Mwenyekiti wa chama cha UDP John Momose Cheyo amesema hakuna haja ya kuifuta kesi ya Mwwnyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake, badala yake iachwe isikilizwe mpaka ifikie mwisho ili ukweli ujulikane
Mzee Cheyo ameyasema hayo muda mchache baada ya mwenyekiti wa kituo cha demokrasia Tanzania (TCD) Zitto Kabwe kumuomba Rais Samia kusaidia mashitaka hayo ya Mbowe yaondolewe mahakamani.
Awali Rais Samia Suluhu Hassan amevunja ukimya kuhusu kinachomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akisema kuwa demokrasia ni kuheshimu sheria.
Akizungumza Jumanne Desemba 15, 2021 wakati akifungua mkutano wa wadau kujadili demokrasia ya vyama vingi, Rais Samia amesema ni muhimu kuzingatia sheria za nchi.
Mkuu huyo wa nchi ameyasema hayo akijibu ombi la Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Zitto Kabwe aliyemuomba kusaida kuachiwa kwa Mbowe ambaye pamoja na wenzake watatu wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021 yenye mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi, inayoendelea katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Rais Samia amesema, “Nataka nijibu lile ombi la mwanangu, iko hivi demokrasia ni kuheshimu sheria, unapoheshimu sheria ndipo demokrasia inapokua, lakini pia ndipo inapoleta heshima.
“Heshima ya mtu inakuja unapoheshimu sheria za nchi, unapovunja sheria za nchi heshima yako haitaheshimiwa, Serikali haitakuheshimu lakini lazima ujue kwamba unapotumia uhuru wako mwisho wa uhuru wako inaanza heshima ya mtu mwingine,”.