![]() |
Mkuu wa wilaya Makete akitoa elimu Kata ya Isapulano |
Elimu kuhusu umuhimu wa Sensa imeendelea kutolewa kwa wananchi wa kata ya Isapulano ambao wametakiwa kutomficha mtu yeyote wakati wa zoezi hilo.
Akitoa elimu hiyo Mkuu wa Wilaya ya Makete Mh. Juma Sweda amesema hairuhusiwi mtanzania yeyote kufichwa ili asihesabiwe bali kila mwananchi anapaswa kupata haki yake ya msingi kuhesabiwa kwenye zoezi hilo.
Amesema ili Serikali iweze kupanga mipango yake vizuri kila baada ya miaka 10 imekuwa ikifanya zoezi hilo muhimu la kujua ongezeko la watu wake kila kitongoji/mtaa, Kijiji, wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla ili kupata idadi ya watu inaopaswa kuwahudumia.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga vizuri kumhesabu kila raia atakapokuwa amelala usiku wa kuamkia siku ya sensa ambayo ni tarehe 23 Agosti, 2022 kwa kuchukua taarifa zake kamili.
Akiwa Kijiji cha Isapulano, Luvulunge na Ivilikinge Mh. Sweda amesema, “hakikisheni hata ambao huwa wanalala mashambani siku hiyo wawe nyumbani ili wahesabiwe, asitokee mtu wa kumficha mwingine asipate haki yake ya msingi ya kuhesabiwa kama mtanzania…Bajeti yetu inatengwa kulingana na idadi ya watu, hivyo jitokezeni kuhesabiwa” Alisisitiza.
Pia amewasihi wananchi kuendelea kujishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji kiuchumi huku na kuacha kuzurura hovyo mitaani bila kufanya kazi.
Mpaka sasa ametembelea vijiji 79 kati ya vijiji 98 vilivyopo Wilayani Makete kwa lengo la kutoa elimu ya sensa sambamba na kusikiliza changamoto za wananchi.