Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya zuio la kuondolewa Bungeni ya Wabunge 19 wa Chadema akiwemo Halima Mdee yaliyowasilishwa baada ya chama hicho kutangaza kuwavua uanachama, pamoja na kutupilia mbali maombi ya msingi ya kutaka kupewa kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa Uanachama.
Chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kupitia kamati kuu yake kiliwavua uanachama wanachama wake hao 19 walioapishwa kuwa Wabunge wa viti Maalum wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Baada ya kuvuliwa ubunge walikata rufaa Baraza kuu la chama hicho ambacho ni ngazi ya juu ya maamuzi ya ndani ya chama.
Hata hivyo maamuzi ya mwezi Mei, 2022 Baraza Kuu la Chama likaunga mkono maamuzi ya kamati kuu ya chama hicho ya kuwafukuza uanachama wabunge hao 19, miongoni mwao ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake BAWACHA Halima Mdee.
Baadae walienda Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Baraza Kuu, na kuomba zuio la muda la ubunge iliyotolewa maamuzi yake leo.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mbunge anapaswa kutokana na chama cha siasa, hivyo wabunge hao huenda wakapoteza ubunge wao, iwapo Spika wa bunge atapata taarifa rasmi na kutekeleza maamuzi ya mahakahama.
Mzozo wa nafasi za kibunge kwa wabunge hao zilianza mara tu baada ya uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2020, ambapo Chadema ilipinga matokeo na ‘kususa’ kupeleka majina ya wabunge wa viti maalumu kwa kile ilichoeleza kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi, uliompa ushindi hayati John Magufuli.
Hata hivyo, wabunge hao, walitangazwa na aliyekuwa spika wa bunge, Job Ndugai kama wabunge wa viti maalumu wa Chadema, lakini chadema ilikana kuwatambua, ikisema haikuwasilisha jina lolote kwa nafasi za wabunge hao.
Tangu kuapishwa kwao Novemba 24, mwaka 2020 wabunge hao waliendelea kuhudhuria bungeni, huku kukiibua mjadala juu ya uwepo wao bungeni na kulipwa na fedha za umma, wakati chama kiliwafukuza.