WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu, amewataka wauguzi katika hospitali zote nchini kuweka mkakati mzuri wa kuwahudumia wagonjwa kwa muda usiozidi saa tatu kwa mgonjwa mmoja.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wananchi waliokua wakipata matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
"Watu wanakaa muda mrefu kusubiri kumuona daktari, nimeshamuelekeza mganga mfawidhi waliwekee mkakati, kuanzia ameingia hospital, kumuona daktari na kufanya vipimo kwa kadri inavyowezekana," amesema Waziri Ummy.
Amewashauri wazazi na walezi kuwakatia bima ya afya watoto (Afya Toto Card) kwa ajili ya kuwaondolea gharama za matibabu, pindi wanapougua ama kupata matatizo ya kiafya.
Alisema wakati wanasubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa wote (UHC), ambayo itasaidia wananchi wote bila kujali hali zao za maisha kupata huduma zote za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa, ambapo kutawekwa kiwango nafuu, ni vizuri wakawatia bima.
"Bima ya afya kwa wote itamuwezesha mwananchi yeyote bila kujali hali yake ya maisha na ukiwa na bima hiyo utapata huduma za matibabu pamoja na vipimo kwenye vituo vya afya hadi ngazi ya Taifa," amesema na kuongeza:
"Wakati tunasubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa wote, hivyo ni muhimu wazazi na walezi kuwakatia bima ya afya watoto wao kwa gharama ya Sh 50,400 kwa mwaka na itamuwezesha kupata huduma mpaka ngazi ya Taifa.
"Kwa sasa bima hii sio lazima, lakini nitakutana na wamiliki wa shule zote za sekondari nchini katika kikao chao ili tuweke takwa hili la kukata bima ya afya kwa wanafunzi wa sekondari," alisema Waziri Ummy