Askari Polisi wa Shehia ya Wambaa kwakushirikiana na kamati za ulinzi shirikishi za shehia ya Wambaa Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, wametunga sheria ndogo ndogo ili kukabiliana na vitendo viovu na vya kihalifu katika shehia hiyo.
Akizungumza na wananchi wa shehia ya Wambaa Mkaguzi msaidizi wa jeshi la Polisi wa shehia ya Chumbageni Suleiman Salim Juma, amesema lengo la wananchi hao kutunga sheria hizo ni kupambana na vitendo viovu na vya kihalifu vinavyojitokeza katika Shehia hiyo.
Nae mkaguzi msaidizi wa Polisi shehia Dodo Pujini na Chambani Ali Juma Abdulla, amesema Jeshi la Polisi Tanzania limeanzisha mfumo wa afisa wa Polisi wenye vyeo vya nyota moja kufanyakazi kwakushirikiana na wanajamii ili kuhakikisha vitendo vya kihalifu vinadhibitwa kwa urahisi.
“Jeshi la Polisi Tanzania limeona kuna kila sababu ya kuanzisha utaratibu wa kupeleka askari wenye vyeo vya nyota moja kila shehia ili kushirikiana na wanashehia husika katika kukabiliana na vitendo vya kihalifu” Ali Juma Abdulla
Kwa upande wake mkaguzi msaidizi wa Polisi shehia ya Wambaa Abdulla Mohammed Abdulla, amewataka wananchi hao kushirikiana na kamati za ulinzi shirikishi katika kuwafichua watuhumiwa pindi wanapofanya vitendo viovu na vya kihalifu.
“Hili sio jukumu la polisi jamii pekee ni jukumu lenu wote, kwahivyo niwasihi mushirikiane na hawa askari jamii katika kuwafichua wahalifu hata kama wakiwa ni marafiki zenu, ndugu zenu na hata watoto wenu ili tuweze kuwachukulia hatua za kisheria” Suleiman Salim
Akisoma sheria zilizotungwa na wana shehia hao Othman Haji Othman, amesema watu ambao watatenda makosa madogo madogo watawajibishwa na uongozi wa shehia na watakaotenda makosa ya makubwa watapelekwa katika vyombo vya sheria.
Miongoni mwa makosa hayo pamoja na adhabu ni pamoja na wanaovaa nguo zisizo za maadili na ukataji wa nywele usiofaa watachapswa viboko vitano (5) kwa kila kosa, wasiosali watachapwa viboko 10 hadi 20, wizi wa kuku faini ni shilingi elfu khamsini, wizi wa nazi faini ni shilingi elfu khamsini, mkungu mmoja wa ndizi faini shilingi laki moja, kuvunja ndoa mtuhumiwa atapelekwa katika vyombo vya sheria, wizi wa muhogo faini shilingi elfu ishirini (20) kwa shina moja, wageni wanaokwenda fukweni awe na kibali cha sheha anakotoka na sehemu husika, kuvaa mavazi ya heshima na kutokukaa na kwa jinsia mbili zinazoweza kufunga ndoa, kwa wanandoa wanatakiwa kuwa na cheti cha ndoa, hairuhusiwi kupika mziki, hairuhusiwi kuendelea kukaa fukweni baada ya saa 12 za jioni.
Akitoa mapendekezo katika mkutano huo Haji Juma Haji, amesema licha wanafunzi walioacha masomo kurudi skuli lakini suala la upungufu wa waalimu maskulini linachangia kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi hao kuacha masomo.
“Kweli wanafunzi ni watoro lakini tukiwachukua wote tukiwapelekea skuli watakwenda fanya nini na walimu ni wachache, kwahivyo kwanza napendekeza kuongezwa kwa waalimu mashuleni” Haji Juma Haji
Nae mwanakijiji Abdalla Mohammed Juma, amewaomba watendaji wa kamati za ulinzi shirikishi kutokutumia mwamvuli wa askari jamii kufanya vitendo vya kihalifu sambamba na kupatiwa mafunzo maalumu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akitoa ufafanuzi juu ya mapendekezo yaliyotolewa na wananchi hao askari mkaguzi msaidizi wa shehia hiyo Abdulla Mohammed Abdulla, ameahidi kuyafanyia kazi mapendekezo hayo ili kuhakikisha ustawi wa wananchi hao unapatikana.
Mfumo huo wa askari wenye vyeo vya wakaguzi wasaidizi kufanyakazi katika shehia umeanza rasmi mwezi February mwaka huu ukiwa na lengo la kushirikiana na wanajamii katika kupambana na vitendo viovu na vya kihalifu.