Na;HASSAN MSELLEM, PEMBA
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Matar Zahor Massoud amewaomba wananchi kutoa taarifa endapo kutakuwa na mtendaji au mamlaka yoyote ambayo itajaribu kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kupambana na kesi za udhalilishaji.
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Matar Zahor Massoud akiteta na baadhi ya watendaji wa Serikali wanaokwamisha juhudi za Serikali katika kupambana na Vitendo vya udhalilishaji. |
Ametoa ombi hilo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika huko Gombani Chake Chake Pemba, amesema kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji kunarudisha nyuma juhudi za Serikali za kuwapatia Watoto haki yao ya elimu pamoja na kutimiza ndoto zao.
‘’Niwaombe wananchi wote endapo unahisi kuna mtendaji wa Serikali au Mamlaka ambayo inazorotesha mwenendo wa kesi nawaomba toeni taarifa ofisini kwangu nitajua vyakumshughulikia” alisema
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema kutoka mwezi June 2021 hadi June 2022 takriban kesi 130 za vitendo vya udhalilishaji zimeripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba, hivyo basi ameahidi kupambana dhidi ya vitendo hivyo ili viendelee kukithiri ndani ya Mkoa Huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amewaomba wazazi na walezi kuhakikisha wanawapatia haki ya elimu watoto wao ili waweze kujikomboa na maisha ya baadae.
Afisa Mdhamin Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohammed Nassor Salim, amesema waathirika wakubwa wa vitendo vya udhalilishaji ni wanafunzi hususan wanaosoma Skuli za msingi, hivyo basi amewaomba waalimu, wazazi pamoja na walezi kuwa karibu na watoto hao ili kuhakikisha wanawakinga na vitendo hivyo.
‘’Niwaombe waalimu,wazazi pamoja na walezi kuwa karibu mno na watoto wao ili kuhakikisha tunawakinga na vitendo vya udhalilishaji yani mzazi anatakliwa afahamu muda wa mtoto wake kwenda skuli na muda wa kutoka lakini wa waalimu nao wanapaswa kutambua mwanafunzi gani kaja shule na nani hakuja ili kuhakikisha usala wao” alitoa rai
Nae Mratibu kutoka Kituo cha huduma za Sheria Zanzibar upande wa Pemba Safia Saleh Sultan, amesema licha juhudi zilizochuliwa kupambana na vitendo vya udhalilishaji lakini kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi juu ya uwepo wa watendaji wasio waadilifu, ajambo ambalo linapelekea baadhi ya wananchi kutokuwa na imani na vyombo vya Sheria.
“Mheshimiwa mgeni rasmi licha ya mikakati, Sera na sheria zinazotungwa za mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji lakini bado kuna wimbi kubwa la wananchi wanaolalamikia uwepo wa baadhi ya watendaji katika vyombo vya Sheria wasio waadilfu na wapendwa rushwa” alieleza
Ameongeza kuwa, licha ya juhudi za Serikali za kupambana na vitendo vya udhalilishaji lakini bado kuna changamoto kwa baadhi ya Sheria ambazo zinaonekana kukinzana na mazingira halisi, jambo ambalo linapelekea kuongezeka kwa matendo hayo.
“Kwa mfano ukiangalia Sheria Nambari 6 ya mwaka 2011 ambayo imewapa mwanya watoto wa kike ambao wanafanya makosa kutokutiwa hatiani lakini pia sheria kutaka kuanzishwa kwa vituo vya kurekebisha tabia vituo ambavyo mpaka sasa havijakuwepo kwa upande wa kisiwa cha Pemba” alifafanua
Tatu Abdalla Msellem ni Mratib wa jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE) amesema jumuiya ya Tujipe ni miongoni mwa jumuiya ambazo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupigania haki za watoto na wanawake Kisiwani Pemba ili kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu, kazi pamoja na Uongozi.
Kilele Cha Maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kila ifikapo June 16 kila mwaka.
Siku ya mtoto wa Afrika ilianzishwa rasmi 1991, na Umoja wa Afrika baada ya maandamano yaliyofanyika Mjini Soweto-Afrika Kusini lenye lengo la kupinga aina ya elimu duni ya kibaguzi waliopewa watoto wa kiafirka na Serikali ya Kibeberu, pamoja na kuitaka Serikali ya Wazungu kuwapa ruhusa ya kufundishwa kwa kutumia lugha zao wenyewe ambapo mamia ya watoto walipigwa risasi na kuuawa na wengine kujeruhiwa vibaya.
![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, akiwaomba wazazi na walezi kuwapeleka Skuli watoto wao kupata haki ya msingi ya Elimu ili iweze kuwakomboa kwa Maisha ya baadae. |
![]() |
Baadhi ya wanafunzi Kisiwani Pemba Walioshiriki Kilele Cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika,, nakuwa walioshiriki Kilele Cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Africa. Ahsante. |
TAZAMA VIDEO HII YA WIMBO HUU KUTOKA KWA BIBI CHALLA ~HAVALLA