JELA KWA KUJARIBU KUUA KWA KUMCHOMA KISU MWENZAKE WAKINYWA POMBE

0

 MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza iliyoketi Geita, imemhukumu Maziku Faida (52), kutumikia kifungo cha nje mwaka mmoja kwa kosa la kujaribu kuua kwa kumchoma mtu kisu tumboni hadi utumbo kutoka nje.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Liliani Itemba, baada ya mshtakiwa huyo kukiri kosa lake.

Awali, Jaji Itemba alimwambia Wakili wa Serikali, Janeth Kisibo, kumsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali.

Wakili Kisibo alidai kuwa Septemba 19, 2016 mshtakiwa akiwa na mlalamikaji, Majuto Bangaya, wakinywa pombe, mlalamikaji alimkuta mshtakiwa akiwa amekalia kiti chake na alipomwomba atoke alikataa kitendo kilichosababisha waanze kupigana na mshtakiwa alipozidiwa nguvu alichukua kisu na kumchoma mlalamikaji tumboni.

Wakili alidai tukio hilo lilisababisha wasamaria wema wamsaidie majeruhi kumpeleka Kituo cha Polisi Geita na kupewa fomu ya PF3 kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya Geita.

Alidai pia, mshtakiwa alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi na baada ya mahojiano alifikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Jaji Lilian alimuuliza mshtakiwa kama maelezo hayo yana ukweli, ndipo alipojibu kuwa ni kweli.

Kitendo cha mshtakiwa kukiri kosa, Jaji Lilian alisema mahakama inamtia hatiani kwa kosa la kujaribu kuua bila ya kukusudia.

Mshtakiwa huyo aliyekuwa akitetewa na Wakili wa kujitegemea Nestory Kuyula, aliomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa sababu ni kosa lake la kwanza pia ana familia pamoja na ndugu wanaomtegemea.

Jaji Lilian alitupilia mbali utetezi huo kumhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja huku akitakiwa kutotenda kosa lolote ndani ya mwaka mmoja.

Aidha, alisema kama kuna upande wowote ambao haujaridhika na hukumu hiyo, rufani ipo wazi.

Akisoma hati ya mashtaka jana Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Mwanza, Josephine Mhina, alidai kuwa Septemba 19, 2016 majira ya saa mbili usiku eneo la Mkoani, Kata ya Kalangalala mkoani Geita, mshtakiwa alijaribu kumuua Majuto Bangaya kwa kumchoma kisu tumboni na utumbo kutoka nje.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)
Youtube Channel Image
Henrick Idawa Subscribe To watch How to Earn Money

 

 




#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top