Kufuatia wanafunzi wa shule ya sekondari Makonde iliyopo mwambao mwa ziwa Nyasa wilayani Ludewa mkoani Njombe kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitanda mabwenini ,Taasisi ya Kifedha ya NMB imeguswa na hali hiyo na kisha kuamua kutoa msaada wa vitanda 40 vyenye thamani ya mil 6.9 vitakavyolaza wanafunzi 80 shuleni hapo huku lengo likiwa ni kuchagiza ukuaji wa elimu nchini.
Msaada huo ni muendelezo wa kurejesha kwa jamii faida inayopata benki hiyo ambapo katika wilaya ya Makete imetoa msaada wa bati 200 zenye thamani ya mil 8.5 kwa ajili kufanikisha ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Ivilikinge ambacho kinatumia jengo dogo lisilo na sifa kutia huduma za afya hali ambayo imekuwa ikisababisha mrundikano wa wagonjwa.
'Hii misumari isipotee lakini haya mabati msiyaibe,sababu mkiyaiba mnakaribisha polisi kuja nyumbani kwenu' amesema Dc Sweda
Wakizungumza mara baada ya makabidhiano wakuu wa wilaya za Ludewa na Makete pamoja na ofisa elimu sekondari Ludewa wanasema misaada hiyo inakwenda kuwa muarobaini wa huduma za afya Ivilikinge na kwa wanafunzi wa Sekondari ya Makonde waliokuwa wakilazimika kutandika magodoro sakafuni na kulala na kisha kutoa onyo kwa watakaoingia tamaa ya wizi.
Zikiwekwa bayana sababu za kuigusa Shule ya Makonde na mradi uliyoibuliwa na wananchi wa Zahanati ya Ivilikinge, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu NMB-Straiton Chilongola na Afisa Mahusiano Kanda Hamfrey Kahaya wanasema ni huduma duni za kijamii zilizopo na kisha kueleza mikakati iliyowekwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini.
Baadhi ya wanufaika wa misaada hiyo akiwem Yona Tweve na Sanday Deogratus wametoa hisia zao kwa kushikwa mkono katika mazingira magumu na benki hiyo.