MWANAFUNZI wa Shule ya Sheria Tanzania, Alphonce Lusako amefungua kesi Mahakama Kuu akiomba itamke kwamba raia wa Tanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 ana haki ya kugombea ubunge.
Lusako ambaye pia ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Utetezi kutoka shirika la PLAO amefungua kesi hiyo namba 6/2022 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo, mwombaji anadai kuwa Ibara ya 67(1) inakinzana na ibara nyingine za katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kinachokataza vijana wenye umri kati ya miaka kati ya 18 hadi 21 kuchaguliwa kuwa wawakilishi katika Bunge, huku sheria za uchaguzi zikitoa haki moja ya kupiga kura kwa vijana hao.
"Kifungu cha 67(1) cha katiba kinasema; bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo (a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza,'' alidai.
Alidai kuwa kifungu cha 10 (1) cha Sheria ya Uchaguzi Tanzania kinasema; ili raia wa Tanzania asajiliwe na awe na sifa ya kupiga kura, ni sharti awe na umri wa miaka 18 au wakati wa kupiga kura atakuwa amefikisha umri wa miaka 18.
Alidai vifungu hivyo vinakinzana na katiba inayosisitiza misingi ya demokrasia, uhuru na haki ya kijamii, usawa wa raia wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Pia alidai kifungu cha 13(1)(2)(5) cha katiba kimefafanua juu ya haki sawa na usawa mbele ya sheria bila kuweka masharti ambayo kwa taathira yake ni ya kibaguzi.
Lusako alidai kifungu cha 21(1) cha katiba kinatoa haki ya uhuru wa raia kushiriki shughuli za umma wakati kifungu cha 29(1) cha katiba kinatoa; haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu, na matokeo ya kila mtu kutekeleza wajibu wake kwa jamii, kama zilivyofafanuliwa katika ibara ya 12 hadi 28 ya katiba.
"Mtu anapofikia umri wa miaka 18 anachukuliwa ni mtu mzima na sheria imeweka nadharia kwamba anaweza kufanya maamuzi sahihi kwa kuwa anakuwa amekomaa kiakili na ndio msingi wa sheria za uchaguzi kutoa haki kwa vijana kati ya miaka 18-21 kupiga kura," alidai.
Pia alidai kuwa hakuna hoja za kitafiti zinazoweza kuthibitika kwamba kijana mweye umri wa miaka kati ya 18 na 21 hana utashi hivyo kukosa haki ya kugombea ubunge na kama ndivyo, waliopaswa kupiga kura walipaswa kuwa watu wenye umri wa miaka 21 na sio wenye umri wa miaka 18.
Katika maombi mengine, Lusako anaiomba mahakama hiyo imuamuru AG ndani ya mwezi mmoja baada ya hukumu hiyo awasilishe kwa msajili wa Mahakama Kuu na kwake maelezo ya mwongozo wa hatua zilizochukuliwa kutekeleza hukumu hiyo ambao utakuwa sehemu ya kumbukumbu za mahakama.
Vilevile anaiomba mahakama hiyo imuamuru AG katika kipindi cha miezi mitatu baada ya hukumu aandae na kuwasilishwa kwa wadau (akiwemo yeye) muswada wa mapendekezo ya marekebisho ya kikatiba katika kutekeleza amri ya mahakama.
Pia anaiomba mahakama hiyo imuamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kipindi cha miezi mitatu tangu tarehe ya maoni ya wadau, kuandaa na kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mwisho ya marekebisho ya Katiba kwa majadiliano.