Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewawekea pingamizi mahakamani makada wa zamani 19 wa Chadema na wabunge wa viti maalumu, waliovuliwa uanachama wa chama hicho, waliofungua maombi ya kibali cha kupinga kufukuzwa uanachama wao, huku kikiwasilisha hoja sita.
Pingamizi hilo lilisikilizwa Jumatatu Juni 13, 2022 na Jaji John Mgetta, ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote alipanga kutoa uamuzi Juni 22, 2022.
Wabunge hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee walifungua maombi Mahakama Kuu, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema, wakiomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kuhusi uamuzi huo wa kuvuliwa uanachama.
Sambamba na maombi hayo, pia wamefungua maombi ya zuio la muda dhidi ya ubunge wao kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi yao ya kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama wao.
Mdee na wenzake walichukua hatua hiyo baada ya uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao za kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho, kuwavua uanachama.
Hata hivyo, jopo la mawakili wa Chadema likiongozwa na Peter Kibatala lilishusha hoja sita, ambapo hoja moja ilikataliwa dhidi ya wadai hao.
TAZAMA VIDEO HII KAMA HUJATAZAMA BADO