Waandishi wa habari Kisiwani Pemba wameombwa kuandika habari zinazoibua changamoto za wananchi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari katika Mkutano wa wanahabari Pemba huko Gombani Chake Chake Pemba, Afisa mdhamini kutoka Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Ahmed Abubakar Mohammed, amesema mwandishi ni mtu mwenye dhima kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii, hivyo basi amewataka waandishi hao kufanyakazi kwa bidii na ubunifu ili kuripoti taarifa zenye maslahi mapana kwa taifa.
“Mwandishi wa habari ana majukumu manne kwa wakati mmoja ana jukumu la kuhabarisha, kuelimisha, kukosoa pamoja kuburudisha jamii lakini yote hayo utayafanya endapo utafanyakazi kwa biidi na ubunifu wa hali ya juu bila ya kujali maslahi unayoyapata kwani maslahi mazuri yatakuja kadri unavyoendelea kufanyakazi zenye ubora zaidi” alisema
Aidha amewataka wanahabari hao kufanyakazi kwa ubunifu na upekee ili kazi wanazozifanya ziweze kuwatofautisha na kuleta mvuto kwa wadau wao.
“Kuna waandishi wa habari wanafanya vizuri sana lakini sio hao wanaenda live tu wa television na radio tu kuna na waandishi wa newspaper na majornal tofauti pia ule mfumo wako wa kuripoti zile taarifa zako tengeneza uniqueness” alishauri
Akiwasilisha mada katibu wa Klabu ya Waandishi wa habari Pemba Ali Mbarouk Omar, amewataka wanahabari hao kutambua umuhimu wa wadau wa habari na kujenga nao mahusiano mazuri wadau hao ili kufanya nao kazi kwa mashirikiano zaidi.
“Kazi yoyote ina wadau wake kwa hivyo habari ina wadau wake pia kwa hivyo tunapaswa kuwatambua wadau wetu wa habari, kutambua umuhimu wao na kujenga nao mahusiano mazuri ili waweze kutambua pia nakutujali kwakufanya hivyo tutaweza kufanya kazi kwa mashirikiano makubwa” alisema
Akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa waandishi wa habari Afisa habari kutoka chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Pemba Gaspery Charles Gaspery, amesema mitandao ya kijamii ina fursa nyingi kwa waandishi wa habari, hivyo basi amewaomba wanahabari hao kuitumia mitandao hiyo kuchapisha taarifa zao sambamba na kujiingizia kipato.
“Kama tunavyofahamu kuwa waandishi wa habari tunakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira lakini ujio wa mitandao ya kijamii imetusaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kujiajiri kwakuanzisha majukwaa mbali mbali yanayotupa fursa ya kuweka taarifa zetu na kujiingizia kipato” Alieleza
Kheir Juma Basha ni Afisa habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, amesema waandishi wengi wamekosa uthubutu wa kujitolea kuandika Habari zinazogusa Changamoto za Wananchi na badala yake kujikita katika kuandika Habari za mialiko pamoja na ziara za Viongozi.
Mkutano huo wa siku moja wa uliohusisha Wanahabari Kisiwani Pemba pamoja na wadau mbali mbali wa Habari, umefadhiliwa na Shirika la Habari la Internews kwa msaada wa watu wa Marekani (USAID).
![]() |
Afisa Habari kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Kheri Juma Basha akichangia Mada katika Mkutano wa Wanahabari na wadau mbali mbali wa Habari Kisiwani Pemba. Picha Na, Hassan Msellem. |
![]() |
Baadhi ya Waandishi wa Habari na wadau mbali mbali wa Habari Kisiwani Pemba walioshiriki katika Mkutano wa Wanahabari Kisiwani Pemba. June 21,2022. Picha Na, Hassan Msellem. |
![]() |
Waandishi wa Habari wakiwa katika Picha ya pamoja na Afisa Mdhamin Ofisi ya Makamo ya kwanza wa Rais Zanzibar na baadhi ya Viongozi kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba. |