JAMII YAKUMBUSHWA KUWAKUMBUKA WATOTO WALIOPO MAHABUSU

0

 JAMII imetakiwa kutowachukulia watoto waliopo katika mahabusu kuwa ni watoto wahalifu na wenye makosa ambayo hawawezi kuungana na kukaa na watu wengine katika kujijenga kimaadili.

Rai hiyo imetolewa jana na Diwani wa Vitimaalum Jiji la Dar es Salaam,Beatrice Nyamisango wakati wa kusherekea maadhimisho ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Mahabusu ya Watoto Upanga.

Nyamisango amesema jamii inapaswa kuondoa imani hiyo na kuona watoto hao ni kama watoto wengine ambao wanatakiwa kupewa haki zote wanazopewa wengine kwani watoto hao ni wale ambao wamekuwa na makosa ambayo wakifundishwa na kuelekezwa wanaweza kurudi uraiani.

Amesema hawa wengi wao walioopo katika mahabusu ni watoto walioishi katika mazingira hatarishi, wengine mazingira magumu  na hali hiyo inatokana na watoto hao kutopata malezi yaliyokuwa bora kutoka kwa walezi au jamii inayowazunguka   yanayoendana na dunia iliyopo.

“Watoto wengi walioletwa hapa  wamepelekea kupata madhira ya aina mbalimbali na aina ya watoto hawa  ni wale watoto wanaotumika katika matendo maovu kama unyang’anyi,madawa ya kulevya na wengine wale waliokosa malezi ya kimaadili kutoka kwa wazazi wao,”amesema na kuongeza

“Licha ya watoto hawa kuwa ndani ya mahabusu lakini wanafanya shughuli mbalimbali na wanajifunza mambo mbalimbali hata ya kijasiliamali ambapo wakitoka hapa wanaweza kwenda kujiendeleza katika kutimiza ndoto zao,”amesema

Kwa Upande Wake Mwenyekiti wa Mahabusu ya Watoto Upanga Mashariki kwa mujibu wa taratibu  za sheria na ustawi wa jamii,Grace  Ndalama  amesema kwa sasa mahabusu hiyo imeweza kubadilika kwa kiasi kikubwa na kutokuwa na msongamano wa watoto wengi kama miaka ya nyuma.

Amesema watoto wamekuwa wakipewa ushauri na nasaha,kujifunza kazi za mikono na masuala ya ujasiriamali na kuhakikisha wanarudi kuwa watoto wazuri na wenye maadili mema.

“Wito kwa jamii mtoto  akikosa wengi wanawaita manunda na wakati mwingine wanasema  waache wafungwe,hapana hawa watoto wote ni sawa mbele za Mungu na mbele ya jamii hata kama amekosa ni vema kuwarekebisha na kuwarudisha katika maadili mazuri,”amesema

Naye Meja wa Kituo hicho,Darius Kalijongo ameshukuru wadau mbalimbali wanaojitokeza kusaidia watoto wanaoshi katika kituo hicho kwani wanaonyesha upendo wa hali ya juu.

“Tunashukuru watu mbalimbali mliokuja kusherekea siku ya mtoto wa Afrika na watoto wetu wa mahabusu ya hapa Upanga hawa ni watoto kama watoto wengine wanapaswa kupendwa na kujaliwa,”amesema

Aidha  Mwanaharakati wa watoto na haki za watu wenye ulemavu,Sylivia Ruambo amesema wameungana na mataifa mengine kusherekea siku hiyo ya mtoto wa Afrika kwa kuwatia moyo ili nao wajue  kuwa jamii inawapenda licha ya kuwa ndani ya mahabusu. “Watoto hawa ni wetu tuwapende tuwajali na wapo hapa kwaajili ya kutengenezwa ili wakitoka hapa wawe wanajamii wenye tija,”amesemaTags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top