Jaji mstaafu wa mahakama ya rufani nchini Robert Makaramba ameishauri Serikali kufanyia kazi marekebisho ya vifungu vya sheria namba 13 na 17 vilivyopo katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kufuatia vifungu hivyo kuonekana kupingana na harakati za kukomesha ukatili wa kijinsia hasa katika ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikirejesha nyuma jitihada za mtoto wa kike katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu.Jaji mstaafu wa mahakama ya rufani nchini Robert Makaramba
Jaji mstaafu makaramba amesema kutokana na mapungufu hayo hakuna haja ya kubatilisha sheria yote isipokuwa vifungu tajwa ambavyo ni 13 na 17 vilivyo shindwa kuainisha umri sahihi wa mtoto wa kike wa kuolewa huku akiwatoa hofu wana harakati wa masuala ya mtoto wa kike kuwa licha ya bunge kuchelewa kutekeleza maamuzi ya mahakama bado kisheria ni kosa mtu kuoa mtoto chini ya umri wa miaka 18 kufuataia mahakama kuamuru vifungu hivyo vibatilishwe.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative's Bi Rebecca gyumi akizungumza na wadau mbalimbali wa masuala ya harakati za mtoto wa kike katika kusherekea siku ya mtoto wa afrika amebainisha kuwa wapo tayari kurejea tena mahakamani kushinikiza utekelezaji wa maamuzi ya mahakama ya kupinga sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kutokana na sheria hiyo kuwa na mapungufu katika baadhi ya vifungu.
Nao baadhi ya wadau wakiwemo wabunge katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania pamoja na wanaharakati wametoa rai kwa Serikali kuunda sheria juu ya ulinzi wa mtoto wa kike badala ya kutoa matamko ili kuepusha mkanganyiko kufutia matamko hayo kubadilika kulingana na utawala .
Yote hayo yanajiri huku hadi sasa ikiwa imesha pita miaka mitatu tangu kutolewa kwa hukumu na mahakama ngazi ya rufani kubatilishwa kwa vifungu vya sheria katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo imelalamikiwa kuruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14.