SERIKALI KUSHUGHULIKIA HOJA NA MALALAMIKO YA MADEREVA NA WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRISHAJI NCHINI

0

Serikali imetoa maelekezo ya kisheria (Compliance Order) ili kuwataka waajiri kote nchini kutoa Mikataba kwa wafanyakazi madereva.


Maelekezo hayo ya serikali yametangazwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi kufuatia hoja na malalamiko yaliyowasilishwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini.

“Katika kushughulikia malalamiko na hoja hizo, tulikutana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva kwa lengo la kusikiliza hoja na malalamiko yao tarehe 24 Aprili, 2022, baada ya kupokea hoja hizo, Serikali iliahidi kuzifanyia kazi katika kipindi cha siku 90 na kutoa taaarifa rasmi ambayo ndiyo hii tunayoitoa kwa umma.”

Amesema ifikapo mwishoni mwa mwezi Agosti, 2022 Serikali itaanza kuwachukulia hatua waajiri ambao watabainika kukaidi maelekezo ya Serikali.

Amesema katika kuhakikisha Madereva wanapatiwa Mikataba ya Kazi, Serikali inaendelea na zoezi la kufanya kaguzi zinazoshirikisha wadau wanaoguswa na sekta hii na tayari kaguzi zilifanyika katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na Mbeya ambapo Jumla ya Kampuni 73 zilikaguliwa na kubaini baadhi ya waajiri hawajatoa mikataba kwa Madereva.

Katambi pia amesema kupitia kaguzi zinazoendea kufanyika katika maeneo ya kazi, Serikali itasimamia suala la Madereva kupatiwa hati za malipo ya mshahara (salary slip) kama inavyoelekezwa kwenye Sheria.

Aidha Serikali inawashauri Madereva kufanya makubaliano na waajiri wao kuhusu utaratibu gani utumike kuwalipa mishahara kwani Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura 366 imeruhusu mwajiri na mfanyakazi kukubaliana namna ya kulipana mshahara ama kupitia benki, fedha taslim au hundi, alisema

Aidha Sheria inawataka waajiri wote kuwasajili na kuwachangia wafanyakazi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na WCF) wakiwemo wafanyakazi Madereva.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top