Mkuu wa Wilaya ya Makete Mh. Juma Sweda amemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya ujenzi wa barabara ya GS kufika ofisini kwake Ijumaa tarehe 17 Juni 2022.
Agizo hilo ni la kutaka kufanya makubaliano ya namna ya kushughulikia barabara alizopewa tenda ya kujenga mapema wakati mvua zimepungua kwenye maeneo mengi Wilayani Makete.
Mh. Sweda ametoa agizo hilo akiwa Kijiji cha Ibaga Kata ya Mang’oto wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho na kupokea kero kubwa ya changamoto ya ubovu wa barabara kutoka Mang’oto mpaka Ibaga.
“Mhandishi wa TARURA bwana Peter John Kawogo hakikisha unamwambia mkandarasi aliyepewa barabara hii kuijenga anafika ofisini kwangu ijumaa wiki hii ili tukubaliane afike haraka hapa kujenga barabara hii yenye wingi wa mahandaki”
“Mmewasikia wananchi hapa wakilalamika na ubovu wa barabara hii na mimi nimepita leo kwa mara ya pili ni mahandaki na siyo barabara tena, ingekuwa mvua tusingefika hapa…kwa hiyo lazima tuwasaidie wananchi hawa”.
Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Makete Ndg. Peter John Kawogo amesema maagizo ya Mkuu wa Wilaya yatafanyiwa kazi kwa kuwa tayari Serikali imeshatoa fedha Milioni 186 kwa ajili ya ujenzi huo na kwa mwaka wa fedha ujao imetenga milioni 74 na hivyo kufanya Milioni 260 kwa ajili ya ujenzi wa Kilomita 12 kutoka Mang’oto mpaka Ibaga
“Hii ndio barabara mbaya kwa Wilaya ya Makete, Serikali imetenga fedha milioni 260 kwa ajili ya kutatua changamoto kubwa ya barabara ya Mang’oto-Ibaga kwa hiyo hili jambo Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya Serikali imeliona na mkandarasi atafika ofisini kwako kama ulivyo agiza”.
Wananchi wa kijiji cha Ibaga wamesema barabara hiyo imekuwa ikijifunga kipindi cha masika na hivyo kupelekea kushindwa kusafirisha abiria, viazi, mkaa, mbao na mazao mengine ya kibiashara na kusababisha kuzorota kwa shughuli za kiuchumi.