ALIYEKUWA Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwege, Halmashauri ya Wlaya Rorya, mkoani Mara, Issaya Gidwana amefungwa jela miaka mitatu na kutakiwa alipe Sh Mil. 4.9, baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya jinai iliyokuwa ikimkabili.
Hukumu hiyo ilitolewa jana Mei 20, 2022 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Veronica Selemani, akieleza kuwa upande wa mashitaka umethibitisha pasi na shaka kuwa mshitakiwa alihusika na mashtaka yote sita aliyoshtakiwa nayo katika Shauri la Jinai Na. 306 la Mwaka 2020 .
Awali ilielezwa na Wakili wa Serikali, Mwinyi Yahaya kwamba Gidwana, alighushi hundi za shule na kuchukua jumla ya Sh 4,965, 000, zilizotolewa na serikali kwa ajil ya ujenzi wa madarasa kwenye shule hiyo.
"Makosa hayo ni chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Mapitio ya Mwaka 2019," alieleza Yahaya.
Hakimu Selemani amesema baada ya kusikiliza pande zote zinazohusika katika shauri hilo, Mahakama imeridhika kuwa Gidwana alitenda makosa yote sita na amehukumiwa jela miaka mitatu au kulipa faini Sh Milioni 2 kwa kila kosa.
Hata hivyo mshitakiwa huyo hadi shughuli za mahakama zinamalizika jana, hakulipa faini hiyo, hivyo kwenda kutumikia kifungo gerezani.
Licha ya kutumikia kifungo, pia atatakiwa alipe kiasi chote cha fedha alizoshitakiwa kuiba.