DC MAKETE AWATAKA MAAFISA UGANI KUTUMIA PIKIPIKI WALIZOPEWA NA SERIKALI KUWASAIDIA WAKULIMA

0

 Mkuu wa Wilaya ya Makete Mh. Juma Sweda amewataka Maafisa Ugani Wilayani Makete kufanya kazi na wakulima kwa lengo la kuwasaidia kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao.

Amesema hayo wakati wa makabidhiano ya pikipiki 69 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao leo tarehe 20 juni 2022 kwenye ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Makete.

Mh. Sweda amesema maafisa ugani hao wanapaswa kutumia pikipiki hizo kwa kuzingatia maadili ya utumishi na kuhakikisha lengo la Serikali linatimia kwa kuwahudumia wananchi.

“Niwasihi maafisa ugani wote matumizi ya pikipiki hizi yawe sahihi na tukibaini unafanya kazi ya kubeba abiria badala ya kwenda shambani kuwahudumia wakulima, hapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako”

“Asilimia 70 ya watanzania tunategemea kilimo ambacho ndio uti wa mgongo kwenye Taifa letu, Rais Samia Suluhu Hassan ameona umuhimu wa kuwasaidia wakulima sasa tafadhali msimuangushe kwenye jambo hili” ameongeza Mh. Sweda

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete Ndg. William Makufwe ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kugawa pikipiki hizo kwa maafisa ugani nchini.

“Pikipiki hizi zinagawiwa kwa maafisa ugani 69 wote ndani ya wilaya yetu lakini hapo awali tulikuwa na pikipiki 21 tu, napenda kumshukuru Rais kwa kuwajali maafisa ugani ambao sasa wataweza kuwafikia wakulima tena mkulima mmoja mmoja ili kujua changamoto zao, kuwapa ushauri na melekezo sahihi ya kilimo katika Wilaya yetu na maeneo mengine”

Awali akisoma taarifa fupi Afisa kilimo Wilaya ya Makete Ndg. Aniseti Ndunguru amesema Wizara ya Kilimo imetoa pikipiki hizo ikiwa na lengo la kuwawezesha maafisa ugani ili waweze kuwafikia wakulima na kutoa elimu ya kilimo bora.

“Tunatarajia tutapata takwimu sahihi za uzalishaji, kilimo chenye tija na biashara huku tukitarajia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya Kilimo kwa asilimia 10 mpaka ifikapo mwaka 2030 kwa uimarishaji unaofanywa na serikali upande wa Kilimo”

Afisa Ugani Kata ya Itundu ndg. Steven Ngoloka kwa niaba ya maafisa Ugani Wilaya ya Makete ameishukuru Serikali kwa kugawa pikipiki hizo ambazo amesema zinakwenda kubadilisha kilimo kwa wanamakete kuanzia sasa.

“Pikipiki hizi zitatufanya tufike kwa wakulima wengi zaidi, haraka na kuweza kuwasikiliza wakulima wetu changamoto zinazowakabili na kuzitatua mapema, tunaishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wetu kwa wakulima na tuihakikishie Serikali kuleta mapinduzi makubwa kwenye Kilimo”

 

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top