Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Matar Zahor Massoud, amesema atawachukulia hatua kali za kisheria wanafamilia ambao huwatorosha ndugu zao ambao ni watuhumiwa wa makosa ya udhalilishaji ili kuhakikisha watuhumiwa wa makosa hayo wanadhibitiwa.
Ametoa kauli hiyo katika dua ya
kuiyombea nchi juu ya kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji huko Gombani
Chake Chake Pemba, amesema katika kipindi hiki kumeibuka tabia ya baadhi ya
wanafamilia kuwatorosha ndugu zao ambao ni watuhumiwa wa vitendo vya
udhalilishaji jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi za kupambana na janga hilo.
“Kijana yeyote alitakayefanya vitendo vya udhalilishaji kisha akakimbia naomba
munivumilie wakiwa ni wazazi wake au ndugu zake walioshiriki kumtorosha wote
nawatia ndani” RC
MATAR
Aidha amesema utafiti unaonesha kuwa
watuhumiwa wa kesi za udhalilishaji ambao hutoroka kutoka sehemu moja kwenda
sehemu nyengine huendeleza kufanya vitendo hivyo bila ya kujali alikotoka
kufanya kosa hilo.
“Na utafiti wetu unaonesha hawa
wanaofanya vitendo hivi vya udhalilishaji kisha kukimbia na huko wanakokwenda
huendeleza kufanya vitenda hivyo kwa mfano mtuhumiwa akitoroka Pemba kwenda
Unguja akifika Unguja anaendelea kufanya vitendo hivyo” alisema
Kwa upande wake, Mratibu kutoka Ofisi ya Mufti
Mkuu Pemba Sheikh Said Ahmad Mohammed, amesema miongoni mwa sababu
zinazopelekea kukithiri kwa maasi mbali mbali katika jamii ni waislamu kuacha
mwenendo wa kiongozi wa dini ya Kiislamu Mtume Mohammad s.a.w, hivyo basi
amewaomba waumini wa dini ya kiislamu kufuata mwenendo wa kiongozi huyo ili
kuepukana na maasi hayo.
“Maasi
na majanga yote haya yanayotukumba ni kwasababu tumeachana na mwenendo wa
kiongozi wetu katika imani Mtume Muhammad sallawahu allayhi wasallam” Sheikh
Said Ahmad

Nae Mwenyekiti wa Istiqama For Development
Pemba Mohammed Suleiman Khalfan, amewaomba wazazi na walezi kufuata maelekezo
ya dini ya kiislamu katika malezi ili kuwa na jamii yenye mustakbali mwema.
Mwenyekiti wa Bodi kutoka jumuiya ya
Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE) Sheikh Abdalla Nassor Abdalla, amesema kumekuwa na
tabia mbaya kwa baadhi ya akina mama ambao husimama barabarani kuomba msaada wa
usafiri lakini baada ya kupatiwa msaada huo huwasingizia madereva kuwa
wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji ili kujipatia fedha.
“Mheshmiwa mgeni rasmi sasa hivi nasikia kumezuka mchezo mchafu sana kuna
akina mama ambao hukaa barabrani wakajifanya wanahitaji huduma ya usafiri
ukimpa lifti waanza kupiga makelele kwamba wamebakwa tumefikia pabaya sana” alisema
Kutoka mwezi June 2021 hadi June 2022
takriban kesi 130 za udhalilishaji zimeripotiwa katika vituo mbali mbali vya
Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Dua hiyo ya kuiyombea nchi dhiya ya
maasi na majanga mbali mbali imeandaliwa na jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba
(TUJIPE) pamoja na Ofisi ya Mufti Zanzibar na KUhudhuriwa na viongozi wa
Serikari, dini pamoja na wananchi mbali mbali.