Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema atamuomba Rais Samia Suluhu Hassan avunje Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, ikiwa viongozi haowatashindwa kufuata misingi ya kuanzishwa kwa Baraza hilo.
Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani hao Mei 17, Hapi amekemea tabia ya baadhi ya madiwani hao kukumbatia migogoro inayokwamisha miradi ya maendeleo.
RC Hapi amesema kuwa madiwani Saba wanatekeleza mikakati inayolenga kusababisha halmashauri hiyo isitawalike.
“Usiku wa kuamkia leo madiwani hao walikutana kwa siri maeneo ya Sirari, wilayani Tarime kukamilisha mpango wa kumteka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Gerald Ong'ong'a ili kukwamisha kikao hicho ambacho moja ya ajenda ilikuwa kuamua eneo la kujengwa Kituo cha Afya cha Kata ya Rabour.”
Ilifahamika kuwa ajenda hiyo imechochea mgawanyiko wa madiwani hao, baadhi wakitaka kituo kijengwe katika Kijiji cha Makongro, wengine wakitaka kijengwe Kijiji cha Oriyo vyote vya Kata ya Rabour ambayo Diwani wake ni Ong'ong'a.
Hata hivyo jaribio hilo lilishindikana baada ya kundi hilo kuzidiwa kete na mbinu za kiintelijensia na hatimaye Ong'ong'a kuongoza kikao hicho.
Hapi ametoa siku Saba kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Mchopanga kushirikiana na uongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha ujenzi huo unaanza katika Kijiji cha Makongro.
Pia ametaka madiwani hao kuacha maramoja kasumba hiyo, akiwataka wajue inatia doa halmashauri yao na kuiweka kwenye hatari ya kuvunjwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema Februali 25 Mwaka huu waliopelekewa Sh milioni 500 za ujenzi wa Kituo hicho cha Afya ambacho kilitakiwa kukamilishwa ndani ya Miezi Mitatu lakini mpaka sasa ujenzi wake haujaamza kutokana na mgogoro huo.
"Historia inaonesha kila mkiletewa fedha badala ya kutekeleza miradi mnaibua migogoro sasa kwa kasi ya mama (Rais Samia) sijui mmejiandaa kuibua mingogoro mara ngap?,"amehoji Hapi.
Licha ya mpango wa kumteka Mwenyekiti huyo, Hapi amesema mpaka wanaingia kwenye kikao hicho walikuwa wanapungukiwa kura mbili, kufisha idadi ya kura ambazo waliamini wangezitumia kujenga na kupitisha hoja ya kukosa imani naye, kisha wangeingia hatua ya kukosa imani na Mkurugenzi huku wakiamini wanavuwezo wa kumng'oa hata Mkuu wa Wilaya.
Bila kutaja majina yao licha ya kuibuka minong'ono ya kutaka awataje, RC Hapi amewataka waache ubinafsi badala yake wajenge umoja ili kuwaletea wananchi maendeleo, vinginevyo katika uchaguzi ujao watasoma namba.
Ametoa mfano wa zaidi ya Sh milioni 700 za ujenzi wa Ukumbi wa halmashauri hiyo kwamba zilipelekwa Mwaka 2017 na kuibua migogoro, mpaka sasa ujenzi upo hatua ya kumwagwa jamvi la gorofa ya kwanza.