Hatima ya kina Mdee kujulikana kesho

0
HATIMA ya Halima Mdee na wenzake 18 ambao wako bungeni kwa viti maalum, inatarajiwa kujulikana kesho, kwenye kikao cha Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, John Mrema, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajenda za kikao cha Baraza Kuu la chama taifa linalofanyika leo.

Aidha, katika kikao hicho Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani Uganda, National Unity Platform (NUP), Bobi Wine, atahudhuria kama mgeni mwalika.

Alisema waliokuwa wanachama wao 19 ambao walishafukuzwa na kamati kuu, hivyo waliamua kukata rufani kwenye baraza kuu, na kwamba wameshaitwa kwa barua rasmi kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa rufani walizokata.

Wabunge hao wa viti maalum waliokata rufani ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga na Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka; wengine ni Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Walifukuzwa uanachama baada ya kukaidi maelekezo ya CHADEMA ya kuwataka kutoenda bungeni, kwa madai kuwa hawakuteuliwa kihalali kuwa wabunge wa viti maalum kupitia chama hicho.

Kamati Kuu ilisema kuwa uteuzi wao uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kuwa na baraka za chama.

Ajenda nyingine ni mpango mkakati wa miaka mitano ya chama pamoja na mpango kazi wa mwaka, ambao utajadili namna watakavyo kiendesha chama hicho hadi kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na serikali za mitaa 2024.

“Hii ni baada ya baraza kuu kupokea taarifa ya uchaguzi mkuu wa 2020 na kwenye mpango mkakati huu ndipo tutakapojadili kwa kina masuala ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi na baada ya baraka kuu tutawaeleza kile ambacho tumekubaliana juu ya mambo hayo,” alisema Mrema.

Aliongeza kuwa ajenda nyingine ni ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama akisema kuwa uchaguzi mkuu wa kuchagua viongozi wa chama ratiba yake imekaribia na baraza kuu ndilo lenye mamlaka ya kutangaza tarehe rasmi ya lini wanakwenda kuanza mchakato wake utakaoanzia ngazi ya msingi, tawi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda na kuhitimishwa kwa ngazi ya taifa.

Ajenda nyingine ni uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini baada ya kufariki kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Arkado Ntagazwa, akieleza kuwa bodi hiyo ni takwa la kisheria na mwenye mamlaka ya kuteuwa wajumbe kujaza nafasi hiyo ni baraza kuu la chama.

“Kesho Baraza Kuu litakuwa na kazi ya kuteuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini kuziba nafasi ya mzee Ntagazwa pamoja na wajumbe wengine kadri watakavyoona inafaa kwasababu sheria ya bodi inataka wajumbe wasiopungua saba na wasiozidi tisa,” alisema Mrema.

Credit:Nipashe

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top