Na;Edwin Moshi Njombe
Mahakama ya wilaya
ya Makete mkoani Njombe imewahukumu wahamiaji haramu 37 kifungo cha mwaka mmoja
gerezani au kulipa faini ya shilingi laki 5 kila mmoja kwa kosa la kuwepo
katika jamhuri ya muungano wa Tanzania bila pasport wala kibali
Washtakiwa hao
Ademasu Mulatu (18) na wenzake 36 raia wa Ethiopia wameshtakiwa katika Mahakama
hiyo baada ya kukutwa Julai 7,2022 katika kijiji cha Kidope wilayani Makete
mkoani Njombe kinyume na kifungu cha 45 (1)(2) cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya
54 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2016
Mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Mh. Ivan Msaki, mwendesha mashitaka wa polisi
Benstard Mwoshe leo Julai 8, 2022 amewasomea washitakiwa wote shitaka lao
ambapo wamekubali shitaka lao la kukutwa hapa nchini kinyume cha sheria
Wakijitetea kabla
ya hukumu hiyo kutolewa washtakiwa hao wamesema walikuwa wakisafiri kuelekea
nchini Malawi na sababu ya kuondoka nchini mwao ni kutokana na maisha magumu
pamoja na ndugu zao kuuawa hivyo wanaiomba mahakama hiyo iwahurumie
Mh. Hakimu Msaki
amesema mahakama hiyo imezingatia utetezi wao wa kuonewa huruma na mahakama
hiyo hivyo akawahukumu Kifungo cha Mwaka mmoja jela ama kulipa faini ya
shilingi laki 5 kila mmoja,na baada ya adhabu watatakiwa kurudi nchini mwao
Washtakiwa hao ni
miongoni mwa wahamiaji haramu 69 waliokutwa Julai 7,2022 katika kijiji cha
Kidope kata ya Iniho wilayani Makete mkoani Njombe baada ya gari walilokuwa
wakisafiria kupata ajali na kusababisha wahamiaji haramu wawili miongoni mwao
kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
TAZAMA VIDEO HII ITAKULIZA WALEMAVU WANAVYOTENGWA KATIKA JAMII