MJASIRIAMALI MWENYE ULEMAVU WA VIUNGO AOMBA MSAADA WA KUWEZESHWA.

0

Na, Hassan Msellem, idawaonlin.com, Pemba.

Ulemavu ni hali ya kuwa na kasoro ya kudumu ya kimwili au kiakili inayomzuia mtu kufanya shughuli zake za kawaida za kila siku.

Kuna aina mbali mbali za ulemavu kama vile ulemavu wa viungo, ulemavu wa akili, ulemavu wa viungo, Uziwi, ualbino nakadhalika.

Issa Muhammed Ussi

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha mtu mmoja miongoni mwa watu kumi (10) katika jamii ni mwenye ulemavu. Hivyo basi Tanzania inayokadiriwa kuwa na watu 34,569,232 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka (2002) ina watu wenye ulemavu wapatao 3,456,900. Ambapo Watu wenye ulemavu wa viungo wakiwa ni 967, 932 sawa na silimia 28, Wasioona 933, 363 sawa na asilimia 27, Viziwi 691, 380 sawa na asilimia 20 na watu wenye ulemavu wa akili 276, 552 sawa na asilimia 8, watu wenye ulemavu mchanganyiko 138, 276 sawa na asilimia 4 na watu wenye ulemavu mwengine 449, 397 sawa na asilimia 13.

Umoja wa mataifa katika kikao chake cha cha tarehe 20 Disemba 1948 ulipitisha Azimio Nambari 27 (a) ambalo linaeleza kuwa binadamu wote wamezaliwa huru wakiwa sawa katika haki na kustahili heshima. Kwa Azimio hili binadamu ana haki ya ambazo anastahili kuzipata toka kwa jamii na pia ana wajibu kwa jamii. Haki hizo ni kuitumia jamii, na rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo na usalama wake.

Issa Muhammed Ussi 55, mkaazi wa kijiji cha Mtadoda kijiji kinachopatikana Kusini mwa kisiwa cha Pemba, ni mzee mwenye familia mbili na baba wa watoto ishirini na tatu (23) lakini pia ni mtu mwenye ulemavu wa viungo anaejishughulisha na ujasiriamali wa kutengeneza majani ya Chai asilia.

NAMNA ALIVYOPATA UJUZI

Akisimulia namna alivyopata ujuzi wa kutengeneza majani hayo ya chai asilia, amesema ujuzi huo aliupata katika soko la bidhaa Chake Chake kutoka kwa wajasiriamali wenzake wanaojishughulisha na ujasiriamali huo wa kutengeneza majani ya chai asilia.

‘’ Taaluma hii niliipata kwenye soko la wajasiriamali Chake Chake kwa wajasiriamali wenzangu baada ya kuona aina ya majani ya chai wanayotengeneza ndipo na mimi nikapata wazo la kutengeneza majani ya chai asili lakini ukweli ni kwamba siwahi kupata mafunzo rasmi ya utengenezaji wa majani ya chai’’ alieleza

Watu wengi wenye ulemavu hushindwa kuanzisha biashara kutokana na kukosa mitaji ya kuanzisha biashara lakini kwa upande wa mzee Issa anasema shillingi laki moja ndio ambayo aliitumia kuanzisha biashara hiyo.

“Suala mtaji nalo lilikuwa ni changamoto kubwa kwasabau kama unionavyo ni mlemavu na kazi zangu ni ngumu sana nalima mihogo na migomba lakini nilidunduliza hivyo hivyo mpaka nikapata shilingi laki moja ndipo nikaanza kazi” alisema

Majani ya Mronge, Mkunazi na Mchaichai ndiyo majani rasmi ambayo mzee Issa hutumia kutengeneza majani hayo ya Chai asilia, huku akisema kuwa majani hayo ni tiba ya maradhi mbali mbali kama vile presa, Gesi, kuongeza nuru ya macho pamoja na kuondoa sumu mbali mbali mwilini.

Mjasirimali huyu anakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo mashine za kusagia majani, vifungashio, taaluma ya pamoja na soko, hivyo basi ameomba wadau mbali mbali kuweza kumsaidia ili kuondokana na changamoto hizo

‘’Kwakweli nakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mashine ya kusagia nenda Mtambile kusaga, vifungashio ninavyotumia ni ghali sana, kupatiwa taaluma zaidi, soko na hata usafiri na ndio maana sina budi kuuza pakti moja 1200 kutokana na gharama’’ alisema

Lakini licha ya changamoto hizo Mzee Issa anasema kwa siku anaweza kuuza majani majani kumi na tano (15) hadi ishirini (20) kiasi ambacho amesema sio kidogo ukilinganisha na hali yake ya maisha.

Biashara ya majani ya Chai asilia ya mzee Issa imeanza kuwa maarufu maeneo mbali mbali ndani ya mkoa wa Kusini Pemba kama vile Soko la Chake Chake, Mtambile, Wambaa na Mkoani.

MRADI WA VIUNGO PEMBA UWASAIDIAJE WAJASIRIAMALI WENYE ULEMAVU?

Asha Mussa Omar, ni Asifa uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kupitia mradi wa  VIUNGO Pemba, amesema kuhakikisha wajasiriamali wadogo wadogo wanajiingizia kipato zaidi wameandaa mafunzo ya kila mwezi kwa wajariamali hao ili kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

‘’Mradi wa Viungo Pemba una kawaida ya kutoa mafunzo na kuwatembelea kwa wajasiriamali na wadogo  wadogo kila mwezi, hivyo basi kwasasa tunampango wa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo wadogo ishirini kwa upande wa Mkoa wa Kusini Pemba ili kuwaongezea ujuzi zaidi’’ alisema

IDARA YA UWEZESHAJI INAWAWEZASHAJE WAJASIRIAMALI WENYE ULEMAVU?

