Kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Makete ndg. Chilomwa Bitulo amewasihi wananchi kujitokeza kuhesabiwa tarehe 23 Agosti 2022 wakati wa zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Bitulo amesema zoezi
hilo litahusisha wananchi wote bila kujali kama mtu ana ulemavu wa viungo au
changamoto ya kiakili, mtoto, mgonjwa au mzee ni lazima ahesabiwe.
Pia amewasihi wananchi
Wilayani Makete kuendelea kupeana hamasa na elimu juu ya umuhimu wa zoezi hilo
litakalofanyika nchi nzima bila kuacha mtu yeyote.
“Kila mwananchi
anatakiwa ashiriki kwenye zoezi la Sensa ya watu na makazi, Serikali itaweza
kupanga vizuri mipango yake na kuweza kutoa huduma mbalimbali kwa watu wake zikiwemo
za afya, kilimo, elimu, miundombinu ya barabara n.k”.
Bitulo ameongeza kuwa
iwapo mtu yeyote atamficha mtu au taarifa za mtu wakati wa zoezi hilo atakuwa
hajamtendea haki mtanzania huyo na kumnyima haki zake za msingi katika nchi
yake.
“Haitapendeza kama kuna
mtu itatokea anaficha taarifa zozote za mtu ambaye atakuwa amelala kwenye
nyumba hiyo usiku wa kuamkia siku ya Sensa ya tarehe 23 Agosti 2022, niombe
wananchi wote tushiriki katika zoezi hili muhimu kwa nchi yetu”.
Sambamba kushiriki
zoezi la Sensa kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Wilaya ya Makete ndg. Bitulo amewaomba wananchi kusimamia miradi ya maendeleo
inayotekelezwa katika maeneo yao bila kuwaachia viongozi pekee.
Amesema ili miradi hiyo
iwe na tija mwananchi anaweza kushiriki bega kwa bega na kuziba mianya ya
rushwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi na kujenga miradi
endelevu yenye manufaa kwa jamii.
“Kila mwananchi
anapaswa asimamie miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kutoa taarifa za
viashiria vya rushwa kupitia namba 113 ili kuwe na miradi inayokidhi vigezo”.