Wanawake watano wauawa, wanyofolewa sehemu za siri

0

Wanawake watano wilayani Masasi wameuawa kikatili na watu wasiojulikana huku watatu kati yao wakikutwa sehemu zao za siri zimenyofolewa.

Mauaji hayo yamefanyika katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, hatua ambayo imesababisha wananchi kuingiwa na hofu juu ya usalama wao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Claudia Kitta, alisema amesikitishwa na mauaji hayo ambayo yameonyesha taswira mbaya hasa kutokana na wanawake kuuawa na kunyofolewa viungo vyao.

“Inasikitisha kuona kwamba ndani ya miezi mitatu, wanawake watano wamekutwa wameuawa katika maeneo tofauti. Hali hii inasikitisha na inatishia usalama wa wananchi,” alisema Kitta ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

Alisema jambo ambalo linashangaza ni kwamba aina ya mauaji ni moja huku sababu zikiwa hazijafahamika na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi bado linaendelea na uchunguzi

Kutokana na mauaji hayo, Kitta alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inaendelea kuimarisha ulinzi ikiwa ni pamoja na kulinda mali za wananchi na kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa.

Kitta aliwataka wananchi wilayani hapa kushirikiana na polisi kuhakikisha wahusika wa matukio hayo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Alisema njia ya peke ambayo pia inaweza kutumika katika kuimarisha ulinzi na usalama ni kuanzisha ulinzi shirikishi ngazi za kata, vijiji na mitaa hatua ambayo alisema itasaidia kupunguza matukio ya mauaji yanayoendelea wilayani hapa.

Pia aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi pale wanapowaona watu ambao hawawafahamu kwenye maeneo yao ili wafuatiliwe na kujua uhalisia wake. 

Baadhi ya wananchi waliozungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti walisema vitendo hivyo vimesababisha hofu miongoni mwa wananchi hasa kinamama ambao mara kwa mara wamekuwa wakijishughulisha na uzalishaji mali wanaotoka nyumbani na kwenda kwenye shughuli zao na kurudi. 

Ismaily Kalindimba, Diwani wa Migongo, alisema wanawake wawili kati ya hao wameuawa katika kata yake. Kutokana na mauaji hayo alisema kila kijiji kimeanzisha ulinzi shirikishi, maarufu kama sungusungu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi (ACP) Nicodemus Katembo, alisema hadi sasa watu wawili wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji hayo.

ACP Katembo pia alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo huku akiwataka wananchi watoe ushirikiano ili kuwapata watu zaidi wanaotuhumiwa kujihusisha na mauaji hayo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top