WATUMISHI WA AFYA WATUHUMIWA KUTELEKEZA WAGONJWA MAKETE

0

Mkuu wa Wilaya ya Makete Mheshimiwa Juma Sweda amekemea tabia ya baadhi ya wauguzi Hospitali ya Wilaya ya Makete kutelekeza wagonjwa kwa muda mrefu bila kuwahudumia kwa wakati.


 Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ivalalila kwenye mkutano wa kusikiliza kero zinazowakabili wananchi hao, amesema kumtelekeza mgonjwa bila kumhudumia ni kutomtendea haki na hii inaweza kupelekea mtu kupoteza uhai. 

“Nimesikia malalamiko yenu kuhusu baadhi ya wahudumu kwenye Hospitali ya Wilaya, pale kuna changamoto tena kubwa ambayo Mganga Mkuu Wilaya anapaswa kuirekebisha haraka iwezekanavyo”

 “Pia wananchi kukosa dawa ilihali wananchi wamelipia kadi ya Afya ya CHF, sitaki kusikia tena Habari za wananchi kukosa dawa wakati tulisema wajiunge na tumekusanya hela lakini dawa hakuna…sitaki kusikia hili tena”.

 Wananchi wa Ivalalila wamesema changamoto ya wahudumu wa Afya kutowahudumia wagonjwa kwa wakati imekuwa ni ya muda sasa na kusababisha wagonjwa kuteseka wakisubiri kuhudumiwa Sambamba na hilo wameiomba Serikali kuhakikisha upungufu wa vifaa tiba na dawa unadhibitiwa mapema ili wagonjwa wasipate shida ya kwenda kununua dawa nje ya Hospitali hiyo. 

Mwananchi mmoja akitoa ushuhuda wa kukosa huduma Hospitalini hapo amesema “nilifika na mgonjwa wangu alfajiri nikakaa naye wodini kwa muda wa masaa mawili wakati mganga anasema anakuja na hakuja ndani ya muda huo…baadaye anakuja amejiremba na mimi nilifuata huduma wodi nyingine kumuomba mganga aje kumsaidia mgonjwa wangu” 

Mwananchi mwingine amesema “tumekuwa tukichangia mfuko wa CHF lakini hakuna huduma ya dawa utaipata kwenye Hospitali yetu ya Wilaya ukiwa na kadi ile, wanasema dawa zimeisha kila wakati, sasa ni bora waturudishie hela zetu” 

Mkuu wa Wilaya akiwa Kijiji cha Maleutsi amesikia kilio cha wananchi wa Kijiji hicho kuhusu changamoto ya barabara ya kutoka Maleutsi kuelekea Dombwela Makete Mjini Ambapo Mhandishi wa TARURA Ndg. John Kawogo amesema Serikali imetenga Milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara hiyo muhimu kwa wananchi wa Maleutsi na Iwawa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top