali chochote niligeuka mama mwenye nyumba.


******

Wiki iliisha nikiwa pale, ni kama nilisahau kwenda kuchukua vyeti vyangu, nyumbani walikuwa wakinipiga kila siku kama nimechukua nawaambia bado mume wangu kasafiri akirudi nitachukua. Wiki mbili ziliisha wakawa na wasiwasi wakataka kumtuma mdogo wangu ndipo nilipoamua kwenda kuchukua.


Nilimuomba Nick kunisindikiza kwani nilitaka pia mume wangu aone kuwa nisha move on na maisha yangu. Labda niseme kitu, mimi na Nick bado tulikuwa kama marafiki kwamba nilikuwa najua kuwa hatuwezi kuwa wapenzi kwani na yeye ana mambo mengi, kusema kweli alikuwa mstaraabu lakini linapokuja suala la wanawake ni shida.


Labda niseme Nick ni wale ndugu zetu wa Bukoba, ndiyo maana hata ni mtanashati na anaishi maisha ya juu pengine kuliko kipato chake, lakini pia ndiyo sababu ni fundi na ndiyo maana hatulii, hivyo hata hizo wiki mbili nilizokaa hapo walishakuja mabinti kama watano kuja kumtafuta niliwaambia tu hayupo wakijua kweli ni Dada yake.


Nilibaki tu kucheka walivyokuwa wakimhangaikia ila kwa shughuli yake sikuwashangaa. Hakuwa na hiyana alinisindikiza, tulienda muda wa jioni muda ambao nilijua mume wangu atakuwa nyumbani, kweli tulimkuta, alishangaa kuniona, akajisemeza semeza sana maneno mengi akijua nitapaniki lakini wapi.


Nilimuambia kilichonipeleka, mwanzoni alihisi nataka mali zake hivyo akaanza kujisemesha kuwa mali zile ni zake kachuma mwenyewe sijui na mambo mengi mengi, nilimsikiliza na huyo mkewe akiniangalia kwa wasiwasi lakini muda mwingi macho yake yakiwa kwa Nick alimuangalia Nick kwa uoga huku akitetemeka tetemeka, lakini hakuongea chochote.


Baada ya mume wangu kujiongelesha nilimjibu kwa kifupi. “Sikiliza sina shida na takataka zako nimekuja kuchukua vyeti vyangu na si huu uchafu mwingine..” Niliongea kwa dharau huku nikinyanyuka na kwenda moja kwa moja chumbani kwetu, nilikuta hakuna kipya kilichobadilika zaidi ya nguo za watoto zilizokuwa chafu mule ndani, nilifungua droo ambapo naweka vitu vyangu kweli nilivikuta.


Nilichambua na kutoa vyeti vyangu, wakati huo alishakuja kanisimamia pembeni yangu, nilitoa vyeti vyangu na kuhakikisha viko sawa kisha nikanyanyuka kuondoka. Nilitoka na kumuambia Nick twende, alinyanyuka tuondoke, wakati nataka kutoka mume wangu aliniambia kuwa kuna vinguo vyako uje uchukue.


Aliongea kwa dharau na mimi nilimuangalia kwa dharau na kumuambia “Wape wale wadogo zako nao angalau wapendeze labda wataolewa..” Nilimshika Nick kiuno na kuondoka. Ile tunatoka tu nje Nick akaniuliza.

“Huyo ndiyo alikuwa mume wako?”

“Ndiyo kwanini? Unamfahamu?”

“Ndiyo, nilishawahi kumuona mitaa flani, na yule ndiyo mke wake mpya? Ndiyo amezaaa naye?”

“Ndiyo na yeye unamfahamu?”

“Ndiyo ni demu wa rafiki yangu…”

“Demu wa rafiki yako au alikuwa demu wa rafiki yako?”

“Hapana ni demu wa rafiki yangu, mpaka sasa ni demu wa rafiki yangu!”


 Unafikiri ni nini kitaendelea


*****ITAENDELEA

Haki miliki ni Iddy Makengo

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top