SIKU mbili baada ya mauaji ya Swalha Salmu (26), kutokea jijini Mwanza, wadogo zake wamesimulia mkasa mzima ulivyokuwa kabla ya kifo chake Jumamosi iliyopita usiku nyumbani kwake eneo la Buswelu, wilayani Ilemela.

Mdogo wake wa watu marehemu, Suleira Salmu, amesimulia mkasa mzima na namna alivyoshuhudia dada yake akimiminiwa risasi saba.
Akizungumza jana nyumbani kwao eneo la Kirumba, Suleira alisema siku hiyo, shemeji yake ambaye alikuwa mume wa dada yake alitoka kwenye biashara zake wilayani Ukerewe na kufika kwake saa 1.45 usiku.
Hata hivyo, hakumkuta mkewe nyumbani, lakini muda mfupi naye alifika akitokea nyumbani kwao Kirumba.
Alipoingia chumbani, alisikia wakigombana na mume wake na muda mfupi, mdogo wake akiwa jikoni na mfanyakazi wa ndani walisikia milio ya risasi.
Milio hiyo ilimshtua na kukimbilia ndani, lakini alikuta mlango wa chumbani umefungwa na baadaye akaendelea kusikia risasi zikiendelea kupigwa mfululizo.
Alisema baada ya muda mfupi shemeji yake alifungua mlango na kutoka nje na yeye alipoingia ndani alimkuta dada yake amelala kitandani huku akiwa anatokwa damu nyingi.
Ilimbidi akimbie kuita majirani ili kumsaidia dada yake, lakini walikataa kwa kuwa siku za nyuma shemeji yake aliwakataza kufika kwake kwa madai wao walikuwa wakichangia ndoa yake kuwa na migogoro.
Baada ya kukosa msaada, alikimbia kwa madereva wa bodaboda na kufanikiwa kuwapata wawili, lakini hata hivyo walipofika nyumbani walikataa kumshika marehemu dada yake na kusimama mbali.
Kutokana na kukosa msaada, alisema ilibidi amuombe mama mmoja jirani yake amsaidie na wakaweza kumbeba hadi sebuleni kabla ya kupiga simu kwa baba yake ili aje kuwasaidia.
Baba yake alipofika na watu wengine, walibeba mwili wa marehemu hadi Kituo cha Polisi cha Kirumba kwa ajili ya kuandika maelezo.
Kwa upande wake, mdogo wake wa pili marehemu, Arafa Salmu, alisema dada yake na mume wake walikuwa na ugomvi wa kwa zaidi ya wiki moja na nusu.
Alisema chanzo kikubwa cha ugomvi wao ilikuwa shemeji yake kumwonea wivu wa kupitiliza na kwamba baadhi ya majirani waliwahi kumpigia simu na kumwambia wamemwona mke wake akiwa katika hoteli moja ya jijini Mwanza.
Alisema ugomvi huo ulimalizika na mume aliaga na kurudi katika biashara zake Ukerewe, kabla ya kurudi tena siku ya Jumamosi usiku na kufanya mauaji hayo.
Arafa anasema mara kadhaa dada yake alikuwa akilalamika kwamba mume wake alikuwa akimpigia simu na kumtukana na alikuwa amechoka na matusi hayo.
Mdogo wake huyo anasema wiki moja iliyopita dada yake alipata kazi ya kwenda kupamba maharusi mkoani Shinyanga na kumuaga mume wake.
Hata hivyo, licha ya kumuaga mume wake ambaye alikuwa Ukerewe kwa njia ya simu na dada yake kwenda Shinyanga kwenye kazi hiyo, aliendelea kumpigia simu na kumtukana.
Alisema hali hiyo ya kutukanwa ilimkasirisha dada yake na kuamua kutopokea simu za mume wake na siku ya Jumamosi mume huyo alirudi Mwanza akitokea Ukerewe na dada yake alikataa kwenda kumpokea na gari lake.
Alisema mara kadhaa alikuwa akishuhudia wakipigana nyumbani kwao kwa kuwa alikuwa akiishi nao.
Mama mzazi wa marehemu, Tiba Mohamed, alikiri mtoto wake kuwahi kumsimulia kuhusu ugomvi wa mara kwa mara na mume wake.
Alisema siku ya tukio mtoto wake alienda kumsalimia nyumbani kwao eneo la Kirumba na wakati akiwa huko, alipigiwa simu na mume wake akimuomba awahi kurudi nyumbani ili akampikie chakula cha jioni kwa kuwa alikuwa hakula kitu tangu asubuhi.
Baadhi ya marafiki zake walisema Swalha aliwahi kuolewa na kuachika mara tatu ingawa hawakusema chanzo cha kuachika kilikuwa ni nini.
“Mimi namfahamu marehemu alikuwa rafiki yangu sana amewahi kuolewa mara tatu na kuachika, lakini hakuwahi kuniambia sababu ya kuolewa mara kwa mara na kuachika,” alisema rafiki yake ambaye aliomba jina lake lisiandikwe.
Swalha alipigwa risasi na mume wake na kufariki dunia usiku wa Jumamosi iliyopita baada ya kutokea ugomvi wa mara kwa mara.
Rafiki yake huyo alisema kabla ya mwanamume huyo kufanya mauaji hayo alituma ujumbe mfupi wa simu kwa marafiki zake kwamba alikuwa amepanga kumuua mke wake.
Mwanamke huyo alipigwa risasi saa 2:00 usiku Jumamosi nyumbani kwao eneo la Buswelu ikiwa ni miezi mitano tangu wawili hao kufunga ndoa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ramdhan Ng'anzi, tukio hilo lilitokea nyumbani kwao baada ya kuwapo na mgogoro wa muda mrefu tangu wafunge ndoa yao.
Akizungumza na Nipashe jana Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Mairi Makori, alisema mwanaume aliyefanya mauaji hayo aliyejulikana kwa jina moja la Said mwili wake umeokotwa kando ya Ziwa Victoria ukiwa na majeraha ya risasi.
"Ni kweli mwili wa mtu anayedaiwa kufanya mauaji hayo umeokotwa na kutokana na picha tulizonazo atakuwa ni yeye,'' alisema.
Alisema wanasubiri ndugu zake ili waende kutambua mwili huo.