SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson wiki hii anatarajiwa kutangaza hatma ya wabunge 19 waliofukuzwa uwanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wabunge 19 wa Chadema wakiongozwa na Halima Mdee wameshindwa rufaa ya kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua uanachama.
Baraza Kuu la chama hicho lilipiga kura kuridhia uamuzi wa kamati hiyo.
Baada ya uamuzi huo, baadhi wabunge hao walihudhuria vikao vya Bunge.
Wabunge walioingia bungeni na kushuhudiwa na gazeti la habari Leo ni, Esther Matiko, Salome Makamba, Tunza Malapo, Jesca Kishoa, Annatropia Theones, Asya Mohammed na Stella Fiao.
Matiko aliliambia gazeti hilo hawezi kuzungumzia suala hilo badala yake asikilizwe akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji.
Spika wa Bunge, Dk Tulia alipotoka bungeni baada ya kikao alikataa kuzungumzia suala hilo akisema atazungumza baadaye.
Ijumaa wakati akiahirisha Bunge hadi leo, Dk Tulia aliomba kukutana na Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Madaraka na Maadili ya Bunge, jambo ambalo inahisiwa kuwa huenda kikao hicho kilihusisha suala la wabunge hao 19.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Benson Kigaila alisema amewasilisha barua ya uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho kukubaliana na adhabu iliyotolewa na Kamati Kuu Novemba 27, mwaka jana.
Alisema pamoja na kuiwasilisha barua hiyo bungeni, alipeleka nakala Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Wabunge waliovuliwa uanachama na Baraza Kuu la Chadema ni Halima Mdee, Ester Bulaya, Kaboyoka, Matiko, Kishoa, Malapo, Asya, Theones, Makamba, Fiao, Cecilia Pareso, Agnes Kaiza, Nuzrat Hanje, Grace Tendega, Hawa Mwaifunga, Felista Njau, Sophia Mwakagenda, Kunt Majala na Conjesta Rwamulaza.
Leo Wizara ya Afya itawasilisha bajeti yake, kesho Wizara ya Kilimo na kesho kutwa ni zamu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.