Rais Samia Suluhu Hassan amewataka watetezi wa haki za binadamu kuacha mapambano na serikali na badala yake waungane na kufanya kazi kwa pamoja.
![]() |
Rais Samia akipokea Tuzo ya Heshima ya kutambuaa mchango wake katika utetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania |
Vilevile, amewataka kuacha kutetea haki za wanasiasa tu na badala yake wageukie makundi mengine yanayohitaji watetezi kama watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na wanaopoteza maisha kwa ajali za barabarani, pia kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki na wajibu hasa kwa makundi hatarishi kama 'panya road'.
Rais Samia aliagiza hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Alisema wanatakiwa kukaa mezani na kufanya kazi kwa sababu katika uongozi wake hakuna mapambano.
“Nikisikia watu wakija na ule uanaharakati, siwakatazi lakini uanaharakati ‘positive’ (chanya) ndiyo unajenga, kama mna jambo njooni tuzungumze, kuna vyombo vya ulinzi na usalama kaeni navyo mzungumze,” alisema Rais Samia.
Aliwataka kufanya harakati wa haki za binadamu kwa mazingira ya Kitanzania na kuacha kupambana na serikali kusiko na tija.
“Hasa ikizingatiwa nchi ina mama, mama hapambani, njooni tukae tuzungumze,” alisisitiza Rais Samia na kusema Watanzania wanatakiwa kukaa pamoja na kuisuka upya nchi na kuwa na umoja na mshikamano.
“Sasa kama kuna sera ya nchi, unapambana na nani, unapambana na mama? Ukipambana na mama kwa Mungu hakuna baraka,” Rais Samia alisema.
Aliongeza kuwa nchi ina sheria na taratibu za Kitanzania, hivyo wakati wanafanya utetezi wanatakiwa kuzingatia hilo.
Alisema watetezi wakijikita kutetea haki za binadamu, wafanyakazi na wakulima, haki zitarejea na mabadiliko yatafanyika, pia wakosoe pale serikali inapokosea kwa kutumia lugha nzuri.
“Mkitumia lugha mbaya haitakuwa na maana kupatiwa majibu mazuri, ni ‘approuch’ (mbinu) ndiyo inayomata, twende na ‘approach’ (mbinu) nzuri ya kujenga Taifa,” alisema.
Aliwakumbusha hakuna atakayekusaidia kujenga Taifa isipokuwa Watanzania wenyewe kwa kukaa pamoja na kujenga nchi.
Rais Samia pia aliwataka watetezi wa haki za binadamu kuelimisha wananchi kujua kuhusu katiba ili wanapodai Katiba Mpya wajue na haki zao ni zipi katika katiba hiyo wanayodai.
“Ndiyo maana nimesema tuelimishane kuhusu haki na wajibu ili akitokea wa kumkorofisha mwenzie anaposhughulikiwa isionekane ameonewa, bali amefanyiwa hivyo kwa kuvunja haki ya wenzake,” alisema Rais Ramia.
Kuhusu watetezi wa haki za binadamu, Rais Samia alisema kwa muda mrefu walikuwa wamejielekeza kwenye haki za wanasiasa kuliko haki za watoto.
Alisema kuna watoto wanabakwa na kufanyiwa ulawiti lakini hakuna wanaowatetea, pia kuna panya road lakini wanaozungumza hakuna watetezi wa haki za binadamu waliozungumza kuhusu vijana hao kutotimiza wajibu wao kwa kuvunja sheria na hakuna anayezungumza nao.
Alisema kuna ajali za barabarani lakini hakuna anayezungumzia kuhusu watu kupoteza maisha zaidi ya asasi inayojihusisha na ajali za aina hiyo.
Kuhusu malalamiko ya sheria yaliyotolewa na watetezi hao, aliwataka kupataja wapi inapowabana, akisema: “Ninajua moja ya eneo ni uwazi wa fedha mnazopokea kutoka nje na namna mnavyozitumia.”
Alisema wameamua kufanya hivyo kulingana na matakwa ya dunia kuwa, kuwe na taarifa za fedha zinazoingia nchini na matumizi yake.
Alisema ripoti za wafadhili zimekuwa zikitaja fedha nyingi zinazoingia nchini, lakini serikali inakuwa haifahamu chochote kuhusu fedha hizo.
Rais Samia alisema wanataka wafahamu wanachofanya nchini kupitia fedha za miradi wanazopokea kutoka nchini.
Awali, Mratibu Kitaifa wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa, aliiomba serikali kuwasaidia eneo la kujenga jengo la Watetezi, ambalo litatumiwa na watetezi wa haki za binadamu wa ndani na nje ya nchi.
Pia aliiomba serikali kuwa na sheria na sera za kuwatambua watetezi wa haki za binadamu nchini ili kufanya kazi zao kwa uhuru na amani.
Alisema miaka ya nyuma walipitia vikwazo mbalimbali ikiwamo kubambikwa kesi, kuonekana wapinzani na kufungiwa akaunti zao.
Aliishukuru serikali kwa kukubali mapendekezo makubwa ya kimataifa yakiwamo ya watetezi wa haki za binadamu na haki za binadamu.
Katika maadhimisho hayo, Rais Samia alizindua ripoti inayozungumzia hali ya watetezi wa haki za binadamu na asasi za kiraia nchini kwa miaka 10.
Wakili wa THRDC, Leopod Mosha, alisema hali ya watetezi wa haki za binadamu nchini imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka licha ya uwapo wa vikwazo mbalimbali.
Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright, aliiomba THRDC kuendelea kufanya kazi ya utetezi wa haki za binadamu na kusimamia upatikanaji wa haki miongoni mwa jamii.
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shahibu, aliwapongeza THRDC katika kuhakikisha wanasimama na kutetea haki za wanaharakati waliokuwa wakikamatwa katika nyakati mbalimbali.
Alisema wakati wakuadhimisha miaka 10 ni muhimu kupatikana kwa Katiba Mpya ili kujenga misingi ya ufanyaji kazi za watetezi wa haki za binadamu.