Matukio hayo ni sawa na 65.17% ya jumla ya matukio 1,361 yaliyoripotiwa katika kipindi hicho kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, hii ni kusema kuwa kuna wastani wa watoto 9 walifanyiwa ukatili na kunyanyaswa kila siku mkoani Katavi.
Akizungumza na wanahabari kuelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani itakayofanyika Mei 15, 2022 mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema kuwa visa vinavyoongoza katika takwimu hizo ni ubakaji, ulawiti, kutelekeza familia, ajira za watoto, vipigo pamoja na mimba za utotoni.
“Niombe sana familia kutenga muda wa kukaa pamoja, kujadili mambo ya kifamilia, kufanya uamuzi na mipango ya pamoja,hii inajenga upendo na mshikamano ikiwa ni pamoja na kufahamu maendeleo ya watoto nyumbani hadi shuleni na kuwapeleka sehemu za ibada, ili kujenga jamii imara” amesema Mrindoko.
Amezitaka familia zote kutimiza wajibu wao katika suala zima la malezi, ili kuondokana na wimbi la familia zinazotelekezwa pamoja na watoto wa mtaani.
“Familia ikipata mahitaji muhimu chakula, malazi, mavazi, ulinzi na upendo, naamini kabisa mambo haya ya ukatili hayawezi kutokea” ameongeza.