ALIYEMUAHIDI MWANAFUNZI ATAMUOA AFUNGWA JELA MIAKA (30)

0

Kijana Faison Sanga (19) Mkazi wa kijiji cha Makwaranga Wilayani Makete mkoani Njombe amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi


Mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo mnamo Februari 12, 2022 nyumbani kwake kitendo ambacho ni kinyume kifungu cha 130(1)(2)e na 131 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo 2019 ambapo hukumu hiyo imetolewa Juni 2, 2022

Imeelezwa mahakamani hapo kwamba mshtakiwa huyo bila halali alimpelekea mwanafunzi huyo nyumbani kwake na kumbaka huku akimuahidi kuwa atamuoa ambapo baadaye baba yake mzazi alihisi kwamba binti yake ni mjamzito na kumchukua hadi kituo cha afya kwa vipimo zaidi na ikagundulika kwamba ni kweli ana ujauzito

Chini ya Hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Makete mh. Ivan Msaki upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne ambao ni mwanafunzi huyo, baba yake mzazi, daktari kutoka hospitali ya wilaya ya Makete na askari polisi G.3615 ambapo ushahidi walioutoa mahakamani hapo umeidhihirishia mahakama hiyo kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo

Mwendesha mashitaka wa serikali Inspekta wa jeshi la polisi Benstard Mwoshe ameiomba mahakama hiyo tukufu kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine ambao wamekuwa na tabia ya kukatisha masomo ya watoto wa kike

Akiiomba mahakama imhurumie kabla ya hukumu hiyo kutolewa mshtakiwa huyo Faison Sanga ameiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa yeye kama kijana ana familia inayomtegemea, ambapo Hakimu Msaki amesema mahakama hiyo imemtia hatiani kwa kosa hilo hivyo kumuhukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top