TAMISEMI YATANGAZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO 2022

0

 MUHULA wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano utaanza Juni 13, 2022 na  wanafunzi wote wametakiwa kuanza kuripoti katika shule walizopangiwa kuanzia Juni 13, 2022.

Kidato cha tano kuanza  masomo rasmi Juni 13

Hayo yamesemwa leo Mei 12, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa ambapo amesema  mwisho ya kuripoti itakuwa Juni 30 2022.

“Wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka 2022 wanapaswa kuanza kuripoti katika shule walizopangwa kuanzia tarehe 13 Juni, 2022.

"Siku ya mwisho ya kuripoti itakuwa tarehe 30 Juni, 2022. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi.

"Na kwa kuzingatia kuwa uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika shule hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule kutokana na ukosefu wa nafasi kwenye shule husika,"amesema.

Amesema jumla  ya Wanafunzi 153,219 wamechaguliwa kujiunga na kidato tano na vyuo vya Ualimu na vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2022 huku

Amesema “Wanafunzi 153,219 wakiwemo wasichana 67,541 na wavulana 85,678 sawa na asilimia 91.8 ya wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari kidato cha tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2022.

"Kwa kuangalia takwimu za mwaka 2022, kumekuwa na ongezeko la wasichana 7,555 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ukilinganisha na mwaka 2021.

"Hata hivyo idadi hii bado ni ndogo kulinganisha na wavulana,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Amesema, ili kukabiliana na changamoto hiyo, wizara inaendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuhakikisha wasichana wengi zaidi wanajiunga na Kidato cha Tano.

Amesema,watahiniwa katika mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2021 waliopata daraja la kwanza hadi la tatu  walikuwa 173,422 wakiwemo wasichana 75,056 na wavulana 98,366.

Kati ya wanafunzi hao, wanafunzi wenye sifa ya kujiunga na Kidato cha tano, vyuo vya Ualimu na vyuo vya Ufundi ni 167,515 wakiwemo wasichana 71,433.

"Idadi hiyo ya wanafunzi wenye sifa imejumuisha wanafunzi wenye mahitaji maalum 508 wakiwemo wasichana 217 na wavulana 291. Hii ni ongezeko la wanafunzi 19,388 kwa kulinganisha na wanafunzi 148,127 waliokuwa na sifa kwa mwaka 2021.

Bashungwa amesema, wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka 2022, ni kutoka Shule za Serikali, zisizo za Serikali, watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima waliokidhi vigezo na waliosoma Nje ya nchi ambao matokeo yao yamefanyiwa ulinganifu wa Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA).

"Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wapo wanafunzi wenye mahitaji maalum 481 ambao kati yao wasichana ni 204. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wanafunzi 41,401 wakiwemo wasichana 17,390 watajiunga kusoma tahasusi za Sayansi na Hisabati na wanafunzi 49,133 wakiwemo wasichana 25,508 watajiunga kusoma tahasusi za masomo ya Sanaa, Lugha na Biashara;

Aidha, Bashungwa amesema wanafunzi 1,880 wakiwemo wasichana 757 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vitatu vya Elimu ya Ufundi ambavyo ni Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Usimamizi na Maendeleo ya Maji (WDMI).


Wakati huo huo, Waziri Bashungwa amesema fomu za maelezo ya mahitaji ya kujiunga na kidato cha tano kwa shule zote zinapatikana kwenye tovuti ya OR-TAMISEMI kupitia kiunganishi cha www.tamisemi.go.tz na kwa wale waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika Vyuo walivyopangwa.

Aidha, "Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2022 inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz na Baraza la Taifa la Elimu ya Mafunzo ya Ufundi ya www.nacte.go.tz

Amesema,wanafunzi 2,294 wakiwemo wasichana 1,127 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Afya ngazi ya Stashahada;

Pia amesema,wanafunzi 2,674 wakiwemo wasichana 1,366 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ualimu ngazi ya Stashahada ya Sayansi, Hesabu na TEHAMA.

Wanafunzi 6,457 wakiwemo wasichana 3,168 wamechaguliwa kujiunga na Astashahada ya Elimu Maalum, Awali, Michezo, Msingi na Ualimu wa Shule zinazofundisha kwa kutumia Lugha ya Kiingereza (English Medium).


Amesema,wanafunzi 49,089 wakiwemo wasichana 18,019 wamechaguliwa kujiunga na kozi mbalimbali za Astashahada na Stashahada (Certificate and Ordinary Diploma) katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top