Haji Khamis Haji ni Mratibu Idara ya Uwezeshaji Pemba, amesema mjasiriamali huyo tayari ameshapatiwa maombi ya kupatiwa mkopo kupitia jumuiya ya Sunday Market ambapo jumla watu wenye ulemavu 20 wameomba mikopo kupitia jumuiya hiyo.

‘’Lengo la Serikali kuanzisha idara hii ya uwezeshaji ni kuhakikisha wajasirimali wote wakubwa na wadogo wanapatiwa mikopo ya fedha ili kuendeleza biashara zao kwakuzingatia vigezo na masharti, kwahivyo mjasiriamali yeyote anaweza kufika ofisini kwetu kujaza fomu na kupatiwa mkopo’’ alifafanua

IDARA YA USAJILI VIKUNDI VYA USHIRIKA PEMBA, IMESAJILI VIKUNDI VINGAPI VYA WATU WENYELE ULEMAVU HADI SASA?

Kwa mujibu wa msajili wa vikundi vya ushirika Pemba Yusuf Seif Yusuf, amesema jumla ya vikundi ishirini na tatu (23) vya watu wenye ulemavu vimesajiliwa katika wilaya zote za Pemba ikiwemo Wilaya ya Mkoani, Chake Chake, Wete na Micheweni.

“Hadi muda huu vikundi vya watu wenye ulemavu ambavyo vimesajiliwa ni ishirini na tatu kwa Pemba mzima ambapo Mkoani ni vikundi vitano (4) Chake Chake sita (6) Wete vikundi nane (7)na Micheweni vikundi saba (6)” alifafanua

Mwadini Juma Ali ni Afisa wa watu wenye ulemavu wilaya ya Chake Chake, amesema bado kuna changamoto kubwa kwa watu wenye ulemavu kuunda vikundi pamoja na kujisajili jambo ambalo linachangia idadi ya vikundi hivyo kuwa vichache.

Alieleza ‘’Bado kuna changamoto kubwa kwa watu wenye ulemavu kuunda vikundi na kujisajili nadhani hii inatokana na kuhisi kuwa watasumbuka kufuatilia usajili na mambo mengine’’

BARAZA LA TAIFA LA WATU WENYE ULEMAVU PEMBA.

Kwa mujibu wa Mritibu kutoka baraza la taifa la watu wenye ulemavu Pemba Mashavu Mabrouk Juma, amesema Mkoa wa Kusini Pemba una vikundi vya wajasiriamali wenye ulemavu 21, Mkoa wa Kaskazini Pemba vikundi 15, sawa na vikundi 36 kwa Pemba mzima.

KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 1977

Sheria ya watu wenye ulemavu ya 2010 nambari 9 sehemu ya 27 (1) inasema "Watu wa umri wowote na jinsia zote walio na ulemavu watakuwa na haki ya kupata elimu, mafunzo katika mazingira jumuishi na faida za utafiti kama watu wengine"

sheria inaonesha wazi usawa baina ya watu wenye ulemavu na wale wasio na ulemavu katika kupatiwa elimu na mafunzo ambayo yatamuwezesha mtu kuweza kupata taaluma fulani itakayomuwezesha kuajiriwa au kujiajiri.

KATIBA YA ZANZIBAR YA MWAKA 1984.

Sheria ya watu wenye ulamavu nambari 9 ya mwaka 2006 (Haki na Fursa)

Sheria Nambari 9 ya mwaka 2006 imetoa haki ya usawa wafursa ya kupata elimu na mafunzo ya  amali ambayo itamuwezesha mtu kuweza kujiajiri au kuwajiriwa bila ya kujali ulemavu alionao.

JE, UONGOZI WA SHEHIA NI KWA NAMNA GANI UNAMTAMBUA MJASIRIAMALI HUYO.

Hamida Ali Khamis ni Sheha wa Shehia ya Minazini, amesema uongozi wa Shehia unafahamu juu ya changamoto zinazomkabili mjasiriamali huyo lakini hakuna kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wenye ulemavu.

“Uongozi wa Shehia unamfahamu mjasiriamali huyo mwenye ulemavu na unatamani kumsaidia lakini hatuna fedha maalumu za kuwasaidia watu wa aina hii lakini tutafanya mpango wa kuzungumza na uongozi wa wilaya ili tuone ni kwa namna gani tunaweza kumsaidia” alieleza

WANAJAMII WANASEMAJE JUU YA WAJASIRIAMALI WENYE ULEMAVU?

Mwandishi wa habari hii alizungumza na baadhi ya wanajamii mbali mbali kuhusiana na suala la ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu, ambapo wengi miongoni mwao wamesema watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kutokuaminiwa na juu ya biashara zao wanazozifanya sambamba na kudharauliwa

“Watu wengi bado hatuamini kuwa mtu mwenye ulemavu anaweza kutengeneza kitu Fulani chenye ubora Fulani hata kama ni kweli hicho kitu kina ubora napia wanadharaulika sana kwakuonekana hawawezi lolote” alisema mmoja miongoni mwa wanajamii hao.

JINSI ALIVYOPATA ULEMAVU

Akisimulia chanzo cha kupata ulemavu huo amesema  ‘’Ulemavu wangu huu niliupata kwa kuonewa mimi nilikuwa mkulima wa ndizi nilikwenda siku moja shambani kwangu muda wa jioni nikiwa na mtoto wangu mdogo anaesoma daraa la saba akaja mwizi akata ndizi  baadaya kukata ndizi nikamuona  nikamuuliza kwanini unanikatia ndizi zangu akanifukuza aliponipata akanipiga mindu (mapanga) nakuniachia ulemavu kama huu’’

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)
Youtube Channel Image
Henrick Idawa Subscribe To watch How to Earn Money

 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top